Magazetini Ujerumani | Magazetini | DW | 17.03.2010
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Magazetini

Magazetini Ujerumani

Wahariri wamejishughulisha zaidi na kadhia ya malipo ya wasiokua na ajira kwa muda mrefu na kuongezeka biashara ya silaha za Ujerumani ulimwenguni

Malipo ya fedha kwa wakosa ajira wa muda mrefu - maarufu kama Hartz 4 na kuongezeka kwa biashara ya silaha za Ujerumani ni baadhi ya mada zilizogonga vichwa vya habari katika magazeti ya Ujerumani leo Jumanne. Tutaanza na gazeti la BAADISCHE NEUESTE NACHRICHTEN. Likiandika kuhusu mageuzi yanayopendekezwa kufanywa katika malipo ya fedha kwa wasio na ajira kwa muda mrefu linaandika:

Baada ya kupata pigo kubwa katika uchaguzi mkuu uliopita, viongozi wepya wa chama cha Social Demokratik SPD wanahitaji kuwatuliza wafuasi wao na hasa kuwakikishia kuwa kanuni za HARTZ 4 sio mfumo unaolazimaka kufuatwa. Lakini haitokuwa rahisi hivyo kwa SPD kutekeleza mapendekezo yake ya mageuzi katika mfumo wa HARTZ 4.

Tukitupia jicho mada nyingine iliyogonga vichwa vya habari,gazeti la BILD ZEITUNG linasema:

Hata mwaka huu wa 2010, bado makampuni ya Ujerumani yanaendelea kuongozwa na wanaume. Ni wanawake 21 tu waliokuwepo katika bodi za makampuni 200 makubwa kabisa - idadi ya wanaume katika bodi hizo ni 812. Sasa, kampuni kubwa ya simu ya Ujerumani, "Deutsche Telekom" inataka kukomesha mtindo huo. Inatazamia kuwatengea wanawake kiwango maalum cha nafasi za uongozi.

Lakini mhariri wa BILD ZEITUNG anasema, kuwatengea wanawake nafasi maalum za kazi,ni tusi na ubaguzi dhidi yao. Hiyo ni kama kusema kuwa bila ya kusaidiwa wanawake hawatoweza kupanda vyeo. Likiendelea linaandika:

Kinachohitajiwa ni nafasi zaidi katika shule za chekechea na muda muwafaka wa kufanya kazi ili wanawake waweze kumudu mahitaji ya familia na kazi.

Tunamalizia uchambuzi wa magazeti ya Ujerumani leo hii kwa ripoti iliyotolewa na SIPRI- taasisi inayosimamia amani duniani kuwa Ujerumani inashika nafasi ya tatu katika biashara ya silaha duniani. Gazeti la OSTSEE ZEITUNG linasema:

Muuzaji mkubwa wa tatu wa silaha duniani- hiyo ni nafasi tusiyopaswa kujivunia. Kwani viwanda vya silaha vya Ujerumani vinafaidika kwa kutokuwepo amani duniani, hata baada ya kumalizika vita baridi. Lakini kupiga marufuku biashara ya silaha sio suluhisho kwani hiyo haitopunguza biashara ya silaha duniani lamalizia OSTSEE ZEITUNG.

Mwandishi:P.Martin/DPA

Mhariri: M.Abdul-Rahman