Kituo cha jeshi la Marekani chashambuliwa Iraq | Matukio ya Kisiasa | DW | 03.03.2021
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Kituo cha jeshi la Marekani chashambuliwa Iraq

Muungano wa kijeshi unaoongozwa na Marekani nchini Iraq umethibitisha kushambuliwa kituo chake cha anga kwa makombora yapatayo 10, siku chache baada ya wao kuwashambulia wanamgambo wanaoungwa mkono na Iran.

Maroketi hayo yalikipiga kituo cha jeshi la anga la Ain Al-Asad katika jimbo la Anbar majira ya saa 1:20 asubuhi ya Jumatano (3 Machi), kwa mujibu wa msemaji wa muungano huo wa kijeshi, Kanali Wayne Marotto, aliyeongeza kwamba "vikosi vya usalama vya Iraq vinaongoza uchunguzi juu ya mashambulizi hayo."

Baadaye, jeshi la Iraq lilitowa taarifa likisema mashambulizi hayo hayakusababisha maafa makubwa na kwamba vyombo vya usalama vilifanikiwa kugundua sehemu ambayo ilitumika kurusha makombora hayo, huku afisa mmoja wa jeshi la Iraq akisema sehemu hiyo ipo kwenye eneo la al-Baghdadi katika jimbo la Anbar.

Hayo ni mashambulizi ya kwanza tangu Marekani kuyashambulia maeneo ya wanamgambo wanaoungwa mkono na Iran kwenye mpaka wa Iraq na Syria wiki iliyopita na kumuuwa mwanamgambo mmoja na yale ya nchini Syria yaliyowauwa wapiganaji wengine 22.

Mashambulizi hayo ya Marekani yalizusha wasiwasi wa kuzuka mkururo wa mashambulizi kama hayo ya kulipizana kisasi yaliyotokea mwaka jana, na kumalizikia kwa Marekani kumuuwa Jenerali Qassim Soleimani wa Iran karibu na uwanja wa ndege wa Baghdad.

Mashambulizi ya Jumatano yalikilenga kituo kile kile ambacho Iran ilikishambulia kwa makombora kadhaa Januari mwaka jana kulipiza kisasi mauaji ya Jenerali Soleimani, ambapo wanajeshi kadhaa wa Marekani walijeruhiwa.

Mashambulizi hayo pia yamefanyika ikiwa ni siku mbili tu kabla ya ziara ya Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani, Papa Francis, nchini Iraq, ambayo inatazamiwa kujumuisha mji mkuu Baghdad, kusini na mji wa kaskazini wa Irbil.

Kulipizana visasi

Irak | Ain al-Asad Militärbasis

Kambi ya jeshi la anga la vikosi vya washirika linaloongozwa na Marekani katika eneo la Ain al-Asad nchini Iraq.

Mashambulizi yaliyofanywa na Marekani wiki iliyopita kwenye eneo la mpakani yalikuwa ni kujibu mashambulizi ya maroketi yaliyolenga maeneo ya kimkakati ya jeshi la Marekani nchini Iraq, yakiwemo yale yaliyomuua mhandisi wa Kifilipino aliyekuwa akiufanyia kazi muungano wa kijeshi wa Marekani katika uwanja wa ndege wa Irbil.

Baada ya mashambulizi hayo, Wizara ya Ulinzi ya Marekani ilisema ni hatua ya kijeshi iliyochukuliwa baada ya kushauriana na washirika wao. 

Marekani ilipunguza idadi kubwa ya wanajeshi wake nchini Iraq mwaka jana, kufuatia uamuzi wa utawala wa Trump kuondosha vikosi vyake kutoka vituo kadhaa na kujikita zaidi kwenye kambi ya jeshi la anga ya Ain Al-Asad na Baghdad.

Maroketi yaliyorushwa mara kwa mara kuelekea eneo lenye ulinzi mkali kabisa liitwalo Ukanda wa Kijani, na ambalo lina majengo ya ubalozi wa Marekani mjini Baghdad, liliufanya utawala wa Trump kutishia kufunga ubalozi huo na kuelekea kwenye mapigano ya moja kwa moja.