Kameroun-simba wa nyika watatamba mbele ya Holland ? | Michezo | DW | 09.06.2010
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Michezo

Kameroun-simba wa nyika watatamba mbele ya Holland ?

Simba wanyika wako kundi E:Holland,Japan na Denmark.

default

Kamerouna Misri:Kombe la Afrika 2010

Simba wa nyika-Kameroun, wanaelewa ndio wafalme wa msituni.Jukumu lao Afrika nzima inawatazamia kutekeleza, sio tu kunguruma katka Mbuga ya Kruger Park,Afrika Kusini kundi E na kuitoa Holland,bali kupindukia pale ilipofika 1990 nchini Itali,robo finali ilipoilaza hata Argentina na Maradona.

Mara hii lakini simba wao mkongwe mzee Roger milla, atakuwa nje ya chaki ya uwanja akiwashangiria tu kinyume na 1990.Isitoshe, Milla amekorofishana majuzi na mshambulizi Samuel Eto-o.Nini hatim,a basi ya simba wa nyika katika Kombe hili la dunia ?

Ni Seenegal tu iliowaigiza simba wa nyika pale nao walipofululiza hadi robo-finali ya Kombe la dunia 2002 huko Korea ya Kusini na Japan na kuzimwa mwishoe na Uturuki.Lakini sio kabla mpira kurefushwa na bao la kitanzi la "Golden Goal".

Kura ya kukatisha tamaa iliopigwa Desemba mwaka jana ,imezitosha timu 6 za Afrika katika m akundi mazito.Kwahivyo, simba wa nyika watabidi kunoa kweli makucha na kuipiku holland ,Denmark na japan kwa tiketi ya duru ya pili.Na simba wakiingia duru ya pili, wanajua porini Afrika, simba pekee ni wao.Holland,iliikomea Ghana majuzi mabao 4:1 na kuipelekea salamu kameroun kwamba, "ukimuona mwenzako anyaolewa,basi nawe tia maji."

Tukitumai Kameroun, salamu za wadachi wamezipata .Kocha wa Kameroun, mfaransa Paul le Guen, alieiongoza Lyon kutwaa ubingwa mara tatu nchini Ufaransa,ilipopigwa kura mwaka jana huko Cape Town, alisema hili ni kundi linaloweza kuwa gumu na pia kuwa rahisi.

Simba wa nyika wanasifa kuwa na mastadi wazuri wa dimba,ari na nidhamu imetengenea tangu misukosuko yao ya Kombe lililopita waliposhindwa kuja Ujerumani.

Kameroun, inasema hili ni Kombe maalumu kwao,kwavile, linaaniwa Afrika.

Kameroun ,hatahivyo, ilipigwa kumbo katika robo-finali ya Kombe la Afrika nchini Angola,mapema mwaka huu na majuzi kulizuka mfarakano kati ya stadi wao Samuel Eto-o wa klabu bingwa ya ulaya Inter Milan na mzee Roger Milla,simba-mkongwe. Milla, aliuliza :"Eto-o kafanya nini kwa Kameroun ? Milla anaungama kwamba, Eto-o, ametamba na FC Barcelona na Inter Milan kwa kutawazwa mara 3 mabingwa wa ulaya.

Samuel Eto-o alikasirika na kumjibu Milla mbali ya mabao yake 4, 1990,huko Itali, kafanya nini zaidi katika dimba ?.

Eto-o, alitishia kufikiria iwapo acheze katika Kombe hili la dunia.Lakini, atateremka uwanjani na pengine, kumuonesha mzee Milla, nani Eto-o hata akivaa jazi ya Kameroun.

Kocha Le guen , amefanya mabadiliko katika kikosi cha simba wa nyika na amemvua taji la unahodha mzee Riggobert Song na kumvika Samuel Eto-o.Hivyo, Eto-o, anaelewa ana jukumu la kutoizamisha jahazi yake. Miongoni mwa walinzi wa zamani na bado wapo, ni Geremi Njitap, alieizamisha Kameroun kwa bao la uzembe langoni mwake pale Kameroun, ilipocheza na Misri,huko Angola.

Kipa Carlos Kameni, bila shaka, ni tumbuu madhubuti langoni.Halafu kuna wachezaji 2 wa Tottenham :Sebastian Bassong na Benoit Assou-Ekotto ambao wana hakika ya kutamba uwanjani.

Alexandre Song wa Arsenal na Achile Emana wa Real Betis , watazamiwa kuwa miongoni walioteuliwa kucheza kati ya uwanja.Idrissou, anaecheza katika Bundesliga ,atamsaidia Eto-o usoni kupiga hodi katika lango la Holland,Denmark na Japan na kutumai, kuitikiwa "karibu".

Mwandishi: Ramadhan Ali:AFPE

Uhariri: Aboubakary Liongo

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com