Kombe la Afrika Angola na Algeria leo uwanjani | Michezo | DW | 18.01.2010
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Michezo

Kombe la Afrika Angola na Algeria leo uwanjani

Malawi na Mali ipi itafuzu kuingia duru ijayo ?

Algeria kulivamia leo lango la Angola Luanda ?

Algeria kulivamia leo lango la Angola Luanda ?

Baada ya Simba wa nyika -Kamerun, kukwepa jana, salama usalimini, risasi za Chipolopolo- Zambia ambazo nusra ziwatimue nje ya Kombe la Afrika, hivi punde (Jumatatu Jioni), itakua zamu ya wenyeji Angola kupambana na Algeria, mjini Luanda,kuania tiketi yao ya duru ijayo.

Sambamba na changamoto hiyo hivi punde,Malawi na Mali, watakuwa nao uwanjani mjini Cabinda huku kila mmoja wao akiania tiketi ya kucheza robo-finali ya Kombe hili.

Bayer Leverkusen,imerejea kileleni mwa Bundsliga mwishoni mwa wiki baada ya kupoteza kwa masaa 24 usukani huo kwa Bayern Munich.

Na huko Tanzania, Ligi Kuu imeanza pia kwa duru ya pili huku mahasimu wa jadi Simba na Young Africans wakianza kufukuzana kuparamia kileleni.

KOMBE LA AFRIKA ANGOLA:

Tuanze na Kombe la Afrika la Mataifa nchini Angola,jioni hii:

Wenyeji Angola, wameahidi kuendelea kuihujumu Algeria hivi punde, firimbi ikilia mjini Luanda hata ikiwa sare ingetosha kwa Angola kuingia robo-finali.Katika kundi hili A, nafasi 2 za kwanza bado si wazi zinakwenda wapi huku timu zote 4 katika kundi hili A, zina nafasi ya kucheza duru ijayo ya robo-finali.Angola inaongoza kundi hili ikiwa na pointi 4,pointi 1 zaidi ya Algeria na Malawi huku Mali ikiwa nyuma kwa pointi 1.

Mali lakini,lazima ishinde Malawi huko Cabinda na kutegemea Angola inaishinda Algeria .Kutokana na hali hii, mapambano yote haya 2-Angola dhidi ya Algeria na Malawi dhidi ya Mali, yanachezwa wakati mmoja.

Angola, inaongoza kwa watiaji magoli mengi,kwani hadi sasa imetia mabao 6 kati ya mastadi wake Flavio na Manucho .Mashambiki 50,000 watarajiwa kusheheni leo uwanjani Luanda kushuhudia timu yao inatamba mbele ya waalgeria.

Katika mpambano wa pili, matarajio ya Mali yakuondoka na ushindi wa kwanza katika Kombe hili nchini Angola,yametiwa doa na kuumia kwa stadi wake Frederic Kanoute na stadi wa kiungo wa Juventus, Momo Sissoko.

Kocha wa Mali, Stephen Keshi aliwaambia maripota jana atapitisha uamuzi dakika ya mwisho iwapo mastadi hao 2 wacheze au la.Mabingwa watetezi Mafraouni (Misri) na Tembo wa Ivory Coast ndizo timu 2 za kwanza zilizokwishakata tiketi zao za duru ijayo ya robo-finali.

Mjini Lubango, simba wa nyika-kameroun walitoka nyuma jana na kuikandika Zambia mabao 3-2 wakati gabon ilibakia kileleni mwa kundi lao baada ya kuachana suluhu 0:0 na Tunisia.

Kocha wa Zambia,Herve Rennard, alisema jana kwamba, amekasirishwa mno na timu yake kwa kuwatilia bao wakamerun na kuwafufua kaburini.Kwa bao la kichwa la Idirosou anaecheza katika Bundesliga, simba wa nyika waliondoka na ushindi wa mabao 3:2.Madhambi ya kipa wa zambia, yaliwachimbia kaburi lilililowazika Lubango.

Nigeria, iliozabwa mabao 3:1 na mabingwa Misri katika mpambano wao wa kwanza ,wameahidiwa kitita cha dala 88.500 kila mchezaji wakiondoka Angola na Kombe la Afrika kwa mara ya 3 katika historia yao.

Shirikisho la dimba la Nigeria, lililikshatangaza kwamba, kila mchezaji wa Nigeria, atapewa dala 30.000 ikiwa Nigeria, itafuzu kucheza duru ijayo ya robo-finali na wakitoka suluhu na mamba wa M sumbiji keshokutwa huko Lubango watatia mfukoni kitita hicho.Mbali na vitita vya fedha, Super Eagles walitunukiwa nyumba bure kila mchezaji walipovaa taji la Afrika mara 2 zilizopita, 1980 na 1994.

Taarifa kutoka Benguela, zinasema mshambulizi mwengine wa Bundesliga,Mohamed Zidan, anakabiliwa na hatari ya kupigwa kumbo nje ya timu ya mafiraouni-Misri baada ya kufoka kwake alipobadilishwa na kutolewa nje ya uwanja pale Misri ilipoichapa Msumbiji mabao 2:0.Zidane, kwa hasira kubwa aliitupa chini jazi iliokua katika bao la wachezaji wa akiba.

BUNDESLIGA:

Zedane anaichezea Borussia Dortmund katika Bundesliga na jana klabu yake hiyo iltia bao la dakika ya mwisho kuinyan'ganya FC Cologne pointi 3 nyumbani.Kwa mabao 3-2 kwa mara nyengine tena FC Cologne imeshindwa kutamba nyumbani licha ya kusawazisha mabao 2:2 kabla bao la ushindi la Dortmund.Baadae kocha wa Dortmund Jürgen Klopp alisema:

"Natumai Kwa bao la Kevin Kreuz, dakika ya mwisho ya mchezo tumeweza kuondoka washindi,ingawa kwa wenzetu FC Cologne, ni bahati mbaya kushindwa baada ya kutoka nyuma na kurejesha mabao 2:2.hatahivyo, ndido mchezo wa mpira ulivyo."

Schalke iliondoka na ushindi wa bao 1:0 Nüremberg, nyumbani dhidi ya na sasa iko nafasi ya pili ya ngazi ya Bundesliga.Bao la Kevin Kuranyi, liliwaokoa Schalke kubakia na pointi 3 nyumbani zilizowapandisha hadi nafasi ya pili nyuma ya viongozi wa Ligi Bayer Leverkusen.Baadae Kevin Kuranyi alisema,

"Baada ya kutia bao hilo, tulijaribu kushambulia usoni tukisaka nafasi za kutia magoli zaidi,lakini muhimu ni kuwa tumezibakisha pointi 3 nyumbani."

Ama viongozi wa Ligi,Bayer Leverkusen walipiga hodi mara 3 na kuitikiwa karibu katika lango la Mainz Jumamosi na sasa wamerudi kileleni kwa pointi zao 38.Awali,Bayern Munich, ilichukua usukani wa kuongoza Bundesliga ilipoanza kwa duru ya pili hapo Ijumaa ilipoizaba Hoffenheim mabao 2-0 na sasa iko nafasi ya 3.

PREMIER LEAGUE:

Katika Premier League-ligi ya Uingereza, Chelsea imekomea mabao 7 kwa mara ya kwanza tangu kupita miaka 50 ilipoikandika Sunderland mabao 7-2 Jumamosi na kubakia kileleni mwa Premier League.Manchester United ina pointi 47 ingawa imecheza mechi 1 zaidi.Manu iliilaza Burnley mabao 3-0.Arsenal inanawafukuzia sana kileleni na inaweza keshokutwa Jumatano ikitamba mbele ya Bolton Wanderes, nyumbani inaweza wao kuparamia kileleni.

LIGI YA TANZANIA IMERUDI UWANJANI:

Nchini Tanzania, Ligi kuu imeanza duru yake ya pili na ya mwisho kwa kishindo huku Símba na mahasimu wao wa jadi Young Africans ,wakianza ubishi wao wa kutaka kupanda kileleni mwa kilimanjaro-Ligi ya Tanzania:

Mwandishi: Ramadhan Ali/RTRE/AFPE

Uhariri: Othman Miraji