1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mazungumzo ya kuunda serikali yaingia hatua za mwisho

Sekione Kitojo
6 Februari 2018

Chama cha CDU na kile cha SPD vinaingia katika duru ya mwisho ya mazungumzo leo Jumanne(06.02.2018) kufikia makubaliano na kumaliza miezi kadhaa ya mvutano wa kisiasa katika taifa hilo lenye uchumi mkubwa katika Ulaya.

https://p.dw.com/p/2sBBz
Kombobild Koalitionsverhandlungen- Martin Schulz und Angela Merkel

Baada  ya  majadiliano ya  siku  nzima jana  Jumatatu , wajumbe  wa majadiliano  kutoka  chama  cha  Angela  Merkel  na  chama  ndugu cha jimboni  Bavaria cha  CSU  pamoja  na  chama  kinachotarajiwa kujiunga  katika  serikali  ya  mseto  cha  Social Democratic SPD, vitarejea  katika  meza  ya  majadiliano  mjini  Berlin kwa  msukumo wa  mwisho  kupata  makubaliano  kuhusu  kurejea  katika  kile kinachofahamika  kama  "Muungano  mkuu".

Deutschland Koalitionsverhandlungen von Union und SPD
Viongozi wa vyama vitatu muhimu katika mazungumzo ya kuunda serikali mpya. Martin Schulz (kushoto) wa SPD, Horst Seehofer wa CSU(katikati)na Angela Merkel wa CDUPicha: Getty Images/AFP/J. Macdougall

Vyama  hivyo  viko karibu  asilimia 95  kufikia  makubaliano  ya kuunda  serikali, amesema  mjumbe  wa  majadiliano  kutoka  chama cha  SPD leo, na  kuongeza  hatahivyo  kwamba,  makubaliano hayatakuwa  na  maana  ya  "kazi bora".

Licha  ya vuta  nikuvute  iliyopo, mazungumzo  hayo  awali yalikuwa yamalizike mwishoni  mwa  juma , vyama  hivyo  vilionesha matumaini  makubwa  ya  mkutano  wa  leo  Jumanne  utakuwa  ni mwisho  wa  mazungumzo  hayo.

"Bado  nina  matumaini ," alisema  Daniel Guenther , waziri  mkuu wa  jimbo  la  kaskazini la  Schleswig-Holstein  kutokea  chama  cha CDU.

Vyanzo  katika  vyama  hivyo  vinasema  maeneo  yenye  matatizo ni  kutokubaliana  kuhusu  huduma za  afya, sera  za  kazi  na matumizi  ya  ulinzi.

Martin Schulz bei den Koalitionsverhandlungen zwischen SPD und Union
Kiongozi wa SPD Martin SchulzPicha: Reuters/C. Mang

Muungano wa walioshindwa

Julia Kloeckner , naibu  mwenyekiti  wa  chama  cha  Merkel  cha CDU, alisema  anatarajia  mazungumzo  hayo  kwa mara  nyingine tena  kuendelea  hadi  usiku  wa  Jumanne, ikiwa  na  maana yanaweza  kuendelea  hadi  alfajiri  siku  ya  Jumatano ili  kufikiwa makubaliano  ya  kuunda  serikali  kuweza  kuwasilishwa rasmi.

Merkel , ambaye yuko  madarakani kwa  zaidi  ya  miaka  12, anaweka  matumaini  yake  ya  kuongoza  kwa  muhula  wa  nne kwa kurejewa  kwa  muungano  na  chama  cha  SPD  baada  ya uchaguzi   wa  mwezi  Septemba  mwaka  jana  ambapo  ulikiacha chama  chake  bila  ya  wingi  wa  kuweza  kuunda  serikali.

Deutschland Koalitionsverhandlungen PK Angela Merkel
Kansela wa Ujerumani Angela MerkelPicha: Reuters/C. Mang

Lakini  wadadisi  wa  masuala  ya  kisiasa  tayari  wameueleza muungano  huo  kuwa  ni  "muungano  wa  walioshindwa" baada ya vyama  vyote  kupata  matokeo  mabaya  kuwahi  kupatikana  katika miongo  kadhaa  ya  uchaguzi, wakati  chama  cha  siasa  kali  za mrengo  wa  kulia  cha Alternative for Germany AFD kilipata  asilimia 13  ya  kura.

Merkel  mwanzoni  alitaka  kuunda  serikali  ya  muungano  wa vyama  vitatu  na  chama  cha  walinzi  wa  mazingira , Greens, na kile  cha  kiliberali  cha  FDP, lakini  mazungumzo  hayo  yalivunjika kwa  kutupiana  lawama mwezi  Novemba mwaka  jana.

Mwandishi: Sekione  Kitojo / afpe

Mhariri: Iddi Ssessanga