Juhudi za amani ya Mashariki ya kati | Matukio ya Kisiasa | DW | 25.08.2008
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Juhudi za amani ya Mashariki ya kati

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani ahimiza utaratibu wa amani kati ya Israel na Palastina

Israel yawaachia huru wafungwa 198 wa kipalastina

Israel yawaachia huru wafungwa 198 wa kipalastinaWaziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani amewasili Mashariki ya kati hii leo kuhimiza utaratibu wa amani kati ya Israel na Palastina.Ziara yake imesadif na kuachiliwa huru waplastina 198 waliokua wakishikiliwa korokoroni nchini Israel.


Israel imewaachia huru wafungwa hao kwa lengo la kumuimarishia umaarufu kiongozi wa utawala wa ndani wa Palastina Mahmoud Abbas na kuwatanabahishia wapalastina mazungumzo ya amani yanaweza kuleta tija..


Miongoni mwa walioachiliwa huru anakutikana pia Said Atabeh,mwanachama wa zamani wa Vugu vugu la kidemokrasi la kupigania ukombozi wa Palastina,mwenyed umri wa miaka 57.


"Ni furaha kubwa kwa mama zetu na umma wetu,hata hivyo ni hatua ndogo tuu,kwasababu tumewaacha nyuma maelfu ya wafungwa wa kipalastina" amesema hayo Atabeh aliyekua amehukumiwa kifungo cha maisha mnamo mwaka 1977 kwa makosa ya kushiriki katika shambulio lililogharimu maisha ya bibi mmoja wa kiisrael na kuwajeruhi dazeni kadhaa wengine.


"Si rahisi kuwaachia huru wafungwa,hasa wale waliohusika moja kwa moja na visa vya kigaidi vilivyogharimu maisha ya raia wasiokua na hatia" amesema kwa upande wake Mark Regev ambae ni msemaji wa waziri mkuu wa Israel Ehud Olmert.


Wafungwa wote 198,wakiwemo wanne wanawake,wamepokelewa Moqataa,makao makuu ya utawala wa ndani wa Palastina huko Ramallah,wakishangiriwa na umati wa wapalastina.


"Hakuna anaebisha,tunataka amani,lakini hakuna amani bila ya wafungwa wote kuachiwa huru" amesema kiongozi wa utawala wa ndani Mahmoud Abbas katika sherehe za mapokezi.


Wafungwa 11 elfu wa kipalastina bado wanashikiliwa nchini Israel.


Wafungwa hao wameachiwa huru muda mfupi tuu kabla ya kuwasili Mashariki ya kati waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani,bibi Condoleezza Rice.


Mara tuu baada ya kuwasili,waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani alielekea Jerusalem kwa mazungumzo pamoja na mkuu wa tume ya Palastina katika mazungumzo ya amani Ahmed Qorei,kabla ya kurejea Tel Aviv kukutana na waziri wa ulinzi wa Israel Ehud Barak.


Kesho jumanne waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani Condoleezza Rice atakua na mazungumzo pamoja na waziri mkuu Ehud Olmert mjini Jerusalem na baadae atakwenda Ramallah kwa mazungumzo pamoja na rais wa Palastina Mahmoud Abbass.


Akizungumza na waandishi habari mara baada ya kuwasili Tel-Aviv,waziri Condoleezza Rice amefifiisha nafasi ya kufanikiwa juhudi hizo japo kwa sehemu,kabla ya mkutano wa hadhara kuu ya Umoja wa mataifa,utakaoanza September 11 hadi october mosi ijayo mjini New-York.


"Ni muhimu kupita kiasi kuendelea kupiga hatua mbele ,lengo letu ni lile lile,nalo ni kufikia makubaliano ya amani hadi mwaka huu utakapomalizika" amesema waziri huyo wa mambo ya nchi za anje wa Marekani na kumaliza tunanukuu:"bado kuna mengi ya kufanya"Mwisho wa kumnukuu.


Hii ni ziara ya 18 ya Condoleezza Rice katika eneo hilo na ya sabaa tangu utaratibu wa amani ulipofufuliwa upya November mwaka jana huko Annapolis Marekani. • Tarehe 25.08.2008
 • Mwandishi Hamidou, Oumilkher
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/F4Xd
 • Tarehe 25.08.2008
 • Mwandishi Hamidou, Oumilkher
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/F4Xd
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com