Mfarakano wa Rais Abdullahi na Waziri Mkuu Gedi wafikia ukingoni? | Matukio ya Kisiasa | DW | 16.10.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Mfarakano wa Rais Abdullahi na Waziri Mkuu Gedi wafikia ukingoni?

Rais wa Somalia na waziri wake mkuu wamekuwa hawako kwenye maelewano mazuri katika mzozo wa kisiasa ambao yumkini sio tu ukakomesha mfarakano wao wa muda mrefu bali pia unaweza kuipeleka mrama kwa mara nyengine tena serikali ya nchi hiyo.

Rais Abdullahi Yusuf wa Somali kushoto na Waziri Mkuu Ali Mohamed Gedi kulia.

Rais Abdullahi Yusuf wa Somali kushoto na Waziri Mkuu Ali Mohamed Gedi kulia.

Rais Abdullahi Yusuf na washirika wake wakiwemo mawaziri 22 kwa mara nyengine tena wanajaribu kumtimuwa Waziri Mkuu Ali Mohamed Gedi kwa kupitia kura ya kutokuwa na imani naye ambayo inaweza ikapigwa leo hii au hapo kesho Jumatano.

Lakini Gedi ambaye alinusurika na jaribio hilo la kura ya kutokuwa na imani hapo mwaka jana yuko mbioni kuwashawishi wabunge na pia amejaribu kutaka msaada wa koo lake la Hawiye ambalo kwa muda mrefi limekuwa likilalamika kwamba alikuwa sio chaguo lao lakini yumkini wakamuunga mkono dhidi ya koo la kabila la Yusuf la Darod.

Kila mtu anaweza kuaguwa vipi kura hiyo itapigwa huku kukiwepo na repoti za kutumika kwa fedha na upendeleo kwa mujibu wa wabunge kadhaa wa Somalia na wachunguzi wa mambo huko Baidoa kituo cha biashara kilioko kusini ya kati ambapo ndipo lilipo bunge katika ghala lililofanyiwa ukarabati.

Michael Weinstein profesa wa siasa ya sayansi katika Chuo Kikuu cha Purdue huko Indiana nchini Marekani amesema hali hiyo inaonyesha kuibuka kwa mgawanyiko ulioko ndani ya serikali ambao unatishia uhai wa serikali yenyewe na kudhoofisha mno msingi wenyewe wa sera ya mataifa ya magharibi kwa Somalia.

Serikali za mataifa ya magaribi na mataifa makubwa katika eneo hilo zimeshinikiza kuimarisha serikali hiyo ya mpito kama tumaini bora la kuunda serikali ya umoja wa kitaifa nchini Somalia. Majaribio 13 ya kuunda serikali ya kitaifa yaliopita yameshindwa tokea kupinduliwa kwa dikteta Mohamed Siad Barre hapo mwaka 1991.

Gedi na Yusuf ambao wote wawili wameingia madarakani kwa kupitia hila za Ethiopia wamekuwa kwenye mfarakano kwa muda mrefu.Suluhu iliopatikana baada ya kura ya kutokuwa na imani na Gedi hapo mwaka 2006 ilivurugwa mapema mwaka huu wakati viongozi hao walipounga mkono kampuni hasimu zenye kuwania haki ya kutafuta mafuta nchini humo.

Mtaalamu wa Somalia mwenye mafungamano ya karibu na kambi za Gedi na Yusuf amekaririwa akisema kwamba Yusuf ametamka Gedi lazima aondoke kwa njia ya halali au isio halali na jambo hilo sio siri.

Upande wa Yusuf unatowa hoja kwamba kipindi cha Gedi muda wake umemalizika chini ya katiba ya serikali ya mpito wakati Gedi mwenyewe anasisitiza kwamba sheria na wakati viko pamoja naye.

Kutokana na washirika wa Yusuf kumtia mbaroni hakimu mkuu wa mahkama kuu mwishoni mwa mwezi uliopita kwa madai ya rushwa kumefanya kutokuwepo kwa msuluhishi wa kipengele hicho cha sheria.

Aidha Gedi anabakia au anan’goka kile kinachomaanisha kupiga kura hiyo ni kuchelewa kusonga mbele kwa serikali hiyo ya mpito kufikia lengo lake la kujenga taasisi za serikali huku uasi ukiwa umechaga katika mji mkuu wa Mogadishu na mzozo unaozidi kukuwa na jimbo lililojitenga la Somaliland kaskazini mwa nchi hiyo.

Mwanadiplomasia wa taifa la magharibi aliekataa kutajwa jina lake anasema kile wanachotaka ni kwa watu kufanya kazi kuelekea kwenye mwelekeo sahihi lakini kutokana na mambo yalivyo wanaiona hali hiyo kuwa ni maafa.

Kuna wanaona kwamba ni afadhali kwa Gedi akajiuzulu badala ya kuadhiriwa na kura ya kutokuwa na imani.

 • Tarehe 16.10.2007
 • Mwandishi Mohamed Dahman
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/C7hc
 • Tarehe 16.10.2007
 • Mwandishi Mohamed Dahman
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/C7hc

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com