Iran: Wanaharakati wa Mazingira wafungwa jela | Matukio ya Kisiasa | DW | 18.02.2020
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Iran: Wanaharakati wa Mazingira wafungwa jela

Mahakama moja nchini Iran imewahukumu wanaharakati wanane wa mazingira kifungo cha kati ya miaka minne na kumi gerezani kwa tuhuma za kushirikiana na serikali ya Marekani.

Msemaji wa idara ya sheria nchini Iran, Gholamhossein Esmaili, amesema wanaharakati hao watatumikia kifungo gerezani na wakati huo huo wanatakiwa kurudisha serikalini pesa zote walizopokea kutoka kwa serikali ya Marekani ambayo inachukuliwa kuwa ni adui wa serikali ya Iran.

Watu hao waliohukumiwa walikuwa wafanyakazi kwenye wakfu unaoshughulikia masuala ya Mazingira "Persian Wildlife Heritage Foundation" na kazi yao ilikuwa ya kufuatilia viumbe vya porini vilivyo hatarini kutoweka na walikamatwa kutokana na tuhuma za ujasusi. Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limesema wanaharakati hao wa mazingira walitiwa nguvuni nchini Iran mnamo Januari na Februari 2018 na wakati wote huo walikuwa wamezuiliwa gerezani bila ya kufunguliwa mashtaka.

Ujerumani na Iran zabadilishana wafungwa

Katika hatua nyengine, msemaji wa idara ya sheria ya nchini Iran Gholamhossein Esmaili ametangaza kwamba raia mmoja wa Ujerumani ameachiwa huru baada kuanza kutumikia kifungo cha miaka mitatu gerezani. Raia huyo wa Ujerumani alikuwa akizuiliwa nchini Iran muda mrefu uliopita, kutokana na makosa ya kupiga picha na kurekodi video za maeneo nyeti.

Idara ya sheria ya Iran imesema mahakama ilitumia uwezo wake wa kisheria kumuachia raia huyo wa Ujerumani na sasa atarejea nchini mwake. Esmaili amesema raia huyo wa Ujerumani ameachiwa baada ya kufikiwa makubaliano ya kubadilishana wafungwa kati ya Iran na Ujerumani.

Raia wa Iran Ahmad Khalil, alifungwa nchini Ujerumani kwa tuhuma za kukiuka vikwazo vya Marekani na alikamatwa kwa ombi kutoka mjini Washington. Raia huyo wa Iran alikuwa anasubiri kupelekwa Marekani ambako angeshtakiwa kwa makosa hayo. Khalil aliruhusiwa kurejea nyumbani siku ya Jumapili akiongozana na Waziri wa Mambo ya nje wa Iran, Mohammad Javad Zarif, ambaye alikuwa anahudhuria mkutano wa usalama wa mjini Munich.

Vyanzo:/AFP/https://p.dw.com/p/3XvGi