May atoa matumaini kwa raia wa nchi za Umoja wa Ulaya | Matukio ya Kisiasa | DW | 23.06.2017
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

May atoa matumaini kwa raia wa nchi za Umoja wa Ulaya

Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa May ameahidi jana kwamba raia wa nchi za Umoja wa Ulaya hawatofukuzwa Uingereza itakapojitoa katika umoja huo 2019, na amesema hatima yao ni suala litakalopewa kipaumbele.

Mapendekezo ya May katika mkutano wa kilele wa siku mbili ulioanza jana yamekuja katika wakati muafaka ikiwa ni siku chache baada ya kuanza mazungumzo ya Uingereza kujiondoa katika Umoja wa Ulaya yanayojulikana kama Brexit. Kansela wa Ujerumani Angela Merkel ameutaja huo kuwa ni mwanzo mzuri.

"Theresa May amesema wazi kabisa kwamba raia wa nchi za Umoja wa Ulaya ambao wamekuwa wakiishi Uingereza kwa miaka mitano wataweza kubakisha haki zao kamili. Huu ni mwanzo mzuri lakini bado kuna masuali mengine mengi. Sambamba na masuali ya Uingereza kujitenga, kuna masuala ya kifedha yanayohusu suala la Ireland. Ina maana tuna mengi yakufanya kabla ya Oktoba," amesema Kansela wa Ujerumani Angela Merkel.

May amewasilisha wazi vigezo vya haki za raia milioni 3 wa nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya wanaoishi kihalali nchini Uingereza na jinsi wanavyopaswa kulindwa na madhara zaidi yanyotokana na Uingereza kujitenga na umoja huo. May pia ameweka wazi kwamba anataka hatua sawa na hizo zitumiwe kwa raia wa Uingereza milioni 1.5 wanaoishi barani Ulaya. Haki za raia ni suala nyeti kabisa katika mazungumzo yajayo ya Brexit.

Hakuna familia zitakazogawanyika baada ya Brexit

EU Gipfel Emmanuel Macron Angela Merkel und Theresa May (Reuters/F. Lenoir)

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel, Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa May, na Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron wakiwa katika mkutano wa kilele wa Umoja wa Ulaya

Afisa wa ngazi ya juu wa Uingereza amesema kulingana na pendekezo la May, raia wa nchi nyingine za Ulaya ambazo ni wanachama wa Umoja wa Ulaya wanaoishi kisheria Uingereza, hawatolazimishwa kuihama nchi na watapewa nafasi ya kuhalalisha hali yao ya maisha baada ya Brexit.

May aliwaambia waandishi wa habari Ijumaa kuwa "hakuna mtu atakayeondoka na hawataona familia zikigawanyika." Waziri Mkuu huyo wa Uingereza anatarajiwa kuchapisha ripoti inayoeleza mipango yake hiyo Jumatatu ijayo lakini alikwisha waeleza baadhi ya mambo viongozi wenzake hapo jana.

Mbali na Merkel viongozi wengine kadhaa wamefurahishwa na mapendekezo ya May, lakini bado wakiwa na wasiwais na kusema kwamba kuna masuala mengine kadhaa ambayo hayakupatiwa ufumbuzi, ikiwa ni pamoja na Waziri Mkuu a Luxemburg Xavier Bettel.

Nadhani watu hawa wanashiriki katika kukuza uchumi wa Uingereza hivyo ni muhimu kwao kujua jinsi maisha yao ya siku za mbele yatakavyokuwa. Tunahitaji kungoja siku chache kupata ufafanuzi zaidi," amesema Xavier Bettel, Waziri Mkuu wa Luxembourg.

Mkutano huo wa kilele wa viongozi wa nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya utaendelea leo kwa siku ya pili na ya mwishho mjini Brussels Ubelgiji

Mwandishi: Yusra Buwayhid/ap/rtre

Mhariri: Iddi Ssessanga

 

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com