Marekani i tayari kujadiliana na Iran? | Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili | DW | 17.07.2008
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Timu Yetu

Marekani i tayari kujadiliana na Iran?

Marekani imetangaza kuwa itampeleka mjumbe wake kushiriki katika mazungumzo ya mpango wa nuklia wa Iran yanayopangwa kufanyika mwishoni mwa juma hili.Hatua hiyo inaashiria kuwa Marekani inataka suluhu ya kidiplomasia

default

Kiwanda cha kurutubisha uranium kilichoko Isfahan,Iran


Hata hivyo uongozi wa Marekani unashikilia kuwa haujabadili msimamo wake wa kuitaka Iran kwanza kusitisha mpango wake wa nuklia kabla majadiliano yoyote kuanza.Dana Perino msemaji wa Ikulu ya Whitehouse anasisitiza kuwa


''Tunataka kusuluhisha suala hili kwa njia ya kidiplomasia..tutaendelea kushirikiana na wadau wetu wa kimataifa na hicho ndicho kitakachofanyika siku ya Jumamosi.Kimsingi hakuna majadiliano yoyote yatakayofanyika mpaka pale Iran itakapositisha mpango wake wa kurutubisha madini ya uranium''William Burns anatarajiwa kujumuika na mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa ulaya Javier Solana pamoja na maafisa kutoka mataifa ya Uchina,Urusi,Uingereza,Ufaransa na Ujerumani.

Ahadi ya msaada na diplomasia

Kikao hicho kinasubiri jibu la Iran baada ya mataifa ya magharibi kuiahidi misaada ya fedha pamoja na kurejesha uhusiano wa kidiplomasia endapo itasitisha mpango wake wa nuklia.Iran kwa upande wake inashikilia kuwa mpango wake wa nuklia una lengo la kutengeza nishati ya matumizi na inakataa masharti inayowekewa ya kusitisha mpango huo.


Mivutano na Iran imekuwa ikiendelea hasa baada ya nchi hiyo kufanya majaribio ya makombora ya masafa marefu na mafupi wiki iliyopita.Hatua hiyo ilisababisha bei za mafuta kuongezeka na Marekani kutangaza kuwa itawalinda washirika wake dhidi ya mashambulizi yoyote.

Mjumbe anafaa?

Hata hivyo baadhi ya maafisa wa serikali ya Marekani walielezea wasiwasi wao kuhusu hatua hiyo ya kumuidhinisha William Burns kuhusika na majadiliano hayo ya Iran.Mjumbe huyo ni afisa wa ngazi za juu katika Wizara ya Mambo ya Nje.

Sean McCormack ni msemaji wa Wizara hiyo na anasisitiza kuwa mjumbe huyo ana uwezo wa kutimiza majukumu hayo.


''Burns ni mmoja ya wanadiplomasia wetu walio na uzoefu mkubwa wa kazi.Naamini kuwa endapo mabishano yatatokea kati yake na mwakilishi wa Iran Saeed Jalili bila shaka atajua hatua ya kuchukua.Atasisitiza kuwa ikiwa serikali yenu inataka kufanya majadiliano naamini munajua la kufanya.''
Uingereza iliyo mwandani wa Marekani katika suala hilo la Iran imeipongeza hatua hiyo ya kumshirikisha William Burns.

Iran na Marekani zilivunja uhusiano rasmi wa kidiplomasia mwaka 1979.


 • Tarehe 17.07.2008
 • Mwandishi Mwadzaya, Thelma
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/Edu2
 • Tarehe 17.07.2008
 • Mwandishi Mwadzaya, Thelma
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/Edu2
Matangazo

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com