Merz na Trump: Mkutano wa dharura kuhusu Mashariki ya Kati
2 Machi 2026
Ni safari ambayo kwa muda mrefu ilikuwa imepangwa chini ya masharti tofauti kabisa: Jumatatu hii Kansela wa Shirikisho Friedrich Merz anaelekea Washington. Jumanne, mkuu huyo wa serikali ya Ujerumani atakutana na Rais wa Marekani Donald Trump. Katikati ya mvutano unaozidi kuongezeka kuhusiana na Iran na Mashariki ya Kati. Na ajenda ya masuala ambayo imebadilishwa kabisa kutokana na matukio ya sasa.
Awali, Merz alikusudia hasa kuzungumza na Trump kuhusu mzozo mkali wa ushuru wa Marekani. Sasa atalazimika kumweleza rais huyo asiyeweza kutabirika msimamo wa Ujerumani na Ulaya kuhusu mashambulizi ya Marekani na Israel dhidi ya Iran pamoja na majibu makali ya Iran.
Merz: Ujerumani katika "mtanziko” kuhusu vita Mashariki ya Kati
Hadi Jumapili, Merz alikuwa amehakikisha mjini Berlin kwamba Ujerumani iko waziwazi upande wa Marekani na Israel. Alilaani mashambulizi ya Iran dhidi ya baadhi ya mataifa ya Ghuba, dhidi ya kambi za kijeshi za Marekani na bila shaka dhidi ya Israel. Kwa mtazamo wa kisheria wa kimataifa kuhusu mashambulizi ya Israel na Marekani, Ujerumani, kwa mujibu wa kansela huyo, iko katika mtanziko.
Kwa maneno mengine: Kwamba mashambulizi hayo hayajafuata sheria ya kimataifa ni jambo lililo wazi. Lakini, Merz aliendelea kusema: Serikali ya shirikisho inashiriki "hisia ya afueni ya Waajemi wengi kwamba utawala huu wa mullah sasa unafikia mwisho wake.”
Na kwa kuzingatia miongo kadhaa ya majaribio yaliyoshindikana kuishawishi Tehran kulegeza msimamo wake kuhusu mpango wa nyuklia na makombora, huu si wakati wa "kuwakosoa au kuwahubiria washirika wetu.” Hata hivyo, mashambulizi hayo hayakuwa bila hatari, Merz aliongeza.
Nini maana ya "hatua za kijeshi za kujilinda”?
Baadaye, Merz pamoja na Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron na Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer walitoa tamko likisema kwamba mataifa hayo yako tayari kwa "hatua za kijeshi za kujilinda.”
Waziri wa Mambo ya Nje Johann Wadephul alieleza Jumatatu katika mahojiano na Deutschlandfunk kwamba Ujerumani haina nia ya kushiriki katika mashambulizi zaidi: "Kama hatuna nia, basi hatutafanya hivyo. Hatutashiriki katika hilo,” Wadephul alisisitiza alipoulizwa.
Akaongeza: "Kwetu sisi, hilo halimaanishi chochote zaidi ya kwamba wanajeshi wetu wa Bundeswehr, endapo wangeshambuliwa, watajilinda kwa njia ya kujihami.” Wanajeshi wa Ujerumani wamewekwa katika kambi, kwa mfano, nchini Jordan na Iraq.
Mwandishi mkuu wa DW, Michaela Küfner, anaandamana na Merz kwenda Marekani. Anaeleza yanayomsubiri kansela huyo sasa: "Merz anasema hatazifundisha Marekani na Israel kuhusu Iran. Hilo ni sawa na kuachana kabisa na sheria ya kimataifa kama mfumo wa marejeo. Ni mabadiliko ya kihistoria.” Trump atamweleza kile ambacho Marekani sasa inatarajia kutoka kwa Ulaya.
Merz atalazimika kujaribu kuunganisha hilo na mada nyingine muhimu: "Hapo, changamoto yake kubwa itakuwa kuhakikisha kwamba hoja yake muhimu zaidi inasikika na Donald Trump: kwamba Ulaya inataka kukaa tena mezani katika mazungumzo kuhusu Ukraine. Kwa sasa, mustakabali wa Ulaya unajadiliwa bila Ulaya kushirikishwa.”
Matumaini ya sera tofauti ya ushuru
Ikiwa muda utaruhusu, Merz bila shaka atataka pia kuzungumzia sera ya ushuru ya Marekani akiwa Washington. Hivi karibuni, Rais wa Marekani Donald Trump alipata pigo kubwa wakati mahakama kuu ya Marekani, ilipobatilisha kwa kiasi kikubwa sera yake kali ya ushuru, pia dhidi ya Ujerumani na Umoja wa Ulaya.
Merz alitoa maoni kuhusu hilo katika televisheni ya umma, ARD mwishoni mwa wiki iliyopita: "Huu ni uamuzi wa kuvutia, ambao wengi walikuwa wameutarajia, kwamba Mahakama Kuu mjini Washington inaweka mipaka kwa serikali hapa.”
Hata hivyo, kansela huyo alieleza kuwa uamuzi wa mahakama hiyo ya juu ulihusu tu ushuru wa jumla uliowekwa na Trump, si tozo muhimu za kisekta. Na baada ya hukumu hiyo, serikali ya Marekani tayari imepitisha ushuru mpya wa asilimia kumi kwa nchi nyingi kwa msingi mwingine wa kisheria na inatishia viwango vipya vya hadi asilimia 15.
Kuchukua msimamo wa moja kwa moja kunalipa
Sera ya biashara hivyo inabaki kuwa moja ya vipaumbele vya mazungumzo kati ya kansela na Trump. Hilo lilithibitishwa pia na msemaji wa serikali Stefan Kornelius kabla ya mkutano wa waandishi wa habari wa shirikisho mjini Berlin: "Huenda safari hii imefika wakati mzuri, ili kwa msimamo ulioratibiwa wa Umoja wa Ulaya kuzungumza moja kwa moja na rais kuhusu hatua zinazofuata.”
Mwaka uliopita, baada ya kuingia madarakani Mei, Merz alikuwa akichukua tahadhari zaidi katika mahusiano yake na Trump. Aliweza hata kuhesabu kama mafanikio kwamba ziara yake ya kwanza katika Ikulu ya White House ilienda kwa utulivu mkubwa. Baadaye, akiwa Marekani pamoja na wanasiasa wengine muhimu wa Ulaya, alitetea suala la Ukraine. Na mwanzoni mwa mwaka 2026, Waulaya waligundua kwamba inafaa kweli kuchukua msimamo wa wazi zaidi mbele ya rais wa Marekani.
Wakati Trump alipotishia kujaribu kuifanya Greenland, ambayo ni sehemu ya Denmark, kuwa chini ya umiliki wa Marekani, sauti ilibadilika, pia kwa Merz. Ujerumani na washirika wengine wa NATO barani Ulaya waliihakikishia Denmark na watu wa Greenland mshikamano wao. Matokeo yake, Trump aliacha kwa muda kuendeleza suala la Greenland.
Hali nchini Ukraine bado ni ya kutisha
Hata hivyo, suala la Ukraine linabaki juu kabisa ya ajenda ya Merz, licha ya hali inayohusiana na Iran. Hata Rais Volodymyr Zelenskiy sasa anakiri kwamba nchi yake inaweza kulazimika kuachia kwa muda baadhi ya maeneo ya taifa ikiwa silaha zitanyamaza kweli.
Lakini Ukraine inakataa vikali wazo la kukabidhi pia maeneo kwa Urusi ambayo majeshi ya Moscow bado hayajayateka. Vita vya uvamizi vya Urusi sasa vinaendelea kwa miaka minne. Ikiwa Merz atapata sikio la kusikiliza kuhusu mada hii hasa kwa Trump, inaonekana kuwa na mashaka kutokana na maendeleo ya hivi karibuni katika Mashariki ya Kati.