Marekani yaituhumu Urusi kwa mashambulizi ya malori ya misaada | Matukio ya Kisiasa | DW | 21.09.2016
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Marekani yaituhumu Urusi kwa mashambulizi ya malori ya misaada

Marekani inaamini ndege mbili za kivita za Urusi ndizo zilofanya shambulio dhidi ya msafara wa magari yaliyokuwa yakiwapelekea misaada Wasyria katika mkoa wa Aleppo, lakini Urusi imekana madai hayo.

Tukio hilo lilosababisha malori 18 kati ya malori 31 yaliyokuwa katika msafara kuteketea, huenda likawa pigo kubwa kwa jitihada za kidiplomasia za kutaka kusimamisha vita vya Syria vinavyoingia mwaka wake wa sita sasa.

Lakini licha ya kuzuka mzozo wa kutupiana lawama juu ya nani wa kulaumiwa kwa mashambulizi hayo yaliyotokea Jumatatu, wanadiplomasia wamejaribu kutaka kuokoa makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyofikiwa kati ya Urusi na Marekani na kuanza kutekelezwa rasmi Septemba 12.

Ikulu ya Marekani imesema ukweli ni kwamba waasi wa Syria hawana vikosi vya angani, kwa maana hiyo ama Urusi au jeshi la Syria walifanya shambulio hilo.

Ben Rhodes stellvertretender nationaler Sicherheitsberater von Barack Obama

Ben Rhodes, Naibu mshauri wa masuala ya usalama wa taifa katika ikulu ya Marekani.

"Habari tulizozipokea zinaonesha wazi kwamba lilikuwa shambulio la angani. Hiyo ina maana kuna pande mbili zinazoweza kuwajibika, ama serikali ya Syria au serikali ya Urusi. Kwa vyovyote vile, bado tunasisitiza serikali ya Urusi ndiyo ya kulaumiwa na kuwajibika kwa shambulio hilo, kutokana na kwamba ahadi yao chini ya makubaliano ya kusitisha mapigano ilikuwa ni kuhakikisha hakufanyiki shughuli zozote katika anga la maeneo ambapo misaada ya kibinaadamu inapita," amesema Ben Rhodes, Naibu mshauri wa masuala ya usalama wa taifa katika ikulu ya Marekani.

Urusi yakanusha madai

Maafisa wawili wa Marekani wameliambia shirika la habari la Reuters kwamba ndege mbili za kijeshi za Urusi za aina ya SU-24 zilikuwa zikiruka angani katika eneo la tukio Jumatatu usiku, na kwa ushahidi huo Marekani imebaini kwamba Urusi ndiyo ya kulaumiwa kwa mashambulizi dhidi ya msafara huo wa malori yaliyokuwa yamebeba misaada ya kiutu.

Hata hivyo, Igor Konashenkov, msemaji mkuu wa Wizara ya Ulinzi ya Urusi amesema wamezifanyia uchunguzi wa kina kanda za vidio zilizonaswa eneo la tukio na watu wanaojiita wanaharakati, lakini hawakugundua ushahidi wowote unaodhihirisha msafara huo ulishambuliwa kwa kutumia silaha za kurushwa kutoka angani.

Russland Igor Konaschenkow Sprecher des Verteidigungsministeriums

msemaji mkuu wa Wizara ya Ulinzi ya Urusi, Igor Konaschenkow

Shirika la hilali nyekundu la Syria limesema mkuu wa mmoja ya vituo vyao pamoja na raia wapatao 20 wameuawa, ingawa kuna idadi zinatofautiana. Aidha, shambulio hilo limeufanya Umoja wa Mataifa kusitisha misafara yote ya misaada kwenda Syria.

Viongozi wa mataifa 23 walikutana kwa zaidi ya saa nzima wakijadili kuhusu Syria, mjini New York, bila ya mafanikio makubwa na badala yake wamekubaliana wakutane tena Ijumaa, kuendeleza mazungumzo ya namna ya kuumaliza mgogoro uliosababisha vifo vya mamia kwa maelfu ya watu na kupelekea mamilioni wengine kuyahama makaazi yao.

Kufuatia shambulio hilo la Aleppo, kumeripotiwa makabiliano makali katika maeneo mbalimbali nchini Syria.

Mwandishi: Yusra Buwayhid/rtre/ape

Mhariri: Caro Robi

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com