Magazetini Ujerumani | Magazetini | DW | 09.05.2011
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Magazetini

Magazetini Ujerumani

Miongoni mwa mada zilizogonga vichwa vya habari katika magazeti ya Ujerumani leo Jumatatu nzinahusika na mzozo wa fedha nchini Ugiriki na ghasia katika Mashariki ya Kati.

Gazeti la MAIN POST likieleza juu ya matatizo ya Ugiriki linasema:

"Ugiriki ikitoka katika kanda ya nchi zinazotumia sarafu ya Euro, basi hatua hiyo huenda ikasababisha matatizo makubwa zaidi kuliko yale yanayohusika na utaratibu wa kisheria na sera za fedha. Hata hivyo, tatizo la Ugiriki litabakia pale pale - nchi hiyo ina deni la takriban Euro bilioni 330. Vile vile sekta ya biashara binafsi ya Ugiriki, inadaiwa mabilioni katika nchi za nje. Kwa hivyo, ni vigumu sana kuamini kuwa Ugiriki, itaweza kulipa madeni ya Euro kwa kuirejea sarafu yake ya zamani Drachmen. Ugiriki ikitaka kuachana na Euro, basi haina budi kueleza waziwazi kuwa haina uwezo wa kulipa madeni yake - kwa maneno mengine, taifa ni muflis."

Kwa upande mwingine, gazeti la WESTDEUTSCHE ZEITUNG linaeleza hivi:

"Ugiriki ikiendelea kuingangania sarafu ya Euro, basi matukio yake hatimae yatakuwa mabaya mno. Kwani hatua kali za kupunguza matumizi ya serikali, kushusha viwango vya riba na kuahirisha kulipa au hata kusamehewa madeni yake, sio tiba. Isitoshe, nchi zingine za Ulaya na walipa kodi wake ndio watakaobeba sehemu kubwa ya mzigo huo. Gazeti la Westdeutsche Zeitung linaamini kuwa, kile ambacho hakijadhaniwa kutokea, huenda kikashuhudiwa - Ugiriki kujitoa katika kanda ya Euro,na itakuwa busara kufanya hivyo."

NEUE OSNABRÜCKER ZEITUNG likiandika kuhusu ghasia za Mashariki ya Kati linasema:

"Siku chache kufuatia kifo cha Osama bin Laden, macho ndio yameelekezwa Cairo nchini Misri. Sababu sio kwamba magaidi walikuwa wakiendesha harakati zao nchini humo, bali huko wanapigana Waislamu na Wakristo waliojaa chuki. Moja ni dhahiri, mapambano hayo yanatisha, kwani huo ni mfano mwingine wa matokeo ya itikadi kali na chuki za kidini. Kwa hivyo, machafuko ya kidini mjini Cairo yanakumbusha kuwa haitoshi tu kuchukua hatua za kupiga vita ugaidi unaochochewa na dini. Watu wanapaswa kuweka kando tofauti zao, ama sivyo, hawatofanikiwa cho chote."

Na RHEINPFALZ likiandika juu ya utaratibu wa kuhesabiwa watu Ujerumani, linasema:

"Kila mwananchi anaweza kuhifadhi habari zake binafsi dhidi ya kutumiwa vibaya. Hiyo inawezekana ikiwa hatoeleza kila kitu kuhusu maisha yake. Na sio kosa kuwa na wasiwasi huo, lakini mchakato wa kuhesabiwa hauwezi kuepukwa na ni muhimu. Kwani data za wananchi zinahitajiwa na serikali kwa ajili ya miradi tofauti, kama vile shule, huduma za wazee, soko la ajira, usafiri, ujenzi wa nyumba - yaani kwa takriban kila sekta."

Mwandishi: Martin,Prema/dpa

Mhariri:M.Abdul-Rahman

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com