1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Matokeo ya uchaguzi wa bunge Urusi

Mohammed Abdul-Rahman3 Desemba 2007

Chama cha rais Putin “Urusi ilioungana” kimepata asili mia 63 ya kura kwa mujibu wa matokeo ya awali.

https://p.dw.com/p/CW4P
Rais Putin akiwa na mkewe Lyudmila .Picha: AP

Tume ya uchaguzi imesema matokeo hayo ya asili mia 63 kwa chama cha rais Vladimir Putin yanatokana na asili mia 85 ya kura zilizokwisha hesabiwa na hivyo chama hicho kimo njiani kushinda theluthi mbili ya wingi bungeni.

Chama cha kikoministi kilikua nyuma kwa asili mia 11.7 kikifuatiwa na vyama vyengine viwili vyenye kuiunga mkono Ikulu-chama cha Urusi ilio na haki na kile cha demokrasia cha waliberali.

Matokeo yalipongezwa na Ikulu ya Urusi-Kremlin- ambayo inayachukulia kuwa ni sawa na kura ya maoni kuhusu uongozi wa rais Putin wakati akijiandaa kurudi akiwa na usemi fulani katika siasa za Urusi baada ya kuondoka madarani kama rais mwaka ujao, ikiwa ni kwa mujibu wa katiba baada ya mihula miwili ya miaka mitano kila mmoja.

Uchaguzi wa rais utafanyika mwezi machi mwakani, na chama cha Urusi iliungana kimetangaza kwamba kitamteuwa mgombea wake wa urais katika mkutano wake mkuu tarehe 17 mwezi huu wa Desemba.

Chama cha kikoministi kimesema kitaitaka mahakama kuu itowe uamuzi juu ya uhalali wa uchaguzi wa jana, kikitaja juu ya kasoro zinazohusika na karibu wapiga kura 10,000.

Hakukua na watazamaji kutoka shirika la usalama na ushirikiano barani ulaya kuangalia uchaguzi huo, baada ya kufuta ujumbe wake kutokana na ukosefu wa ushirikiano kutoka kwa maafisa wa serikali mjini Mosko.

Vyama vyengine saba kikiwemo chama cha upinzani cha kiliberali vimeshindwa kupata asili mia 7 ya kura , kiwango kinachohitajika kuingia bungeni. Ni mara ya kwanza tangu kusambaratika kwa uliokua muungano wa kisoviet yaani Urusi ya zamani 1991 kwa chama cha kiliberali kinashindwa kupata hata kiti kimoja .

Waziri mkuu wa zamani Mikhail Kasyanov ambaye anapanga kugombea urais mwezi Machi ameuita uchaguzi wa jana kuwa Usiokua wa haki, wakati viongozi wa umoja wa kiliberali wa kile kinachoitwa makundi yanayotetea haki, wameahidi kuchukua hatua za kuyakana matokeo.

Baadhi ya wachambuzi wameashiria Putin anaweza kumkabidhi madaraka ya urais mshirika muaminifu kwa muda na baadae kurudi tena baada ya uchaguzi mpya na hivyo kufutwa kifungu cha katiba kinachopiga marufuku mhula wa tatu .

Miongoni mwa wanaopewa nafasi kubwa ya kushika nafasi itakayoachwa na Putin ni Waziri mkuu Viktor Zubkov na manaibu waziri mkuu Sergei Ivanov na Dmitry Mdvedev.

Wakati huo huo, kufanikiwa chama cha demokrasia cha waliberali chenye kufuata siasa kali za kizalendo, kumemfungulia njia Andrei Lugovoi anayetakiwa na Uingereza kuhusika na mauaji kwa njia ya sumu ya mpinzani wa Kremlin Alexander Litvienko ya kuwa mbunge na hivyo kuwa na kinga nchini Russia. Tayari Urusi ilikata ombi la kumkabidhi kwa maafisa wa Uingereza.