Mashambulizi ya Israel huko Gaza yazidi kuwagawa Waarabu | Matukio ya Kisiasa | DW | 29.12.2008
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Mashambulizi ya Israel huko Gaza yazidi kuwagawa Waarabu

Mashambulizi ya Israel yaliosababisha maafa makubwa kwa Ukanda wa Gaza yamezidi kuugawa ulimwengu wa Kiarabu.

Maafa ya mashambulizi ya Israel katika Ukanda wa Gaza.

Maafa ya mashambulizi ya Israel katika Ukanda wa Gaza.

Mgawiko huo ni kati ya wale wenye itikadi kali za Kiislam ambao wana mvuto kwa umma na serikali za ukandamizaji ambazo kwa kiasi kikubwa zinaonekana kushirikiana na Israel na Marekani.

Hususan nchini Misri malumbano yamekuwa wazi kabisa kuliko ilivyokuwa kabla wakati wanachama wa chama tawala wakiwapa ushauri Waislamu wao wa itikadi kali washirika wa kundi la Kipalestina la Hamas kwamba iwapo hawapendi yale yalioko Misri wanaweza kwenda Gaza.

Hussein Megawir mbunge anayeitetea serikali amesema wakati wa mjadala juu ya Gaza hapo Jumamosi kwamba kuna mpango wa Iran kwa kushirikiana na Hamas na chama cha Wanandugu wa Kiislam cha Misri kuchochea vurugu katika maeneo ya Wapalestina na nchini Misri.

Chama cha Wanadugu wa Kiislam wa Misri kundi kuu la upinzani nchini humo likiwa na moja ya tano ya viti bungeni kina ushirikiano wa karibu na kundi la Hamas ambalo liliibuka kama tawi la chama hicho.

Kwa upande wake chama hicho cha wanandugu wa Kiislam wa Misri kinasema Waarabu na Waislamu wanapaswa kusimama dhidi ya ukimya wa dharao na kufumbia macho matendo ya Israel kunakofanywa na takriban tawala na serikali nyingi za nchi za Kiarabu na Kiislamu.

Katika taarifa zilizotolewa hadharani juu ya mashambulizi hayo ya Israel serikali ya Misri na washirika wake wa kundi la Wapalestina la Fatah zilikuwa zinakaribia kusema kwamba Hamas kwa kiasi kikubwa ilikuwa inastahiki kulaumiwa kwa mashambulizi hayo yaliouwa takriban watu 300.

Waziri wa mambo ya nje wa Misri amesema kwamba Misri ilionya juu ya uwezekano wa shambulio la Israel na kwamba wale waliopuuza onyo hilo wanawajibika na matokeo yake.

Mjini Cairo hapo Jumapili Rais Mahmoud Abbas wa Mamlaka ya Wapalestina ametowa kauli kama hiyo.

Amesema wamezungumza na Hamas na kuwaomba wasikomeshe usitishaji wa mapigano na Israel na waache makubaliano hayo yaendelee kwamba wangeliweza kuepusha kile kilichotokea.

Mchambuzi wa kisiasa wa Misri Hassan Nafaa akiandika katika gazeti la kujitegemea la Al Masry Al Yom amesema Hamas inaonekana kama vile ni adui wa pamoja wa Misri Israel na Mamlaka ya Wapalestina.

Amesema Israel na Marekani zimefanikiwa katika kuzifanya serikali za Misri na Saudi Arabia ziamini kwamba wimbi la Kishia linaloongozwa na Iran ni tishio kubwa kwa Mashariki ya Kati nzima.

Lakini kinyume na wahafidhina wa Kiarabu wanaolaumu Hamas katika sehemu nyingi za ulimwengu wa Kiarabu waandamanaji na watu wengine wamezishutumu serikali za Kiarabu kwa kubakia kimya bila ya kuchukuwa hatua juu ya mashambulizi hayo.

Kiongozi wa Libya Muammar Gaddafi ameungana na shutuma hizo kwa kusema viongozi wa Kiarabu wanapaswa kuona aibu kwa kuwa wanauza jina la mapambano ya Wapalestina kwa misimamo yao dhaifu ya woga na kukubali kushindwa.

Waandamanaji na makundi ya upinzani wamekuwa wakitaka Misri na Jordan kuvunja uhusiano wao na taifa hilo la Kiyahudi na kwamba Misri ifunguwe mpaka wake na Gaza uliofungwa tokea Hamas iliposhinda uchaguzi wa bunge wa Wapalestina hapo mwaka 2006.

Kambi hizo mbili za Kiarabu zimegawika katika mipaka ile ile kama ilivyokuwa miaka michache iliopita serikali za Misri, Jordan,Saudi Arabia na Mamlaka ya Wapalestina zikiwa upande mmoja na Hamas,Syria kundi la Hezbollah la Lebanon na makundi mbali mbali ya Waislamu wa itikadi kali, wafuasi wa sera za mrengo wa shoto na Waarabu wenye misimamo mikali ya kitaifa wakiwa upande mwengine.

 • Tarehe 29.12.2008
 • Mwandishi Mohamed Dahman
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/GOSz
 • Tarehe 29.12.2008
 • Mwandishi Mohamed Dahman
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/GOSz
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com