1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kosovo: Alama ya udhaifu wa siasa za Umoja wa Ulaya

13 Septemba 2012

Hata baada ya miaka minne ya kujitangazia kuwa huru na kutambuliwa na zaidi ya nchi 80 ulimwenguni, bado Kosovo imesimama kama alama ya udhaifu wa Umoja wa Ulaya ambao haujaonesha umoja imara kuelekea taifa hilo dogo.

https://p.dw.com/p/167nr
Bendera ya Kosovo
Bendera ya KosovoPicha: picture-alliance/dpa

Kitendo cha Kosovo kujitangazia uhuru wake mwaka 2008 kiliziweka pahala pagumu nchi za Umoja wa Ulaya zikijiuliuza ikiwa walitambue jimbo hilo, ambalo hadi wakati huo lilikuwa katika Serbia, kama nchi huru.

Baada ya hapo nchi nyingi za Umoja wa Ulaya, ikiwemo Ujerumani, ziliitambua Kosovo kama nchi huru. Waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani wa wakati huo, Frank-Walter Steinmeier, alitoa sababu ya kuchukuwa hatua hiyo kuwa ni imani ya Ujerumani kwamba "kuitambua Kosovo kutakomesha miaka mingi ya ukosefu wa usalama na utulivu. Ni kwa njia hiyo tu ndipo tutaelekea katika mustakbali ulio bora, sio tu kwa Kosovo, lakini kwa eneo lote la Magharibi ya Balkan."

Hivi sasa, nchi zaidi ya 80 zimeitambua Kosovo yenye wakaazi milioni mbili wenye asili ya Kialbania, lakini sio Serbia. Pia watu 40,000 wenye asili ya Ki-Serbia wanaoishi kwa wingi katika wilaya nne za kaskazini ya Kosovo hawautambui uhuru huo. Wao wana mabaraza, mahakama, mifumo yao ya kiusalama na hata shule.

Katika kura ya maoni iliofanyika Februari 2012, asilimia 99.7 ya watu hao wenye asili ya Ki-Serbia walikataa kuzitambua taasisi za Kosovo zilizoko katika mji mkuu wa Pristina.

Ulaya imegawika kuhusiana na Kosovo

Waserbia wakiandamana kupinga uhuru wa Kosovo.
Waserbia wakiandamana kupinga uhuru wa Kosovo.Picha: picture-alliance/dpa

Pia serikali za Ugiriki, Romania, Slovakia, Hispania na Cyprus, zote hizo ni nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya na bado hazijaitambua Kosovo. Waziri wa zamani wa mambo ya kigeni wa Cyprus, Marcos Kyprianou, aliwahi kusema katika mkutano wa mawaziri wa Umoja wa Ulaya mjini Brussles kwamba "jambo lolote linalohusiana na heshima ya utawala lazima lifanyike kupitia mashauriano na mazungumzo na sio kupitia nchi kujitangazia uhuru wake yenyewe."

Lakini kwa nini nchi hizo tano za Umoja wa Ulaya zinakataa kuitambua Kosovo? Jibu alilolitoa Rais wa Kosovo, Atifete Jahjaga, ni kwamba ndani ya nchi hizo kuna makabila makubwa ya yalio wachache, na kuna hofu kwamba makabila hayo yalio ya wachache yanaweza kudai uhuru.

Lakini Rais Jahjaga anasema kwamba hawana nia ya kurudi nyuma. "Hata baada ya mwisho wa kipindi cha uhuru unaosimamiwa, tutabakia na nia ya kushikilia misingi ambayo tumeijenga dola hii ya Kosovo, nayo ni demokrasia, uhuru na usawa mbele ya sheria kwa kila raia wetu, bila ya kujali."

Kazi bado ipo

Waserbia wakiandamana kupinga uhuru wa Kosovo.
Rais wa Kosovo, Atifete Jahjaga akikaribishwa na Rais wa Umoja wa Ulaya, Herman Van Rompuy, mjini Brussels.Picha: dapd

Kuna kazi kubwa ya kujenga amani ya kudumu katika Kosovo, nchi ambayo bado inaugua majaraha ya mzozo wa mwaka 1999, huku ikikumbwa na matatizo ya ukosefu wa ajira, uhalifu wa kupangwa na ufisadi.

Hadhi gani ilionayo Kosovo ni suala ambalo bado halijapatiwa ufumbuzi wazi kabisa; eneo la kaskazini ya Kosovo ni kama tanuri lenye cheche za moto, huku kukiweko hofu kwamba cheche ndogo inaweza kuleta mripuko mkubwa.

Kwa mfano katika mwaka 2004, baada ya watoto wawili wenye asili ya Kialbania kuzama katika Mto Ibar huko Mitrovica, tukio ambalo Waserbia kwa makosa walilaumiwa, kulitokea michafuko ilioelekezwa dhidi ya Waserbia na ilienea katika Kosovo nzima. Si chini ya watu 30 walikufa na 900 walijeruhiwa.

Kamwe Serbia haiukubali ukweli kuwa Kosovo si yake tena

Rais wa Kamisheni ya Umoja wa Ulaya, Jose Manuel Barroso.
Rais wa Kamisheni ya Umoja wa Ulaya, Jose Manuel Barroso.Picha: AP

Pia hasira zilichomoza mnamo katikati ya mwaka 2012 baada ya Jamhuri ya Serbia kuwaruhusu Waserbia wa Kosovo kupiga kura katika uchaguzi wake wa urais na bunge.

Japokuwa uchaguzi huo ulifanyika, lakini ulitanguliwa na mikwaruzano baina ya Waserbia na Waalbania. Nyumba moja iliripuliwa kwa bomu huko Mitrovica ambapo Mualbania mmoja aliuwawa na pia walikamatwa watu kutoka pande zote mbili.

Vile vile Julai 2011, mapigano yalizuka na wanajeshi wa kulinda amani wa Jumuiya ya NATO walizidishwa huko Kosovo pale serikali ya nchi hiyo ilipotuma maafisa wake yenyewe wa forodha kuudhibiti mpaka wa kaskazini na Serbia baada ya kutokea mzozo wa kibiashara.

Baada ya kisa hicho, Kansela Angela Merkel wa Ujerumani aliwataka Waserbia waondoshe taasisi zao huko Kaskazini ya Kosovo ikiwa ni shuruti kabla ya Umoja wa Ulaya kuipa Serbia hadhi ya kuwania kuwa mwanachama wa Umoja wa Ulaya.

Lakini baada ya Kosovo na Serbia kutanzua baadhi ya masuala waliyokuwa wanayabishania, Umoja wa Ulaya uliipa Serbia hadhi ya kuwa nchi yenye kuwania uwanachama wa Umoja huo, hivyo kuwa na hamu ya kuibakisha nchi hiyo ikiwa na tamaa ya kuwa siku moja angalau mwanachama kamili wa Umoja wa Ulaya.

Udhaifu wa siasa za nje za Umoja wa Ulaya

Rais wa Baraza la Umoja wa Ulaya, Herman van Rompuy.
Rais wa Baraza la Umoja wa Ulaya, Herman van Rompuy.Picha: Reuters

Bila ya shaka, mgawanyiko ulioko kati ya nchi za Umoja wa Ulaya juu ya uhuru wa Kosovo unadhoofisha siasa ya Umoja huo katika eneo hilo.

Ikiwa nchi zote za Umoja wa Ulaya zinaitambua Kosovo, basi siasa ya umoja huo kwa nchi hiyo zinaweza kuwa na uzito mkubwa zaidi. Lakini hilo kwa sasa halitazamiwi, kwani hivi sasa urais wa Umoja wa Ulaya unashikiliwa na Ugiriki ambayo inapinga vikali uhuru wa Kosovo.

Kama Umoja wa Ulaya haujaungana kikamilifu katika suala la Kosovo, isitarajiwe kwamba nayo Serbia itaachilia rasmi kushikilia kwamba eneo hilo ni sehemu ya ardhi yake.

Rais mpya wa Serbia, Tomislav Nikolic, katikati ya mwaka huu baada ya kufanya mazungumzo na Rais wa Baraza la Umoja wa Ulaya, Herman Van Rompuy, na Rais wa Kamisheni ya Umoja wa Ulaya, Jose Mnuel Barroso, alitoshelezeka kwa kusema yeye amepokea uhakikisho kwamba Umoja wa Ulaya hautailazimisha Serbia iitambuwe Kosovo. Kinyume na hivyo ingekuwa ni jambo lisilokubalika kwa Nikolic ambaye ni mzalendo kindakindaki kutoka Serbia.

"Serikali hii mpya ina nia ya kutekeleza kila kitu kilichokubaliwa jatika mdahalo wa kiufundi baina ya Kosovo na serikali ya zamani ya Serbia,na pia zaidi kufanya mdahalo wa kisiasa katika ngazi ya juu kabisa kwa madhumuni ya kufikia suluhisho la kudumu kwa eneo letu ambalo limechafuka. lakini fikra yetu ni kwamba ni tu suluhisho ambalo ni la haki na la kudumu litahifadhi amani na utulivu katika eneo hili." Alisema Nikolovic.

Bado Umoja wa Ulaya waitega Serbia

Rais Atifete Jahjaga wa Kosovo na Rais wa Umoja wa Ulaya, Herman Van Rompuy.
Rais Atifete Jahjaga wa Kosovo na Rais wa Umoja wa Ulaya, Herman Van Rompuy.Picha: dapd

Hiyo haina maana Umoja wa Ulaya hautaitaka Serbia inywe shubiri chungu ya kuitambua Kosovo pale wakati utakapofika kutakiwa kufanya hivyo, pale itakapokuwa tayari kutaka kuingizwa kama mwanachama wa Umoja wa Ulaya.

Hivi karibuni, huyo huyo Barroso alipofanya ziara huko Belgrade aliweka wazi kwa kusema kuwa anasisitiza "Serbia kuwa na uhusiano wa kawaida na Kosovo linabaki kuwa shuruti muhimu kabisa ya kusonga mbele kuelekea hatua inayofuata ya maendeleo."

Kwa maneno mingine, jambo hilo litakuwa muhimu kuiwezesha Tume ya Umoja wa Ulaya mwishowe "kupendekeza yaanzishwe mashauriano ya kuiingiza Serbia kuwa mwanachama kamili wa Umoja wa Ulaya."

Kwa hivi sasa Umoja wa Ulaya unataka pande zote mbili - Serbia na Kosovo - zivifanye vivuko vyao vya mpakani viwe vya kawaida.

Kosovo yapaswa kujirekebisha kwanza

Mkuu wa Sera za Nje wa Umoja wa Ulaya, Caherine Ashton.
Mkuu wa Sera za Nje wa Umoja wa Ulaya, Caherine Ashton.Picha: AP

Kosovo hivi sasa haina hadhi ya kuwa nchi inayowania kuwa mwanachama wa Umoja wa Ulaya kwa vile sio nchi zote wanachama wa Umoja wa Ulaya wanaoitambua nchi hiyo.

Hata hivyo, njia ya kuelekea kujiunga na Umoja huo iko wazi. Na ndio maana Kosovo inataka kuboresha uhusiano wake na Serbia na kuwaheshimu Waserbia walio wachache katika ardhi yake.

Lakini kwa vyovyote vile, hadhi ya Kosovo lazima itanzuliwe na jambo hilo litachukuwa muda mrefu kwa Serbia na Kosovo kila upande kuutambua mwengine.

Kosovo bado sio tulivu, hasa linapokuja suala la utawala wa sheria na uhusiano wake na Waserbia walioko eneo la kaskazini ya nchi hiyo. Pia nchi tano za Umoja wa Ulaya ambazo haziitambuwi Kosovo au suala la Kosovo kutokuwa mwanachama wa Umoja wa Mataifa ni mambo ambayo hayatabadilisha hali hiyo.

Kwa hakika kuondoka majeshi ya kimataifa ya kuweka amani kutoka nchi hiyo kutasababisha hatari zaidi kwa Waserbia wa Kosovo walio wachache. Bado Kosovo ni eneo la hatari ambalo linahitaji kuweko majeshi ya kimataifa kwa miaka mingi ijayo.

Njia ya kuelekea mustakbali mzuri katika eneo hilo ni kwa serikali ya Pristina na ile ya Belgrade kufanya mazungumzo ya ana kwa ana, bila ya kuwekeana masharti ya kabla, na mwishowe huenda suluhisho likawa ni kuwa na taasisi za pamoja na kuwa na bunge la pamoja kama ilivyotokea katika Ireland ya Kaskazini. Tamaa iko, kwani maadui wa leo wanaweza kuwa washirika wa kesho.

Mwandishi: Christoph Hassel/Othman Miraji
Mhariri: Mohammed Khelef