1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni ya wahariri wa magazeti

Abdu Mtullya21 Novemba 2005

Katika maoni yao ,wahariri leo wanazungunzia juu ya miaka saba ya uongozi wa Gerhard Schröder na juu ya ziara ya rais Bush wa Marekani nchini China

https://p.dw.com/p/CHXo

Ukuransa mpya wa siasa unanza wiki hii hapa nchini Ujerumani baada ya vyama vikuu vya siasa kutia saini mkataba juu ya kuunda serikali ya mseto mkubwa.Maana yake ni kwamba enzi ya Gerhard Schröder alieiongoza Ujerumani kwa kipindi cha miaka saba sasa imefikia tamati.

Juu ya hayo mhariri wa gazeti la Kölner Express anasema kuondoka kwa bwana Schröder maana yake ni kuanza kwa uongozi wa bibi Angela Merkel mwanamke wa kwanza kushika wadhifa wa Ukansela katika historria ya Ujerumani.

Lakini mhariri pia anatilia maanani kwamba vyama vya kihafidhina vya CDU na CSU pamoja na chama cha SDP vimefikia mapatano ya kuiongoza Ujerumani licha ya kukabiliana kihasimu kabla ya uchaguzi mkuu uliofanyika mnamo mwezi wa septemba.

Mhariri anakumbusha kwamba vyama hiyvo vilikabiliana takriban kiadui mpaka dakika ya mwisho ya uchaguzi huo.Lakini kutokana na shinikizo la wananchi yaani wapiga kura vyama hivyo havikuwa na njia nyingine licha ile ya kukubali dhamana ya pamoja katika kuoingoza nchi.Mhariri anasema kwamba kinachotakiwa sasa ni siasa ya kutambua hali halisi badala ya malumbano ya kisiasa yasiyoleta ujenzi.

Mhariri wa gazeti la Märkische Oderzeitung anauliza iwapo bwana Schröder alikuwa Kansela mzuri kwa wajerumani?.

Akizingatia mapana na marefu yote juu ya uongozi wa bwana Schröder mhariri wa gazeti hilo anasisitiza kwamba hakuna Kansela mwingine wa Ujerumani aliyeshughulikia suala la amani kwa moyo wote kama Gerhard Schröder. Gazeti pia linampa bwana Schröder maksi za juu kutokana na uamuzi wake wa kuanza kuleta mageuzi muhimu.

Naye mhariri wa gazeti la mji wa bandari Rostock, Ostsee Zeitung anasema ni kweli kwamba bwana Schröder hakufanikiwa katika siasa ya ajira.Wajerumani wengi hawana kazi, lakini anasisitiza kuwa kansela huyo ambae ni wa tatu kutoka chama cha SDP katika historia ya Ujeruamni aliwaambia wananchi wake ukweli juu ya hali mbaya sana ya fedha baada ya enzi ya Kansela Helmut Kohl.

Bwana Schröder alipitisha mpango wa mageuzi ili kuikabaili hali hiyo.Mhariri wa gazeti hilo anasema mpango huo wa kihistoria ndio urithi ulioachwa na Gerhard Schröder.Lakini mhariri anasema mageuzi hayo yaliyomwondoa madarakani sasa yanapaswa kutekelezwa kwa nguvu zote na Kansela anayemfuatia.

Wahariri wa magazeti ya hapa nchini pia wanazaumguzia juu ya ziara ya rais G. Bush nchini China.

Juu ya ziara hiyo mhariri wa gazeti la Financial Times Deutschland anasema bwana Bush alikuwa na maneno makali ya kutamka katika hotuba zake.

Mhariri wa gazeti hilo anaeleza kwamba hakuna kiongozi mwingine wa nje aliyewahi kutumia kauli wazi , kama rais Bush katika kutoa mwito kwa watawala wa kikomunisti wa China juu ya kuwapa wananchi wao uhuru zaidi wa kisiasa na kiuchumi.

Katika hayo bwana Bush anastahili kusifiwa. Lakini mhariri anasema ujumbe wa bwana Bush haukuelekezwa hasa kwa utawala wa Peking bali kwa wapiga kura wa nyumbani . Ujumbe wa rais Bush , mhariri anatamka ,umeonyesha udhaifu uliopo katika siasa za ndani ya Marekani.

Udhaifu huo mhariri anasema utageuka kuwa tatizo la kimataifa.

Mhariri wa gazeti la Frankfurter Rundschau anasema mkutano wa rais Bush na rais Hu wa China haukuleta ukaribiano baina yao. Ni tabaini yake.

Marekani inaiona China kuwa mshindani,kadhalika China nayo ina mashaka juu ya Marekani.Mahariri anaeleza katika maoni yake kwamba viongozi hao hawakuwa namsingi wa pamoja katika mkutano wao.Wakati Bush alipokuwa anazumguzia juu ya suala la uhuru na haki za binadamu, rais wa China bwana Hu alikuwa anazumguzia juu ya suala la Taiwan.

Juu ya ziara hiyo gazeti la Neue Ruhr linasema kauli zote za bwana Bush, na hata kuenda kwake kanisani na kusali pamoja na wakristo wa China hakutawatikisa viongozi wa China.

Rais Hu wa nchi hiyo anatambua vizuri sana kwamba amekutana na rais anayezungumzia juu ya haki za binadamu wakati majeshi yake yamehusika na kashfa ya jela ya Abu Ghraib na mazingira ya ukosefu wa haki za kisheria kwa wafungwa katika jela ya Guantanamo.Kashfa hizo zimetia dosari kauli za bwana Bush juu ya kutetea haki za binadamu.