1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAsia

Mawaziri wa Quad wakutana India kuimarisha ushirikiano

26 Mei 2026

Mawaziri wa mambo ya nje kutoka Australia, India, Japan na Marekani kundi linalojulikana kama Quad, wamekutana Jumanne mjini New Delhi kujadili namna ya kuimarisha ushirikiano wao katika eneo la Indo-Pasifiki.

https://p.dw.com/p/5ELHG
Mkutano wa Mawaziri Wanne wa Mambo ya Nje wa kundi la Quad katika Ikulu ya Hyderabad
Mkutano wa Mawaziri Wanne wa Mambo ya Nje wa kundi la Quad katika Ikulu ya HyderabadPicha: Julia Demaree Nikhinson/REUTERS

Mkutano huo unawakutanisha Waziri wa Mambo ya Nje wa India Subrahmanyam Jaishankar, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio, Waziri wa Mambo ya Nje wa Japan Toshimitsu Motegi, pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje wa Australia Penny Wong.

Wizara ya mambo ya nje ya India imesema viongozi hao watajadili maendeleo ya hivi karibuni katika ukanda huo na mbinu za kuimarisha ushirikiano kati ya mataifa yao.

Mbali na hilo, mawaziri hao wa kundi la nchi za Quad  wanatarajiwa pia kujadili vita vya Iran pamoja na kusitishwa kwa usafirishaji wa nishati kupitia mlango muhimu wa bahari wa Hormuz, jambo linalozua wasiwasi katika usalama wa nishati duniani.

India New Delhi 2026 | Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio baada ya Mkutano wa Quad
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio baada ya Mkutano wa QuadPicha: Julia Demaree Nikhinson/AP Photo/picture alliance

Quad ni kundi gani haswa?

Kundi la Quad linachukuliwa kama muungano muhimu wa kimkakati, unaolenga kuimarisha usalama wa bahari, minyororo ya usambazaji bidhaa na sera za kikanda, hasa wakati China ikiendelea kupanua ushawishi wake wa kijeshi na kiuchumi katika eneo la Indo-Pasifiki.

Mataifa hayo manne mara kwa mara yameishutumu China kwa kuonyesha nguvu za kijeshi katika Bahari ya Kusini ya China na kupuuza madai yake ya mipaka ya bahari kwa njia ya ukali.

Hata hivyo, Beijing imekuwa ikisisitiza kuwa shughuli zake za kijeshi ni za kujilinda na kulinda haki zake za kisheria, huku ikiitaja Quad kama jaribio la kuzuia ukuaji wake wa kiuchumi na ushawishi wake duniani.

India New Delhi 2026 | Mkutano na waandishi wa habari kufuatia mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje wa Quad
Mawaziri wa mambo ya nje wa kundi la nchi za QuadPicha: Adnan Abidi/REUTERS

Mkutano huo unafanyika siku chache baada ya Rais wa Marekani Donald Trump kufanya ziara nchini China, ziara iliyofuatiliwa kwa karibu na India, ikitafsiriwa kama ishara ya mwelekeo wa sera ya Washington kuelekea Beijing.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio, aliyewasili India Jumamosi, amesema Washington inataka kuona Quad ikienda zaidi ya kuwa jukwaa la majadiliano na badala yake ichukue hatua za vitendo katika masuala kama usalama wa bahari na madini muhimu.

Pia alibainisha kuwa maandalizi yanaendelea kwa mkutano wa viongozi wa Quad utakaofanyika baadaye mwaka huu, ingawa tarehe rasmi bado haijatangazwa.

Awali, mataifa hayo manne  yalikuwa yanapanga kufanya mkutano wa kilele nchini India mwaka uliopita, lakini uliahirishwa kutokana na changamoto katika uhusiano wa Marekani na India, ikiwemo tofauti za kibiashara na ushuru.