Dilma Rousseff amechaguliwa kuwa rais wa Brazil na kugeuka kuwa rais wa kwanza wa kike katika nchi hiyo kubwa ya Amerika kusini | Matukio ya Kisiasa | DW | 01.11.2010
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Dilma Rousseff amechaguliwa kuwa rais wa Brazil na kugeuka kuwa rais wa kwanza wa kike katika nchi hiyo kubwa ya Amerika kusini

Rais mpya wa Brazil aahidi kufuata nyayo za mtangulizi wake na kutoigusa bajeti ya huduma za jamii na miundo mbinu

Bibi Dilma Rousseff,mshindi wa uchaguzi wa rais nchini Brazil

Bibi Dilma Rousseff,mshindi wa uchaguzi wa rais nchini Brazil

Na sasa tunaelekea Brazil ambako kwa m,ara ya kwanza katika historia ya nchi hiyo,mwanasiasa wa kike-Dilmaq Rousseff amechaguliwa kuwa rais wa nchi hiyo ya Amerika ya Kusini.

Dilma Rousseff,aliyechaguliwa jana kuwa rais wa Brazil,ameelezea azma ya kufuata nyayo za mtangulizi wake Lula,na kudhamini maendeleo ya kiuchumi na kijamii yaliyoppelekea Brazil kuifikia daraja ya "dola kuu linaloinukia."

Akipanda kutokana na umashuhuri wa mtangulizi wake,Luiz Inacio Lula da Silva,mgombea huyo wa kutoka chama tawala cha wafanyakazi PT,amejikingia asili mia 56 ya kura dhidi ya asili mia 36 za mpinzani wake,wa kutoka chama cha Social Democratic,José Serra.

Wafuasi wa Rousseff walimiminika kwa maelfu katika barabara za Sao Paulo na Brazilia kuonyesha furaha yao na kusherehekea ushindi wao.

Akihutubia kwa mara ya kwanza baada ya matokeo jumla kutangazwa,rais huyo mteule mwenye umri wa miaka 62,aliyekua akionyesha ameduwaa na machozi yakimlenga lenga , ameahidi kufyeka umasikini hadi mhula wake utakapomalizika miaka minne kutoka sasa.

Ameahidi kuendeleza kile alichokiita "enzi ya neema" na kuheshimu mikataba iliyoko akisisitiza hana azma ya kuipa kisogo siasa iliyokuwa ikifuatwa na Lula.

Rais mteule Dilma Rousseff anaendelea kusema:

"Serikali yangu itazidisha bidii katika masuala yote yanayohusiana na masilahi ya jamii.Idara za uchunguzi zitaendesha shjughuli zao bila ya kuwaandama wapinzani na bila ya kuwakinga marafiki."

Brasilien / Rousseff / Präsidentschaft / NO-FLASH

Rais mteule baada ya matokeo ya uchaguzi kutangazwa

Bibi Rousseff aliyewaahi kufungwa miaka mitatu jela kutokana na harakati zake za ukombozi amekuwa mwanamke wa kwanza kuongoza mustakbal wa dola hilo kuu la kiuchumi la Amerika ya kusini.

Mtaalam huyo wa kiuchumi aliyewahji pia kuwa waziri wa mazingira amerithi hali ya kutia moyo iliyofuatia mihula miwili ya mtangulizi wake Lula.:Idadi ya wasiokua na kazi imefikiwa kiwango ncha chini kabisa cha asili mia 6,2,watu zaidi ya milioni 20 wametoka katika hali ya umaskini tangu mwaka 2003 na kuibuka jamii ya tabaka ya kati inafikia zaidi ya nusu ya wakaazi wa Brazil.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/afp,Reuters

Mpitiaji:Josephat Charo

 • Tarehe 01.11.2010
 • Mwandishi Oumilkher Hamidou
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/PvNf
 • Tarehe 01.11.2010
 • Mwandishi Oumilkher Hamidou
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/PvNf
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com