Mawaziri wa Mambo ya Nje na Maendeleo wa nchi za G20 wakutana nchini Italia. | Matukio ya Kisiasa | DW | 29.06.2021
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Italia

Mawaziri wa Mambo ya Nje na Maendeleo wa nchi za G20 wakutana nchini Italia.

Mawaziri wa mambo ya nje wa nchi 20 zilizostawi na zinazoinukia kwa kasi kiuchumi duniani za G20 wamesema janga la virusi vya corona limedhihirisha haja ya kuwepo ushirikiano mkubwa ulimwenguni.

Mawaziri wa mambo ya nje pamoja na wa maendeleo wa mataifa yenye ushawishi mkubwa ulimwenguni wanakutana kwenye mji wa Matera, kusini mwa Italia kujadili mikakati ya kupambana na COVID 19 na wakati huo huo kutafuta mbinu za kuharakisha kuufufua uchumi wa ulimwengu.

Je! Mawaziri wa G20 wanapanga nini juu ya COVID?

Mawaziri hao wanajadili njia za kuratibu jinsi dunia inavyolishughulikia swala la COVID 19 ambalo ni dharura ya kiafya katika dunia yote. Pia watatafuta njia zitazohakikisha kuwa nchi zote duniani zinakwenda sambamba katika maswala ya upatikanaji wa chanjo na upimaji wa virusi vya corona.

Waziri wa Mambo ya nje wa Italia Luigi Di Maio ameuambia mkutano huo kwamba janga la corona linaangazia uhitaji wa kuwa na ushirikiano wa kimataifa kwa ajili ya kuzishughulikia dharura ambazo zinavuka mipaka ya kitaifa.

Waziri wa Mambo ya nje wa Ujerumani Heiko Maas amesema lengo la mkutano huo ni kuweka msingi utakaokuwa sare kimataifa katika mapambano dhidi ya janga hilo. Waziri Maas amesema sasa ni wakati muafaka wa kuweka miundo imara na inayofanana ya afya ulimwenguni ili iwe rahisi kukabiliana na matatizo ya kiafya.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Heiko Maas

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Heiko Maas

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken amesisitiza juu ya umuhimu wa kupeleka chanjo kwenye nchi masikini ambazo zinahangaika hadi sasa kupata dozi za chanjo dhidi ya COVID 19 ili kulimaliza janga la corona duniani.

Katika mkutano wa ulimwengu juu ya afya uliofanyika huko mjini Rome, Italia mnamo mwezi Mei, nchi za G20 tayari zilikubaliana kuunda ushirikiano wenye nguvu katika maeneo yote yanayohusu utoaji wa huduma za afya kwa kuweka maandalizi bora yatakawozesha kukakibiliana na majanga ya afya ya hapo baadaye ulimwenguni kote.

Je! Ni kipi kingine kilichomo kwenye ajendaya mkutano wa G20?

Katika mazungumzo ya mjini Matera, mawaziri hao wa mambo ya nje pamoja na wa maendeleo wa mataifa wanachama wa kundi la G20 pia watajumuisha maswala kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa, biashara ya kimataifa, maendeleo endelevu na msaada kwa bara la Afrika.

Italia, ambayo inashikilia urais unaozunguka wa G20, imesema swala la maendeleo endelevu barani Afrika litapewa umakini mkubwa.

Waziri wa mambo ya nje wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Christophe Lutundula aliyealikwa na Italia katika mkutano huo, amelitolea wito kundi la G20 kuzisaidia nchi zinazoendelea kutengeneza chanjo zao wenyewe na kusaidia katika kuanzisha shirika litakalosimamia ushirikiano wa kisanyanyi kote barani humo.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken

Tutarajie nini kutoka kwenye mkutano wa Matera?

Kwa kuzingatia nchi anuwai katika kundi hilo la G20, ni vigumu kwa washiriki kufikia kwa haraka makubaliano juu ya maswala yenye ukakasi, hiyo ni kawaida.

Teresa Coratella wa Baraza la Ulaya juu ya uhusiano wa mambo ya nje ameiambia DW kwamba maswala ya maendeleo endelevu na hali ya hewa yanaweza kutawala kwenye mkutano huo.  Amesema hatua hii inaweza kuwa kiunganishi sahihi kwa wahusika wote kuweza kuwa na mtazamo wa pamoja kuhusu  mkakati wa muda mrefu wa kulishirikisha bara la Afrika kama mshirika mwenza na sio msikilizaji tu katika mikutano na kisha kusubiri maamuzi.

Je! G20 ni nini hasa?

G20 inazijumuisha nchi zenye uchumi mkubwa ulimwenguni, yaani nchi zilizoendelea na zinazoendelea kama Marekani, China, Ujerumani, India na Brazil.

Nchi hizi zina zaidi ya asilimia 80% ya pato la uchumi ulimwenguni, asilimia 75% ya biashara ulimwengu kote na asilimia 60% ya idadi ya watu ulimwenguni.

Mkutano huo wa mawaziri wa mambo ya nje na wa maendeleo unaandaa msingi wa mkutano wa kilele wa viongozi wa nchi za G20 wa mwaka huu wa 2021 utakaofanyika huko mjini Rome, Italia mwishoni mwa mwezi Oktoba ambao unatarajiwa kuwa ni  mkutano wa kwanza utakaowakutanisha Rais wa Marekani Joe Biden na mwenzake wa China Xi Jinping wakati kukiwa na  mvutano mkali kati ya nchi hizo mbili kubwa kiuchumi duniani.

Vyanzo:/AFP/ https://p.dw.com/p/3vjH4