1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani na mamlaka ya kiadilifu

P.Martin7 Mei 2007

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lenye wanachama 192 litakapokutana kati kati ya mwezi huu kuwachagua wanachama wapya 14 wa Baraza la Haki za Binadamu (HRC),Marekani haitokuwepo kupiga kura yake.

https://p.dw.com/p/CHEn

Marekani ikitetea uamuzi wake,inasema itajiepusha kupiga kura kwa vile Baraza hilo lenye wanachama 47 limejipotezea uaminifu kwa sababu,zaidi huilenga nchi moja-yaani Israel na hupuuza nchi zinazovunja haki za binadamu kama vile Iran, Zimbabwe na Korea ya Kaskazini.

Lakini wanadiplomasia katika Umoja wa Mataifa, pamoja na wanaharakati wanaogombea haki za binadamu na hata wataalamu wa sheria wanasema, serikali ya rais George W.Bush haina haki ya kupitisha uamuzi kuhusu ukiukaji wa haki za binadamu unaotendwa na wengine wakati ambapo mwenendo wake wa uovu hauchunguzwi na shirika lolote lile la kimataifa.

Kwa mujibu wa Michael Ratner alie rais wa Kituo cha Haki za Kikatiba chenye makao yake mjini New York,Marekani haipo tayari kuchunguzwa kwa sababu ina hofu kuwa ukweli utafichuliwa.Marekani inakiuka misingi ya haki za binadam na ulimwengu unajua hilo.Amesema,Marekani hutumia mateso na inapuuza Mkataba wa Geneva kuhusika na wafungwa wa kivita na inawazuia watu kwa muda usiojulikana bila ya kufungua mashtaka.Akiendelea,Ratner wa Kituo cha Haki za Kikatiba amesema,Marekani haikubakiwa na hata chembe moja ya mamlaka ya kiadilifu…………mamlaka yake pekee ni matumizi ya nguvu.Kwa maoni ya Ratner,ni Marekani iliyopoteza uaminifu wake na kwa sababu hiyo kamwe haitochaguliwa.Ye yote atakaeulizwa humu duniani kama Marekani inahusika na vitendo vya mateso,yasikitisha kuwa jawabu litakuwa “ndio” aliongezea Michael Ratner.

Itakumbukwa kuwa Mei mwaka 2001,Marekani ilipojaribu kugombea kiti,ilitimuliwa kutoka iliyokuwa Halmashauri ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa kwa mara ya kwanza kabisa tangu kuundwa kwa halmashauri hiyo hapo mwaka 1947.

Kuanzia mwaka jana,Baraza la Haki za Binadamu ndio limechukua nafasi ya halmashauri ya hapo awali iliyokuwa na wanachama 53.Marekani ilijiweka mbali na uchaguzi wa kwanza wa baraza hilo jipya,ikidhaniwa kuwa ilihofia kushindwa. Sasa,ni mara ya pili kwa mfululizo kwa Marekani kutogombea uchaguzi katika shirika muhimu la Umoja wa Mataifa ambalo hutetea haki za binadamu.Msimamo huo wa Marekani umekosolewa pia na mbunge mmoja wa Marekani wa chama cha Demokrats,Tom Lantos.Yeye amesema,uamuzi wa serikali ya Washington ni kitendo cha kukata tamaa kisicho na mfano.