Marekani yaitaka Hizbollah kuondoka Syria | Matukio ya Kisiasa | DW | 30.05.2013
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Marekani yaitaka Hizbollah kuondoka Syria

Marekani imewataka wapiganaji wa kundi la Hizbullah kuondoka mara moja nchini Syria ambako wanaripotiwa kushirki katika operesheni mjini Qusayr. Kuwepo kwa Hizbollah pia kumelaaniwa na Umoja wa Mataifa.

Marekani yawataka wapiganaji wa Hizbollah kuondoka Syria

Marekani yawataka wapiganaji wa Hizbollah kuondoka Syria

Kupitia wizara yake ya mambo ya nchi za nje, Marekani imesema kuwepo kwa wapiganaji wa Hizbullah katika mgogoro wa Syria ni jambo la hatari kubwa na lisilokubalika, na kuwataka wapiganaji hao kuondoka mara moja. Vile vile, msemaji wa wizara hiyo Jen Psaki alilaani mauawaji ya wanajeshi wa Lebanon yaliyotokea kwenye kituo cha ukaguzi wa barabara karibu na mpaka wa Syria.

Msemaji huyo ameonya kuwa kuhusishwa kwa Hizbullah sio kitisho kwa Syria peke yake, bali pia kwa utengamano nchini Lebanon.

Kuingilia kati kwa wapiganaji wa Hizbullah katika vita vya Syria kumesaidia kuwasambaratisha waasi nchini humo, hali ambayo imelaaniwa na Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa.

Azimio la Baraza la Haki za Binadamu

Navi Pillay, mkuu wa Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa

Navi Pillay, mkuu wa Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa

Wanachama 36 kati ya 47 wanaounda baraza hilo wamepiga kura kuunga mkono azimio linalolaani kushirikishwa kwa wapignaji hao, katika operesheni kali kwenye mji wa Qusayr. Azimio hilo lililowasilishwa na Marekani, Uturuki na Qatar, linakemea uingizwaji wa makundi ya kigeni kupigana upande wa serikali ya Rais Bashar al-Assad.

Mkuu wa Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa, Navi Pillay, amesema dunia haina budi kupata suluhisho la haraka kutanzua mgogoro wa Syria.

''Mgogoro nchini Syria unaelekea pabaya. Zinahitajika hatua za haraka kusimamisha umwagaji damu zaidi, na mateso ya watu wa nchi hiyo.'' Amesema Pillay

Inaaminika kuwa Hizbullah imetuma wapiganaji takribani 1,700 kupigana bega kwa begi na wanajeshi wa serikali ya Rais Assad, lakini Ufaransa inakadiria kuwa huenda idadi ya wapiganaji hao nchini Syria ikafikia 4,000.

Urusi yawaponda wapinzani

Urusi imesema yaelekea waasi wa Syria wanapendelea suluhisho la kivita

Urusi imesema yaelekea waasi wa Syria wanapendelea suluhisho la kivita

Huku hayo yakiarifiwa, Urusi imekosoa msimamo wa muungano wa waasi wa Syria, unaoweka kuondolewa madarakani kwa Rais Assad kuwa sharti la kushiriki kwao katika mkutano wa kimataifa unaoandaliwa kujadili suluhisho la amani kwa mgogoro wa Syria.

Akizungumza leo hii mjini Moscow, Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi, Sergei Lavrov, amesema inaelekea waasi hao na wanaowaunga mkono katika eneo hilo, watafanya kila juhudi kuhakikisha mgogoro huo haupati suluhisho la kisiasa. Lavrov amesema nia ya waasi hao ni kutaka uingiliaji kati wa kijeshi, limetangaza shirika la habari la Interfax.

Tangazo lililotolewa na Muungano wa Kitaifa wa Syria kupitia mkutano ambao umeendelea kwa wiki nzima mjini Istanbul, limesema waasi hao watakuwa tayari kushiriki katika mkutano unaoandaliwa, ikiwa tu Rais Assad atatengwa katika mchakato wa kisiasa.

Aidha, Muungano huo ulitaka hakikisho kutoka jamii ya kimataifa, kuwa hatua zitachukuliwa kusimamisha kile walichokiita ukandamizaji na mauaji yanayofanywa na utawala wa Assad, na kupatiwa msaada wa kuweza kulinda maisha ya wananchi wa Syria.

Taarifa za hivi karibuni zinasema kuwa Rais Assad ametangaza kuwa tayari shehena ya kwanza ya mfumo wa kisasa wa kujikinga na mashambulizi ya ndege imekwishawasili kutoka Urusi, na Israel imesema inachunguza ukweli wa taarifa hizo. Awali Israel ilikuwa imesema itajua la kufanya endapo silaha hizo za Urusi zingewasili Syria.

Mwandishi: Daniel Gakuba/AFPE/RTRE/APE

Mhariri: Mohammed Khelef

DW inapendekeza

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com