Marekani na Japan kuijadili China | Matukio ya Kisiasa | DW | 15.03.2021
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Marekani na Japan kuijadili China

Waziri wa Mambo ya Nje wa Japan Toshimitsu Motegi amesema mazungumzo yake ya kwanza na waziri mwenzake wa Marekani, Antony Blinken yanatarajiwa kuingazia China.

Akizungumza Jumatatu na kamati ya bunge inayohusika na masuala ya bajeti, Motegi amesema Japan na Marekani kwa pamoja zitachukua msimamo thabiti dhidi ya jaribio la China kubadilisha mambo yalivyo sasa.

Wakati wa ziara yao Japan, ikiwa ni ya kwanza nchi za nje Blinken na Waziri wa Ulinzi wa Marekani, Lloyd Austin wanatarajiwa kufanya mkutano utakaowashirikisha mawaziri wawili kutoka nchi hizo mbili siku ya Jumanne ambao ni Motegi na Waziri wa Ulinzi wa Japan, Nobuo Kishi. Mkutano huo utazungumzia masuala ya kidiplomasia na usalama.

Motegi amesema ziara hiyo nchini Japan ni fursa nzuri ya kuonesha kwamba muungano wa nchi hizo mbili hauwezi kutetereka ulimwenguni. Mkutano huo utafanyika wakati ambapo kuna wasiwasi kuhusu kuongezeka kwa ushawishi wa China katika ukanda wa Indo-Pasifiki.

USA Wilmington, Delaware | Joe Biden, Vorstellung Team | Anthony Blinken

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Anthony Blinken

Gazeti la Washington Post lililochapishwa leo, limeandika kuwa Blinken na Austin wamesema Marekani kwa sasa inashinikiza kuufufua uhusiano na marafiki pamoja na washirika wake katika uhusiano wa mmoja mmoja na katika taasisi za kimataifa na kujizatiti tena katika malengo, maadili na majukumu yao ya pamoja.

Wakizungumza kabla ya kuanza ziara yao, mawaziri hao wa Marekani wamesema kwa pamoja wataiwajibisha China pale itakapokiuka haki za binadamu katika jimbo la Xinjiang na Tibet, kuharibu uhuru wa Hong Kong, kukandamiza demokrasia nchini Taiwan au kudai eneo la baharini katika Bahari ya China Mashariki inayokiuka sheria ya kimataifa. Blinken na Austin wamesema wasipochukua hatua na kufanya maamuzi, China itafanya hivyo.

Marekani na Japan zinatarajiwa kuelezea wasiwasi wake kuhusu sheria ya China ambayo inawaruhusu walinzi wa pwani wa Beijing kutumia silaha.

USA | Kabinettsmitglieder | Lloyd Austin

Waziri wa Ulinzi wa Marekani, Lloyd Austin

Mapema mwezi huu, Waziri wa Mambo ya Nje wa China, Wang Yi alisema sheria hiyo haiilengi nchi yoyote ile. Meli za walinzi wa pwani wa China mara nyingi huonekana karibu na visiwa vidogo visivyo na watu katika Bahari ya China Mashariki, chanzo cha mvutano wa kidiplomasia kati ya China na Japan.

Aidha, Japan na Marekani pia wanatarajia kuthibitisha umuhimu wa muungano wa pande tatu na Korea Kusini na huenda wakagusia uhusiano mbaya kati ya Japan na Korea Kusini kuhusu masuala ya fidia wakati wa vita.

Ama kwa upande mwingine wapatanishi wa Marekani na Korea Kusini wamefikia makubaliano ya muda ya kulipia uwepo wa wanajeshi wa Marekani Korea Kusini. Makubaliano hayo yatajadiliwa katika mikutano ya Blinken na Austin.

(AP, DPA, AFP)