Kura ya maoni Sudan ya kusini, mashakani kufanyika katika muda uliopangwa. | Matukio ya Kisiasa | DW | 29.10.2010
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Kura ya maoni Sudan ya kusini, mashakani kufanyika katika muda uliopangwa.

Mkuu wa Tume inayopanga zoezi la kura ya maoni itakayoigawa Sudan mara mbili, amesema itakuwa maajabu iwapo kura ya maoni juu ya uhuru wa Sudan ya kusini, itafanyika katika muda uliopangwa.

default

Rais wa Sudan ya kusini Salva Kiir.

Mohamed Ibrahim Khalil, Mkuu wa Tume inayopanga zoezi la kura ya maoni Sudan ya kusini, amewaambia waandishi wa habari kwamba muda uliopangwa hautoshi, na kwamba ametangaza kuchelewa kwa siku moja kwa zoezi la kujiandikisha kupiga kura, ambapo sasa zoezi hilo litaanza Novemba 15.

Kuchelewa kuanza kwa zoezi hilo kumetokana na kwamba, walitarajia vifaa vitakavyotumika katika zoezi hilo kuwasili mjini Khartoum, Oktoba 23, lakini vilichelewa kwa siku moja.

Aidha amesema tume yake haijapata fedha zozote kutoka katika Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Maendeleo -UNDP-, ingawa shirika hilo limeahidi kwamba litatoa zaidi ya dola milioni saba kwa ajili ya mradi huo.

Amefahamisha pia kwamba, hawajapata fedha zozote toka kwa wafadhili na kwamba kiasi kidogo cha fedha walichopata kutoka katika serikali ya kitaifa na serikali ya utawala wa ndani wa Sudan ya kusini, inasababisha matatizo katika kuwagharamia wafanyakazi katika vituo vipatavyo 10,800 vya kupigia kura.

Bajeti nzima kwa ajili ya zoezi zima la upigaji kura  inakadiriwa kuwa zaidi ya dola milioni 370.

Mkuu huyo wa tume ya kupanga uchaguzi, ameongezea kusema kuwa tume yao pia imekuwa ikikumbana na vikwazo vipya kila siku wakati ikihangaika kuhakikisha kuwa kura hiyo ya maoni inafanyika Januari 9, mwaka 2011.

Aidha muda uliopo umeelezwa kuwa ni mchache kuweza kusafirisha fomu za kupigia kura katika maeneo ya mbali ya Sudan ya kusini, ambako kuna matatizo ya miundo mbinu, na pia kwa ajili ya kutoa mafunzo kwa wafanyakazi watakaosimamia shughuli hiyo, kabla ya kuanza kwa zoezi la kuandikisha wapiga kura.

Mapema mwezi huu, Waziri wa Ulinzi wa Sudan ya Kaskazini alisema zoezi hilo la upigaji kura linaweza kuchelewa kwa sababu ya matatizo yaliyotokana na mpangilio wa usafirishaji vifaa hivyo.

Watu wengi wanawasiwasi kwamba kuchelewa kwa zoezi hilo kutasababisha kuzuka kwa ghasia miongoni mwa Wasudan ya kusini, ambao wanaona kura hiyo ya maoni kama njia pekee ya kutumia haki ya kujiamulia mambo yao.

Kura hiyo ya maoni ni moja ya makubaliano ya amani yaliyofikiwa mwaka 2005, kati ya Sudan ya kusini na kaskazini ya kumaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa zaidi ya miongo miwili na kusababisha vifo vya watu takriban milioni 2, na wengi walikufa kutokana na njaa na magonjwa. 

Mwandishi: Halima Nyanza(Reuters)

Mhariri:  Yusuf Saumu Ramadhan

 • Tarehe 29.10.2010
 • Mwandishi Halima Nyanza
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/PrcQ
 • Tarehe 29.10.2010
 • Mwandishi Halima Nyanza
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/PrcQ
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com