1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hifadhi ya Snowden yazua uhasama kati ya Marekani na Urusi

2 Agosti 2013

Uamuzi wa Urusi wa kumpa mfichua siri za Marekani Edward Snowden hifadhi umeighadhabisha serikali ya Marekani na bunge la nchi hiyo na kuzua wasiwasi kuwa uhusiano kati ya nchi hizo mbili utazoroteka hata zaidi.

https://p.dw.com/p/19Ifd
Picha: picture-alliance/dpa

Baada ya Snowden kuondoka katika eneo la kubadilishia ndege ndani ya uwanja wa ndege wa Moscow na kuingia nchini Urusi rasmi hapo jana,ikulu ya Rais wa Marekani ilitoa taarifa kuwa imevunjwa moyo kabisa na kudokeza kuwa huenda Rais Obama asikutane na mwenzake wa Urusi Vladimir Putin kabla ya mkutano wa nchi 20 zilizostawi kiuchumi G20 unaopangiwa kufanyika mjini Moscow mwezi ujao.

Wabunge wa Marekani wametishia hata zaidi,wakitaka Urusi iachilie haki zao za kuuandaa mkutano huo na kutilia shaka iwapo baada ya hatua hiyo ya Urusi ya kumpa hifadhi Snowden nchi hizo mbili zitashirikiana kwa lolote.

Wamarekani waghdahbishwa na hatua ya Urusi

Seneta wa chama cha Republican John Mcain amesema uamuzi huo ni fedheha na imefanywa kimakusudi kuiaibisha Marekani na ni pigo kwa wamarekani wote na kuongeza kuwa ni wakati wa kutathmini upya uhusiano kati ya nchi hizo mbili.

Rais wa Marekani Barrack Obama.Serikali yake imeghadhabishwa na Urusi kumpa Snowden hifadhi
Rais wa Marekani Barrack Obama.Serikali yake imeghadhabishwa na Urusi kumpa Snowden hifadhiPicha: REUTERS

Hata hivyo iwapo Marekani haikuwa tayari kufutilia mbali uhusiano wake na Urusi kutokana na masuala ya silaha za makombora,haki za binadamu au misimamo yao tofauti kuhusu vita vya Syria,hili la Snowden halionekani litaweza kuvunjilia mbali mahusiano kabisa kati ya mahasimu hao wa jadi.

Rais Putin ambaye amekuwa madarakani kwa zaidi ya muongo mmoja sasa ameuthibitishia ulimwengu kuwa atajibu shutuma na hatua zozote Marekani itazielekeza kwa nchi yake kupitia nguvu zake kisilaha au kidiplomasia hasa ikija katika suala la ushawishi wa Urusi katika mataifa mengine kama Ukraine,Georgia na mataifa mengine jirani.

Putin ana ushawishi mkubwa

Na licha ya cheche za maneno kutoka Marekani,nchi hiyo inafahamu fika inamhitaji Putin kuendeleza masuala kadhaa ya kiusalama wa taifa na imejaribu kufunika hisia zake kuhusu uchokozi wa Urusi.

Rais wa Urusi Vladimir Putin
Rais wa Urusi Vladimir PutinPicha: Y.Lapikova/AFP/GettyImages

Bila ya usaidizi wa Urusi,Marekani itakuwa na wakati mgumu kuyadhibiti makundi ya kigaidi ya Amerika ya kusini,kupata vyanzo vingi vya majeshi yake kuingia Afghanistan,kuizuia Iran kutengeneza silaha za kinyuklia na pia itapoteza nafasi zote za kumshawishi Rais wa Syria Bashar al Assad kukaribia meza ya mazungumzo na waasi kutafuta amani itakayomaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Maoni ya kwanza ya Marekani kuhusu hifadhi ya Snowden yalikuwa ya shutuma ila kwa uzingativu.Msemaji wa ikulu ya rais wa Marekani Jay Carney alisema

Hata hivyo hata Putin ameonekana kujaribu kuepusha mzozo zaidi na marekani kwani kabla ya uamuzi wa hapo jana alikuwa amesema hifadhi itatolewa kwa mfichua huyo wa siri za kijasusi iwapo tu atasita kufichua mengi zaidi kuhusu mpango huo wa udukuzi wa Marekani.

Mwandishi:Caro Robi/ap/reuters

Mhariri:Josephat Charo