Kura ya maoni Uturuki, raia wataka mageuzi | Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili | DW | 13.09.2010
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Timu Yetu

Kura ya maoni Uturuki, raia wataka mageuzi

Katika kura ya maoni ambayo ilikuwa muhimu sana kwa taifa la Uturuki, raia nchini humo wameidhinisha mageuzi ya katiba ambayo hayajawahi kufanyika katika muda wa miongo kadha.

Waziri mkuu wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan akipiga kura yake ya maoni kuhusu mageuzi ya katiba, Septemba 12.

Waziri mkuu wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan akipiga kura yake ya maoni kuhusu mageuzi ya katiba, Septemba 12.

Katika kura ya maoni hapo jana ambayo ilikuwa muhimu sana nchini Uturuki, raia wa nchi hiyo wameidhinisha mageuzi makubwa ya kikatiba ambayo hayajawahi kufanyika katika muda wa miongo kadhaa. Waziri mkuu Recep Tayyip Erdogan amewahutubia wafuasi wa chama chake na kusema , huo ni ushindi kwa demokrasia. Katika vifungu karibu 26 vilivyofanyiwa mabadiliko, raia wa Uturuki sasa watakuwa na haki zaidi, katika kwa mfano uwezekano wa mtu binafsi kupeleka mashtaka katika mahakama ya katiba. Pamoja na hayo udhibiti wa raia katika jeshi umeimarishwa, kwani majenerali ambao watafanya mapinduzi wanaweza kwa mara ya kwanza kufikishwa mbele ya sheria.

Kama katika tamasha la muziki, waziri mkuu Recep Tayyip Erdogan alisherehekea ushindi huo na wafuasi wa chama chake. Kila wakati wafuasi hao walikuwa wakikatiza hotuba ndefu ya ushindi ya waziri huyo mkuu. Erdogan amesisitiza , kwamba si chama , bali ni demokrasia nchini Uturuki ambayo imeshinda katika kura hii ya maoni. Waziri mkuu amesisitiza pia maana ya Septemba 12, kwamba ni tarehe ya kura ya maoni. Tarehe 12 Septemba , mwaka 1980, ikiwa ni miaka 30 kamili , jeshi la Uturuki lilifanya mapinduzi na matokeo yake ni kile kinachojulikana kama katiba ya mapinduzi ya kijeshi. Na katiba hiyo ilikuwa hadi jana ni sehemu kubwa ya katiba ambayo haikubadilishwa na hivi sasa kwa kupitia matokeo ya kura hiyo ya maoni imefanyiwa mageuzi.

Tarehe hii ya Septemba 12 hadi sasa , kupitia katiba iliyotokana na mapinduzi ya kijeshi ilikuwa imechafuliwa. Kutokana na kura hii ya maoni , ambayo imefanyika pia tarehe 12 Septemba , inaanza sasa enzi mpya katika demokrasia. Tunafungua sasa ukurasa mpya na kuusafisha uchafu huo.

Waturuki wamepiga kura kwa wingi wa kushangaza katika kuidhinisha katiba hiyo. Kiasi cha asilimia 58 ya wapiga kura wamesema ndio , asilimia 42 wamekataa. Hadi hivi karibuni watafiti wa maoni ya wapiga kura walitabiri matokeo yanayokaribiana sana . Kiasi cha asilimia 78 ya wapigakura walishiriki katika kura hiyo ya maoni.

Kura nyingi za ndio zimepigwa hususan na wapiga kura kutoka upande wa mashariki ya Uturuki, katika eneo la Wakurdi nchini humo. Katika eneo hilo vyama vya Wakurdi na makundi ya kijamii yalitoa wito ya kususia kura hiyo ya maoni. Katika mji mkuu Ankara matokeo yalikuwa asilimia 57 ya wapiga kura wamesema ndio, na katika mji wa Istanbul kiasi cha wapiga kura asilimia 56 wamesema ndio.

Erdogan katika sherehe za ushindi wa kura hiyo ya maoni katika makao makuu ya chama chake mjini Istanbul amesisitiza uzalendo. Kura hiyo itaingia katika historia ya Uturuki, ameeleza.

Ni lazima watu wawakumbukeni, ni lazima watu watukumbuke.

Kupitia mageuzi hayo kutakuwa na sheria kadha za kiraia katika katiba hiyo. Miongoni mwa hizo ni haki kubwa zaidi kwa watoto na wafanyakazi, hususan ulinzi wa data utaimarishwa . Jeshi la Uturuki linapoteza zaidi umuhimu wake. Majenerali ambao wako hai ambao wamefanya mapinduzi katika mwaka 1980 wanaweza kufikishwa mahakamani, na hasa mamlaka ya mahakama ya kijeshi yatawekewa mipaka.

Zaidi ya hayo bunge la Uturuki litapatiwa mamlaka makubwa na jopo la majaji wa mahakama kuu nchini humo. Suala hili lilikuwa mada muhimu iliyokosolewa na upande wa upinzani kuwa inaingilia uhuru wa wabunge waliochaguliwa na wananchi.

Washindi dhahiri hata hivyo wa kura hii ya maoni ni chama tawala cha kihafidhina AKP cha waziri mkuu Erdogan. Kinaingia na kura ya wazi ya ndio , katika kinyang'anyiro cha uchaguzi wa bunge mwaka ujao.

Mwandishi : Steffen Wurzel / ZR / Sekione Kitojo

Mhariri:Abdul-Rahman

 • Tarehe 13.09.2010
 • Mwandishi Sekione Kitojo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/PAnQ
 • Tarehe 13.09.2010
 • Mwandishi Sekione Kitojo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/PAnQ
Matangazo

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com