Majadiliano yapamba moto kuhusu juhudi za kujumuishwa wageni katika maisha ya kila siku ya jamii humu nchini | Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili | DW | 03.09.2010
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Timu Yetu

Majadiliano yapamba moto kuhusu juhudi za kujumuishwa wageni katika maisha ya kila siku ya jamii humu nchini

Kansela Angela Merkel asema hakubaliani na hoja za Thilo Sarrazin hata hivyo anasema kuna haja ya kushadidia upande wa elimu miongoni mwa wahamiaji

Thilo Sarrazin akitembeza kitabu chake alichokipa jina-Ujerumani yajitokomeza

Thilo Sarrazin akitembeza kitabu chake alichokipa jina-"Ujerumani yajitokomeza"

Mvutano uliozushwa na hoja za Thilo Sarrazin, mwanachama wa bodi ya uongoziya Benki Kuu ya hapa Ujerumani, na pia mwanachama mashuhuri wa Chama cha Social Democratic, SPD, umezusha mjadala mwengine wa juhudi za kujumuishwa wageni katika maisha ya kila siku ya jamii.Rais wa shirikisho ameitaka serikali kuu ielezee msimamo wake pia kuhusu maombi ya wanachama wa bodi ya benki kuu wanaotaka Thilo Sarrazin afukuzwe kazi.

Kansela Angela Merkel ameliambia gazeti la kituruki, Hurriyet, hii leo kwamba juhudi za kujumuishwa wahamiaji katika maisha ya kila siku ya jamii ni mada muhimu katika wakati huu tulio nao.Kwa mujibu wa ripoti ya gazeti la Saarbrücker Zeitung, mkutano maalum utaitishwa mwaka huu kuhusu juhudi hizo na kusimamiwa na serikali kuu ya muungano wa vyama vya Christain Democratic, CDU; Christian Social Union, CSU, na kile cha kiliberali cha Free Democratic, FDP.

Thilo Sarrazin anatakiwa apokonywe cheo chake kama mwanachama wa bodi ya benki kuu na huenda akatolewa katika chama cha Social Democratic, kwa sababu ya hoja alizozichambua ndani ya kitabu chake kuhusu kasoro za wahamiaji katika kujumuika na wenzao katika jamii, pamoja na yale aliyoyasema katika mahojiano kuhusu aina maalum ya maumbile ya Wayahudi.

Kuhusu maombi ya wanachama wa bodi ya uongozi ya benki kuu wanaotaka Sarrazin apokonywe cheo chake, rais wa shirikisho la Jamhuri ya Ujerumani, Christian Wulff, atabidi aamue. Ofisi ya rais wa shirikisho imesema imepokea maombi hayo hii leo.Katika utaratibu wa kutathmini maombi hayo,serikali kuu imeombwa na rais wa shirikisho itoe maoni yake.

Katika mahojiano na gazeti la Hurriyet, kansela Angela Merkel amesema kinaga ubaga anapinga hoja za Sarrazin. Hoja za Sarrazin kwamba Ujerumani inajitokomeza, ni "upuuzi mtupu." Hata hivyo, kansela Angela Merkel amesisitiza " mengi zaidi yanabidi kufanywa katika juhudi za kuwajumuisha wahamiaji katika maisha ya kila siku ya jamii"."Inamaanisha,elimu,elimu na tena elimu"-amesema kansela Merkel.

Berlin Demonstration Sarrazin

Maandamano ya jumatatu iliyopita mjini Berlin dhidi ya mwanachama wa bodi ya benki kuu Sarrazin dhidi ya kitabu kinachozusha mijadala kuhusu wahamiaji humu nchini

Katibu mkuu wa chama cha CDU, Hermann Gröhe, ameliambia gazeti la Saarbrücker Zeitung- toleo la kesho jumamosi, baada ya kuvuliwa cheo chake Sarrazin, kama mwanachama wa bodi ya uongozi ya benki kuu, utawadia wakati kwao wao kuzungumzia mada yenyewe hasa. Anasema kujumuishwa wahamiaji wanaoishi humu nchini ni mojawapo ya changa moto muhimu zinazowasubiri. Mjumbe wa serikali kuu anaeshughulikia masuala ya wahamiaji, Maria Böhmer, wa kutoka chama cha CDU, ameshaitisha mkutano maalum kuzungumzia mipango ya kuwajumuisha ipasavyo wahamiaji katika maisha ya kila siku ya jamii.Utakua mkutano wa kwanza wa aina hiyo tangu serikali hii ya muungano wa vyama vya CDU, CSU na FDP kuingia madarakani mwaka jana na wanne kwa jumla.

Mwandishi: Oummilkheir Hamidou

Mpitiaji: Miraji Othman

 • Tarehe 03.09.2010
 • Mwandishi Oumilkher Hamidou
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/P3po
 • Tarehe 03.09.2010
 • Mwandishi Oumilkher Hamidou
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/P3po
Matangazo

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com