Kumbukumbu za mashambulio ya Septemba 11 mwaka 2001 zafanyika leo | Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili | DW | 11.09.2008
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Timu Yetu

Kumbukumbu za mashambulio ya Septemba 11 mwaka 2001 zafanyika leo

Kampeni za uchaguzi nchini Marekani zinasita leo kwa heshima ya Wamarekani waliouwawa wakati wa mashambulio ya Septemba 11 mwaka 2001

Ujenzi wa mnara wa uhuru, Freedom Tower, mahala palipokuwa kituo cha kimataifa cha kibiashara mjini New York

Ujenzi wa mnara wa uhuru, Freedom Tower, mahala palipokuwa kituo cha kimataifa cha kibiashara mjini New York

Marekani leo inafanya kumbukumbu za miaka saba tangu mashambulio ya kigaidi kufanywa katika miji ya New York na Washington mnamo Septemba11 mwaka 2001. Rais George W Bush wa Marekani anaongoza kumbukumbu hizo wakati akilazimika kuongeza idadi ya wanajeshi nchini Afghanistan, ambako wanamgambo wa al Qaeda hupanga mashambulio yao dhidi ya Marekani. Vita dhidi ya ugaidi vinaonekana bado havijafua dafu na kiongozi wa al Qaeda, Osama bin Laden. bado hajakamatwa.

Kwa kipindi cha ukimya na kuyaweka wakfu makumbusho ya wizara ya ulinzi ya Marekani, Pentagon, Marekani leo inafanya kumbukumbu ya saba ya mashambulio yaliyofanywa katika miji ya New York na Washington mnamo mwaka wa 2001, ambayo yameiongoza Marekani kuingia vitani mara mbili.

Rais George W Bush wa Marekani amewataka Wamarekani kunyamaa kimya kwa dakika moja mwendo wa saa 8:46, wakati ambapo ndege ya kwanza iliyokuwa imetekwa nyara iligonga mnara wa kaskazini wa jengo la kituo cha kibiashara cha kimataifa, mjini New York mnamo tarehe 11 mwezi Septemba mwaka wa 2001. Baada ya dakika chache ndege ya pili iliyokuwa imetekwa nyara na wanamgambo wa kiislamu iliupasua mnara wa kusini wa jengo hilo.

Kufikia mwisho wa saa nzima baada ya matukio hayo, ndege ya tatu iligongeshwa makao makuu ya wizara ya ulinzi ya Marekani, Pentagon, mjini Washington na ya nne ikaanguka huko Pennsylvania baada ya kile kinachokisiwa kuwa mapambano kati ya abiria na watekaji nyara ya kuidhibiti ndege hiyo.

Katika muda wa chini ya saa mbili, watu 2,975 walikuwa wamekufa. Wengine walifunikwa na vifusi na kuchomeka na mioto iliyozuka baada ya mashambulio hayo. Wazima moto 300 wa mjini New York na maafisa wa polisi walikufa wakati walipokuwa wakijaribu kuwaokoa watu huku minara ya jengo la Warld Trade Centre lilipokuwa ilipokuwa ikianguka. Wahanga wengine waliokufa walikuwa wafanyakazi wa wizara ya ulinzi, Pentagon au abiria waliokuwa ndani ya ndege zilizotumiwa kufanyia mashambulio hayo.

Washukiwa wote 19 wa mashambulio hayo walikufa. Kundi la al Qaeda na kiongozi wake Osama bin Laden nchini Afghanistan, lilidai kuhusika na hujuma hizo. Mgombea umakamu wa rais wa Marekani wa chama cha Republican Sarah Palin ameonya kwamba kitisho cha al Qaeda dhidi ya Mareka ni kingalipo.

Kumbukumbu za leo zitamjumulisha bendera kupeperushwa nusu mlingoti kwenye majengo ya serikali na nyumba za kibinafsi nchini kote. Wagombea urais wa Marekani, Barack Obama wa chama cha Democratic na John McCain wa chama cha Republican wamekubali kusitisha matangazo ya kampeni kwenye televisheni na kuachana na ratiba zao za kampeni. Wagombea hao watakutana katika chuo kikuu cha Columbia mjini New York kwa ibada ya kumbukumbu ya mashambulio ya Septemba 11 mwaka 2001.

Akimkosoa McCain kuhusu mashambulio hayo Barack Obama amesema, ´´Wakati McCain alipoiangalia Irak siku chache baada ya Septemba 11 nilisimama kupinga vita hivi nikijua vingetuelekeza vibaya na kutufanya tuache kitisho halisi kinachotukabili. Nilitaka raslimali na wanajeshi zaidi kumaliza vita dhidi ya magaidi waliotushambulia Septemba 11 na nikaweka wazi lazima tumkamate Osama bin Laden na viongozi wake.´´

Mjini New York familia za wahanga zitaanza sherehe zao kwa kusoma orodha ya majina ya marehemu katika bustani ya Zucotti na kisha baadaye watatembea hadi mahala palipokuwa jengo la kituo cha kimataifa cha biashara ambapo pamepewa jina la ´Ground Zero.´ Wakiwa hapo wataruhusiwa kuteremka kwa ngazi hadi ngazi ya mwisho chini.

Rais George W Bush na waziri wa ulinzi Robert Gates watahudhuria kuwekwa wakfu kwa kumbukumbu ya wizara ya ulinzi, Pentagon, mkusanyiko wa benchi 184 za chuma cha pua, moja kwa kila mtu aliyeuwawa katika makao hayo makuu ya wizara ya ulinzi.

Mabenchi 59 ya kuwakumbuka abiria waliokuwa katika ndege ya shirika la American Airlines nambari 77 zimewekwa katika hali itakayowalazimu wageni kutazama angani wakati watakapokuwa wakiyasoma majina ya wahanga hao. Mabenchi mengine 125 yamewekwa kuwageuza wageni kuyatizama makao makuu ya wizara ya ulinzi, Pentagon, kuwakumbuka wanajeshi na wafanyakazi wa kiraia waliokuwa ndani ya jengo hilo wakati ndege iliposhambulia.

 • Tarehe 11.09.2008
 • Mwandishi Charo, Josephat
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/FG2a
 • Tarehe 11.09.2008
 • Mwandishi Charo, Josephat
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/FG2a
Matangazo

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com