Marekani kuamua Juni juu ya ushuru wa bidhaa za chuma kutoka EU | Matukio ya Kisiasa | DW | 01.05.2018
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Marekani kuamua Juni juu ya ushuru wa bidhaa za chuma kutoka EU

Viongozi wa Umoja wa Ulaya wameupokea kwa shingo upande uamuzi wa Marekani kusitishia kwa muda ushuru wa bidhaa za chuma cha pua na bati kwa nchi hizo pamoja na Mexico na Canada. Ujerumani inadai ushuru uondoshwe kabisa.

Rais Donald Trump ameakhirisha hadi juni mosi uamuzi wa kuzitoza ushuru wa forodha bidhaa za chuma puwa na bati zinazoagiziwa kutoka Canada, nchi za Umoja wa ulaya na Mexico na wakati huo anasema yamefikiwa makubaliano ya kuziondolea moja kwa moja ushuru kama huo, Argentina, Australia na Brazil.

Uamuzi huo umepitishwa masaa machache kabla ya kumalizika muda uliopanagwa wa kusimamishwa kwa muda ushuru huo kwa nchi hizo.

Akitangaza uamuzi huo rais Donald Trump alisema:"Leo nnatetea usalama wa taaifa la Marekani kwa kuzitoza ushuru bidhaa zinazoagiziwa  kutoka nje za chuma puwa na bati.Tutatoza  ushuru wa asili mia 25 kwa chuma puwa na asili mia 10 kwa bati, ikiwa bidhaa hizo zitavuka mpaka wetu.Tunahitaji chuma puwa bila ya shaka lakini tunataka tupatiwe bidhaa hiyo kwa njia za haki na tunataka wafanyakazi wetu walindwe na tunataka makampuni yetu pia yalindwe."

UK Sheffield Stahlwerk Symbolbild Strafzölle (picture-alliance/empics/J. Giles)

Kiwanda cha chuma cha pua cha Uingereza kilichoko Sheffield. Umoja wa Ulaya unasema hatua ya Rais Donald Trump kuahirisha uamuzi kuhusu ushuru wa bidhaa hizo inarefusha mashaka.

Umoja wa Ulaya uko tayari kujadiliana lakini sio kwa vitisho

Umojua wa Ulaya haujaridhishwa na uamuzi wa rais Trump."Uamuzi wa rais wa Marekani unazidisha hali ya wasi wasi katika masoko ya dunia, hali ambayo tayari inaathiri maamuzi ya kibiashara" wamesema viongozi wa halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya katika taarifa yao.

"Umoja wa Ulaya unastahiki kuondoshewa moja kwa moja ushuru huo kwasababu Umoja wa Ulaya hauwezi kuwa kitisho kwa usalama wa taifa la Marekani.Taarifa ya halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya imeongeza kusema majadiliano pamoja na Marekani yataendelezwa, lakini hawako tayari kuzungumza katika hali ya vitisho.

Serikali kuu ya Ujerumani pia imepokea shingo upande uamuzi wa rais wa Marekani wa kuakhirisha kwa muda ushuru wa forodha kwa bidhaa za chuma puwa na bati kutoka nchi za Umoja wa Ulaya.

Naibu msemaji wa serikali, Martina Fietz amesema tunamnukuu" Hakuna si Umoja wa Ulaya na wala si Marekani atakaefaidika na kuzidi mivutano katika uhusiano wa kibiashara."Ameongeza kusema Umoja wa Ulaya utaendelea kusaka majadiliano pamoja na Marekani.

01.10.2009 DW-TV Quadriga Martina Fietz

Naibu Msemaji wa serikali ya Ujerumani Martina Fietz.

 Wasaa utumiwe kupunguza mivutano ya kibiashara

Mwenyekiti wa baraza la biashara na viwanda la Ujerumani DIHK Eric Schweitzer amesema "wasaa uliopo utumiwe kama fursa ya kupunguza mzozo wa kibiashara."

Jana waziri wa uchumi wa serikali kuu ya Ujerumani Peter Altmeier alisema kuna nafasi ndogo tu ya kufufuliwa makubaliano yaliyopooza ya biashara kati ya Marekani na umoja wa ulaya, makubaliano yanayojulikana kama "Ushirika wa biashara na uwekezaji kati ya nchi zinazopakana na bahari ya atlantik-TTIP.

Mwandishi: Hamidou Oummilkheir: Reuters/

Mhariri: Mohammed Khelef

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com