Magazetini Ujerumani | Magazetini | DW | 02.09.2010
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Magazetini

Magazetini Ujerumani

Mada kuu ni mazungumzo ya amani ya Mashariki ya Kati mjini Washington na kumalizika kwa operesheni za kijeshi za Marekani nchini Iraq.

Tunaanza na gazeti la WESTDEUTSCHE ZEITUNG linalosema:

"Amani inaweza kupatikana, wahusika wakiikubali hali halisi.Israel yapaswa kukubali kuwa wakati umewadia kwa Wapalestina kuwa na taifa lao wenyewe. Na kundi la Hamas lenye itikadi kali za Kiislamu vile vile likubali kujijumuisha kama kundi la kisiasa na hapo chama cha Fatah hakitokuwa na budi kugawana madaraka."

Binadamu hapotezi matumaini, ama sivyo mazungumzo ya amani ya mjini Washington yasingewezekana lasema gazeti la MÜNCHNER MERKUR na kuongezea:

"Hata hivyo, kuna sababu ya kuwa na wasiwasi mkubwa.Kwani tango makubaliano ya kwanza ya Oslo kutiwa saini miaka 17 iliyopita, Wapalestina wangali wakingojea kuwa na taifa lao huru. Waisraeli pia wana matumaini ya kuishi kwa amani na usalama.Pande zote mbili zinahitaji kuwa na subra - sababu si kwamba hakuna anaetaka amani, bali bado kuna masuala mengi ya kufumbuliwa."

Tukipindukia mada nyingine, gazeti la VOLKSSTIMME linauliza nini kitakachotokea Iraq baada ya Marekani kukamilisha operesheni yake ya mapambano nchini humo?

"Hilo ni suala muhimu lakini tusisahau kuwa kwanza kabisa, uamuzi wa Obama kuvirejesha nyumbani vikosi hivyo unahusika na siasa za ndani. Wakati aliochagua si sadfa, kwani Novemba ijayo Wamarekani wanapiga kura kulichagua bunge jipya. Na hivi sasa, vita vya Iraq vinapingwa vikali na Wamarekani."

Gazeti la MÄRKISCHE ALLGEMEINE linatufungia pazia la udondozi wa magazeti ya Ujerumani kwa mada iliyokuwa midomoni kwa miezi kadhaa. Je, Michael Ballack atabakia nahodha wa timu ya taifa ya Ujerumani?

"Kocha Joachim Löw ameshajibu. Ballack atabakia nahodha wa kwanza na asipokuwepo uwanjani Phillip Lahm atashika usukani huo.Lakini kwa maoni ya gazeti hilo, kocha Löw alichukua muda mrefu sana kupitisha uamuzi wake. Na kusitasita kwake kumewaathiri wote; yeye, Ballack na Lahm."

Mwandishi:P.Martin/DPA

Mhariri: M.Abdul-Rahman