Kimbunga kipya Rita chahofiwa kupiga ghuba ya jimbo la Texas nchini Marekani,Jumamosi
23 Septemba 2005
Wakati huo huo wabunge nchini Marekani pamoja na watetezi wa maslahi ya wanyama nchini humo, wametoa mwito wa kuwepo mikakati ya kuwalinda wanyama wanaonaswa katika majanga ya kiasili.
Kimbunga Rita kinahofiwa kuingia kwa kasi katika ghuba ya jimbo la Texas na pia katika maeneo ya machimbo ya mafuta kikiwa na mwendo wa kasi ya kilomita 145 kwa saa.
Maelfu ya watu wameanza kuuhama mji huo wa nne kwa ukumbwa nchini Marekani . Mapema Jumatano, viongozi wa majimbo ya Texas na Louisiana wamewatolea mwito raia wapatao milioni mbili kuondoka katika maeneo ya pwani kabla ya kimbunga Rita kuwasili.
Maafisa wa jimbo la Texas wanatarajiwa kusafirisha zaidi ya lita laki mbili za gesi kwa ajili ya kuhudumia vituo ambavyo vimekabiliwa na upungufu wa mafuta.
Wataalamu wa masuala ya hali ya hewa, wanasema kwamba kimbunga Rita kitakuwa na nguvu sawa na kimbunga Katrina kilichopiga maeneo ya Pwani Kusini mwa Marekani wiki tatu zilizopita.
Taarifa zinasema kuwa kimbunga Rita kitapiga katika mpaka wa jimbo la Texas na Louisiana kesho Jumamosi.
Wakati huon huo mwanasayansi mmoja wa Uingereza John Lawton, amesema kwamba wimbi la vimbunga ambalo sasa linayaathiri maeneo ya Kusini mwa Marekani, linatokana na ongezeko la joto Duniani. Mwanasayansi huyo amekosoa sera za rais George Bush za kupuuza suala hilo.
Bwana John Lawton ambaye ni mwenyekiti wa tume inayoshughulikia kupambana na uchafuzi wa mazingira na kutoa ushauri wa serikali ya Uingereza, ameulaumu utawala wa Marekani kwa kile alichosema ni kushindwa kwake kutilia maanani athari za ongezeko la joto Duniani, hali ambayo sasa inaathiri watu wasio na hatia.
Katika kipindi kisichotimia mwezi mmoja baada ya kimbunga Katrina kupiga na kuangamiza maeneo ya pwani Kusini mwa Marekani, kimbunga kipya kinachojulikana kama Rita, kinakaribia kupiga Ghuba ya Mexico na hata maeneo ya kati ya Marekani kuliko na machimbo ya mafuta.
Amebainisha mwanasayansi huyo, ambaye amesema kuwa kupinga athahari za ongezeko la joto Duniani, ni sawa na kupinga kwamba uvutaji wa sigara husababisha kansa ya mapafu.
Sera za mabadiliko ya hali ya hewa zimemtenga rais wa Marekani George Bush na viongozi wengine wa Dunia, ambao wamekwisha tia saini mkataba wa Kyoto wa Umoja wa mataifa, juu ya kupunguza uchafuzi wa hewa kutokana na moshi unaotokana na viwanda.
Rais Bush alipuuza mkataba huo mwaka 2001 akisema kuwa ni gharama kubwa.
Hata hivyo kiongozi huyo wa Marekani anatarajiwa kuzulu jimbo la Texas leo kutathimini maandalizi ya kukabiliana na athari za kimbunga kipya Rita.
Wakati haya yakiarifiwa, wabunge pamoja na watetezi wa maslahi ya wanyama nchini Marekani, wanataraji kuwashinikiza maafisa wa masuala ya dharura nchini humo kutafakari usalama wa wanyama walionaswa na mafuriko yaliyotokana na kimbunga Katrina.
Mawakili wanaotetea ustawi wa wanyama wamewalaumu viongozi katika majimbo ya Louisiana , Mississippi na Alabama kwa kuwalazimisha watu kuhama makaazi yao huku wakiacha nyuma mifugo yao ambayo imekufa kwa njaa, magonjwa na hata wengine kufa maji kutokana na mafuriko.
Wabunge wa chama cha Republikani wamesema kwamba utawala wa rais Bush hauna budi kujifunza kutokana na makosa yaliyopita wakati kimbunga Katrina kilipopiga maeneo ya pwani ya Kusini mwa Marekani na kuepuka mtego kama huo.
Wamesema mara hii watu hawana budi kuchukua mikakati imara ya kuweka misaada ya dharura na kuwaokoa watu pamoja na mifugo yao.
Huku kukiwa na wasiwasi wa kimbunga kipya kupiga maeneo ya pwani katika jimbo la Texas, watu walionusurika na kimbunga Katrina katika mji wa New Orleans pamoja na maafisa wa mji huo wanahofia kwamba maeneo hayo huenda yakakabiliwa na mafuriko mengine.