Maoni ya wahariri juu ya Rais wa Uturuki Tayyip Erdogan | Magazetini | DW | 30.03.2016
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Magazetini

Maoni ya wahariri juu ya Rais wa Uturuki Tayyip Erdogan

Katika tahariri zao wahariri karibu wote wanauzungumzia wimbo wa tashtiti juu ya Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan uliosikika kwenye kituo kimoja cha televisheni cha Ujerumani, NDR.

Rais wa Uturuki Tayyip Erdogan

Rais wa Uturuki Tayyip Erdogan

Wimbo huo unadhihaki kinachodaiwa kuwa ubadhirifu katika matumizi ya fedha na kampeni ya Erdogan ya kubana uhuru wa vyombo vya habari na haki za kiraia.

Mhariri wa gazeti la "Brauschweiger" anatilia maanani jinsi Rais Erdogan alivyohamaki juu ya mzaha uliomo katika wimbo huo. Mhariri huyo anasema hatua ya serikali ya Uturuki kumwita balozi wa Ujerumani nchini humo ili aeleze kuhusu tashtiti iliyotangazwa na kituo kimoja cha televisheni cha Ujerumani, inaounyesha mtazamo wa Rais Erdogan juu ya vyombo vya habari kwani alikitaka kituo hicho cha televisheni kiache kuitangaza tashtiti hiyo.

Mhariri wa gazeti la "Braunschweiger" anaitaka serikali ya Ujerumani ione jinsi serikali ya Uturuki inavyoubana uhuru wa vyombo vya habari.

Naye Mhariri wa gazeti la "Emder" anatilia maanani kwamba makala ya mzaha iliyotangazwa na televisheni ya Ujerumani imesababisha mvutano wa kidiplomasia baina ya nchi hiyo na Uturuki. Mhariri huyo anaeleza kwamba Rais wa Uturuki Tayyip Erdogan ameounyesha msimamo wake halisi juu ya vyombo vya habari. Kiongozi huyo hawezi kuvumilia kukosolewa na vyombo vya habari.

Erdogan aviandama vyombo vya habari

Uhuru wa vyombo vya habari wabanwa nchini Uturuki

Uhuru wa vyombo vya habari wabanwa nchini Uturuki

Gazeti la "Thüringischen Landeszeitung" limeshangazwa na jinsi Rais Erdogan alivyohamaki juu ya makala ya mzaha iliyotangazwa na televisheni ya Ujerumani.

Mhariri wa gazeti hilo anasema hasa, tashtiti kutokea Ujerumani ndiyo iliyosababisha mkwaruzano katika uhusiano baina ya nchi hiyo na Uturuki. Lakini jinsi Rais wa Uturuki alivyokasirishwa na mzaha juu yake ni jambo la kuchekesha. Kwa njia hiyo Uturuki inaipunguza fursa ya kufanyika mazungumzo juu ya nchi hiyo kuweza kukubalika kuwa mwanachama wa Umoja wa Ulaya. Kutokana na kutoikuwa na hisia za utani, Erdogan mwenyewe ndiye aliegeuka kuwa tashtiti.

Gazeti la "Badische" linasema ni jambo lisilokubalika kwamba Erdogan anajaribu kuishinikiza serikali ya Ujerumani juu ya vyombo vya habari. Mhariri wa gazeti hilo anaeleza kuwa Erdogan anafikiri anaweza kuishinikiza serikali ya Ujerumani ili izuie matangazo kwenye televisheni yanayomkosoa yeye. Sababu ni kwamba anafikiri Umoja wa Ulaya una hofu juu ya idadi kubwa ya wakimbizi walioko nchini Uturuki wanaotaka kuingia Ulaya

Vitisho vya Erdogan lazima vipingwe vikali kwa sababu ni lazima maadili ya nchi za magharibi yalindwe. Kinyume chake kitakuwa maafa kwa Ujerumani na Umoja wa Ulaya.

Mwandishi:Mtullya Abdu/Deutsche Zeitungen:

Mhariri:Iddi Ssessanga