Magazeti ya Ujerumani | Magazetini | DW | 13.05.2008
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Magazetini

Magazeti ya Ujerumani

Tetemeko la ardhi nchini China na mkasa wa Rais wa Venezuela kumlinganisha Kansela wa Ujerumani na Adolf Hitler,ni miongoni mwa taarifa zilizogonga vichwa vya habari nchini Ujerumani leo Jumanne.

Basi hebu tuanze na tetemeko la ardhi lililotokea katika Wilaya ya Sichuan kusini-magharibi ya China hapo Jumatatu mchana.Gazeti la BAADISCHE NEUESTE NACHRICHTEN linasema:

Bila shaka haikuwa rahisi hivyo kwa viongozi wa China kukubali kupokea misaada ya kimataifa ili misaada hiyo ipate kuharakishwa kwa wahanga wa tetemeko la ardhi.Baadae ndio kazi za ukarabati zitaweza kuanza. Líkiendelea linasema:

Hivi sasa China haitaki kutoa nafasi ya kukosolewa,kwani ipo katika pirikapirka za matayarisho ya Michezo ya Olimpiki.China inataka kuwaonyesha wananchi uwezo wake - na ulimwengu nao uone jinsi nchi hiyo ilivyoendelea.Lakini mashirika ya misaada ya kigeni yakiingia nchini humo hivi sasa,wafadhili wanatazamia ripoti juu ya hali halisi.Bila shaka Beijing haitofurahishwa na hilo.Lakini nchi hiyo italaumiwa zaidi ikiwa itakataa misaada.Vibaya zaidi ni kwamba wahanga wa tetemeko hilo ndio watakaoathirika.

Tukiendelea na mada hiyo hiyo,OLDENBURGISHE ZEITUNG linasema upo mfumo onaoonya mapema mitetemeko ya ardhi.Lakini haijulikani iwapo onyo la tetemeko kubwa kama lile lililiotokea huko Sichuan lilitiwa maanani.Gazeti hilo likiendelea linasema:

Inavyodhihirika umma haujaonywa kuhusu tetemeko hilo.Na hiyo inatoa sura mbaya ya viongozi wa Kikomunisti nchini China.

Sasa tunabadilisha mada.Bei ya petroli inazidi kupanda na kuvunja rekodi katika masoko ya ulimwengu na hakuna hata dalili kuwa mtindo huo utabadilika.EMDER ZEITUNG linasema:

Bila shaka wanasiasa wanaamini kuwa huu ni wakati wa kupaza sauti kuhusu madai yao-na mojawapo ni pendekezo la kuwafidia wafanyakazi wanaotumia gari za binafsi kwendea kazini.

Gazeti hilo likiendelea linasema:

Moja ni hakika,mafuta yatakuja kumalizika siku moja.Kwa hivyo ni dhahiri kabisa kuwa bei ya petroli itafuata mkondo mmoja tu yaani itaendelea kupanda na hapo serikali haina uwezo wa kubadili mengi isipokuwa mwendesha gari mwenyewe.Yaani apunguze matumizi ya petroli kila inapowezekana.

Tunamalizia kwa mkasa wa Rais wa Venezuela Hugo Chavez kumlinganisha Kansela wa Ujerumani Angela Merkel na Adolf Hitler na ufashisti.OSTSEE ZEITUNG linaeleza hivi:

Rais Hugo Chavez anaejiona kama mtetezi wa nchi za Amerika Kusini anajulikana kwa ulimi wake mkali.Lakini hata kwa maoni ya nchi zingine za Amerika Kusini,Chavez alikwenda mbali mno alipomlinganisha Kansela wa Ujerumani na Adolf Hitler.

Gazeti hilo likiendelea linasema:

Kansela Merkel amefanya lililokuwa la busara ili kuzuia mvutano zaidi kati ya Berlin na Caracas.Yeye amepuuza ulinganisho huo wa kipumbavu.Kwani ziara yake ya Amerika Kusini haipaswi kutiwa dosari na mwanasiasa anaeropokwa lamalizia OSTSEE-ZEITUNG.