1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hotuba ya rais wa shirikisho kuhusu wahamiaji ingali bado inawashughulisha wahariri wa magazeti humu nchini

Oumilkher Hamidou6 Oktoba 2010

Juhudi za kuwajumuisha wahamiaji na hasa waislam katika maisha ya kila siku ya jamii sawa na vitisho vbya kuzuka mashambulio ya kigaidi ni miongoni mwa mada magazetini

https://p.dw.com/p/PWfQ
Afisa wa polisi anachunguza mambo katika sherehe za bija mashuhuri kwa jina la Sherehe za October" mjini Munich,kusini mwa UjerumaniPicha: AP

Tuanzie lakini na hotuba ya rais wa shirikisho la jamhuri ya Ujerumani aliyoitoa Bremen katika sherehe za kuadhimisha miaka 20 ya muungano wa Ujerumani, october tatu iliyopita.Hotuba hiyo imepalilia mijadala kuhusu suala hilo katika jamii na kuwashughulisha zaidi pia wahariri-kama kwa mfano mhariri wa gazeti la "Rheinische Post" la mjini Düsseldorf anaesema:

Rais wa shirikisho ameipata mada aipendayo:yaani kujumiishwa wahamiaji katika maisha ya kila siku ya jamii.Aliyoyasema katika hotuba yake kuadhimisha miaka 20 ya muungano wa Ujerumani yamepata msukumo.Timu ya taifa ya Ujerumani inaonyesha kuwa mfano wa kuigizwa na unaoambatana na msimamo wa rais wa shirikisho.Miongoni mwa wachezaji wa timu hiyo ya taifa kuna wenye asili ya Poland,Tunisia,Uturuki,Ghana,Brazil na Bosnia pia.Katika michuano ya kombe la dunia wameteremka kwa furaha na kama kitu kimoja na huo ni mfano mzuri wa jinsi jamii nzima inavyopaswa kuwa.

Gazeti la "Nürnberger Zeitung" lina maoni mengine kabisa na linaandika:

"Ingawa hivi sasa kuna makamishna wa polisi wenye asili ya kituruki na vituo vingi zaidi vya nyama choma ya kituruki kuliko vile vya nyama ya soseji ya nguruwe,hata hivyo bado watu wana shaka shaka na wafuasi wa dini ya kiislam.Pengine kwasababu katika misikiti mingi,maimam hawaelewi kijerumani.Wanajua kweli kuhusu sheria msingi,na uhuru wa mtu kuabudu dini aitakayo?Bila ya shaka kuna waislam walioelimika na ambao wanatambua umuhimu wa kutenganisha shughuli za serikali na zile za kidini.Lakini kwa wakati wote ule ambao bado watakuwepo waislam wengi ambao watang'ang'ania maisha ya jadi,basi haitakua rahisi pia kujipatia nafasi katika ulimwengu wa magharibi.

Mada yetu ya pili magazetini inahusu onyo la kutokea mashambulio ya kigaidi ya wafuasi wa itikadi kali ya dfini ya kiislam.Na gazeti la "Hannoversche Allgemeine Zeitung" linaandika:

Msako ni sawa na kutafuta sindano iliyodondoka ndani ya mchanga.Lakini sheria zilizofanayiwa marekebisho wakati wa utawala wa serikali ya muungano wa vyama vikuu zinarahisisha mambo.Inatosha kumdhania mtu ana azma ya kufanya mashambulio ya kigaidi,akikutikana na silaha au miripuko.Pia juhudi za kuwasaka watuhumiwa zimerahisishwa kutokana na ushirikiano wa watumishi wa idara za upelelezi kote ulimwenguni.Kwa miaka eneo la waziristan kwa mfano lilikua haliingiliki,ilikua ngome ya wafuasi wa itikadi kali.Hivi sasa eneo hilo linamulikwa na kuchunguzwa kwa msaada wa zana za elektroniki.Pengine nchi za magharibi zina wasi wasi wasi,lakini hata wafuasi wa itikadi kali wakilala hawapati usingizi.

Mada yetu ya mwisho inahusiana na idadi ya wanafunzi waliojiandikisha msimu huu katika vyuo vikuu vya jimbo hili la Northrhine Westfalia .Gazeti la "Westdeutsche Zeitung" linaandika:

Tarakimu zilizotangazwa na wizara ya elimu ya juu zinatia wasi wasi.Takriban thukluthi mmoja tuu ya wanafunzi wenye haki ya kwenda vyuo vikuu ndio waliojiandikisha.Idadi hiyo ni ndogo sana ikilinganishwa na tarakimu kama hizo katika vyuo vyengine vikuu humu nchini.Mtu akitupia macho Bayern au katika jimbo la Rhinland Pfalz hatokosa kutambua kwamba majimbo mengine yana tarakimu tofauti,yanawapatia elimu vijana ambao ni muhimu kwa maendeleo ya maeneo hayo.

Mwandishi:Hamidou,Oummilkheir/ Dt Agenturen

Mpitiaji:M.Abdul-Rahman