Mabilionea wakanusha kuhusika kashfa ya FinCEN | Matukio ya Kisiasa | DW | 21.09.2020
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

FINCEN

Mabilionea wakanusha kuhusika kashfa ya FinCEN

Kufuatia kufichuliwa kwa kashfa ya Majalada ya FinCEN yanayoonesha ufisadi na utakatishaji fedha unaofanywa na benki kubwa, matajiri kadhaa wamejitokeza kukanusha kuhusika huku hisa za benki zikiporomoka.

Bilionea wa Kirusi na mshirika wa Rais Vladimir Putin, Arkady Rotenberg, amekanusha shutuma kwamba aliitumia Benki ya Barclays kutakatisha fedha na kukwepa vikwazo, kama ilivyoripotiwa kwenye uchunguzi wa Majalada ya FinCEN. 

Msemaji wa bilionea huyo ameliambia gazeti la kibiashara la RBK la nchini Urusi kwamba taarifa kuhusu miamala yenye mashaka iliyofanyika kupitia Benki ya Barclays yenye makao yake makuu London, Uingereza ni za kipuuzi.

Ndugu wawili, Arkady na Boris Rotenberg, ni marafiki wa tangu utotoni na washirika wa Putin kwenye mchezo wa judo. Walijipatia utajiri wao wakati Putin alipoingia madarakani kwa kukabidhiwa kandarasi kadhaa za ujenzi, hasa kuelekea Michezo ya Olimpiki ya Sochi mwaka 2014. 

Kampuni ya Arkady Rotenberg pia ndiyo iliyojenga daraja linaloiunganisha Urusi na mkoa wa Crimea, ambao Putin aliunyakuwa kutoka Ukraine mwaka 2014. Ndugu hawa wawili waliwekewa vikwazo na mataifa kadhaa ya Magharibi ambayo yalizizuwia benki zake kufanya kazi nao.

Barclays na Deutsche Bank zatajwa

FinCEN Files / Morgan Stanley Bank, New York

Benki kadhaa ulimwenguni zimehusishwa na ufisadi na utakatishaji fedha kupitia miamala.

Uchunguzi uliofanywa na mashirika 108 ya habari ya kimataifa kutoka mataifa 88 unamtuhumu Rotenberg kutumia Benki ya Barclays kutakatisha fedha na pia kukwepa vikwazo hivyo. 

Uchunguzi wao unajikita kwenye maelfu ya nyaraka za shughuli zenye mashaka zilizowasilishwa kwa Idara ya Usalama ya Wizara ya Fedha ya Marekani na benki mbalimbali ulimwenguni. Nyaraka hizo zinaonesha kuwa kulikuwa na miamala ya dola trilioni 2 baina ya mwaka 1999 na 2017. 

Uchunguzi huo unawataja mabilionea wengine wa Kirusi walio karibu na Kremlin, wakiwemo Oleg Deripaska na Alisher Usmanov.

Hayo yakijiri, Benki ya Ujerumani ambayo inatuhumiwa kuwa zaidi ya nusu ya miamala hiyo ilifanyika imepoteza asilimia 8.15 ya hisa zake kufikia mchana wa leo, likiwa anguko kubwa kwenye soko la hisa mjini Frankfurt, yaliko makao makuu ya benki hiyo.

Vyombo kadhaa vya habari, ukiwemo mtandao wa BuzzFeed, BBC na gazeti la Sueddeutsche Zeitung la hapa Ujerumani yanasema nyaraka hizo za FinCEN zimeonesha jinsi beni kubwa ulimwenguni, ikiwemo Deutsche Bank, zilivyowaruhusu wahalifu kuhamisha fedha kote duniani.
 

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com