1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIran

Nyuklia: Mazungumzo kati ya Marekani na Iran kufanyika Rome

30 Aprili 2025

Iran na Marekani zinatarajiwa kuanza tena mazungumzo kuhusu mpango wa nyuklia wa Tehran mjini Rome mwishoni mwa wiki hii.

https://p.dw.com/p/4tmXJ
Iran Teheran 2025 | Außenminister Abbas Araghchi telefoniert bei einer Zeremonie
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi, akizungumza kwa simu wakati wa hafla iliyofanyika magharibi mwa Tehran, IranPicha: Morteza Nikoubazl/NurPhoto/IMAGO

Hayo yamesemwa leo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Abbas Araghchi.

Mwanadiplomasia huyo wa Iran amesema pembezoni mwa kikao cha Baraza la Mawaziri leo kwamba duru ya mazungumzo kati ya Washington na Tehran, yanayosimamiwa na Oman, yamepangwa kufanyika Jumamosi ijayo katika mji mkuu wa Italia, Rome.

Marekani hata hivyo haijatoa tamko lolote kuhusu suala hilo. Mkutano tofauti na wawakilishi kutoka Ujerumani, Ufaransa na Uingereza umepangwa kufanyika siku ya Ijumaa.

Soma pia: Iran yapendekeza mazungumzo ya nyuklia na nchi za Ulaya 

Ingawa hakukuwepo na uthibitisho kutoka Wizara ya mambo ya nje ya Ujerumani, tovuti ya habari ya Iran ya Iran Nuances imeripoti kuwa mazungumzo hayo yatafanyika katika ngazi ya manaibu mawaziri wa mambo ya nje.

Mataifa hayo matatu ya Ulaya yalikuwa miongoni mwa yaliosaini makubaliano muhimu ya nyuklia ya mwaka 2015 kati ya Iran na mataifa mengine sita yenye nguvu, yaliyo na lengo la kuizuia Iran kutengeneza silaha za nyuklia.