Chanjo ya Covid kuwafikia watu wote Ujerumani kufikia mwezi Juni | Matukio ya Kisiasa | DW | 23.04.2021
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Chanjo ya Covid kuwafikia watu wote Ujerumani kufikia mwezi Juni

Ujerumani itatoa chanjo ya Covid-19 kwa watu wazima wote kufikia mwezi juni wakati rais Frank-Walter Steinmeier akisaini marekebisho ya sheria yanayoipa serikali ya shirikisho mamlaka zaidi kuanzisha vizuizi vya dharura

Ujerumani inatarajiwa kutoa chanjo ya Covid-19 kwa watu wazima wote kufikia mwezi juni wakati rais Frank-Walter Steinmeier akisaini marekebisho ya sheria ambayo inaipatia serikali ya shirikisho mamlaka zaidi ya kuanzisha vizuizi vya dharura nchi nzima vya kukabiliana na ugonjwa huo. 

Waziri wa afya wa Ujerumani Jens Spahn alilieleza baraza la juu la bunge la Ujerumani kwamba chanjo dhidi ya virusi vya corona inaweza kupatikana kwa wananchi wote ambao wako tayari kuchanjwa kufikia mwezi Juni. Kulingana na takwimu zilizotolewa, hadi kufikia sasa ni karibu asilimia 21.6 ya idadi ya wakaazi wa Ujerumani ambao tayari wamepatiwa dozi ya kwanza.

Wakati huohuo rais wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier Alhamis, alisaini marekebisho ya sheria ambayo ilipitishwa na baraza la juu la bunge la Ujerumani, na kuipatia serikali ya shirikisho mamlaka zaidi ya kuanzisha vizuizi vya nchi nzima vya kukabiliana na Covid-19. Marekebisho hayo ya sheria yalichochea maandamano makubwa mjini Berlin siku ya Jumatano.

Fernsehansprache Bundespräsident Steinmeier

Rais wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier

Miongoni mwa hatua zinazoweza kuchukuliwa ni marufuku ya nchi nzima ya kutotoka nje usiku katika maeneo ambayo yana idadi kubwa ya maambukizi pamona na shule kufungwa. Taasisi ya udhibiti wa magonjwa ya kuambukiza ya Robert Koch jana ilitangaza maambukizi mapya elfu 29, 518 katika kipindi cha saa 24 zilizopita.

Kwingineko Canada imezizuia ndege zote zinazotoka India na Pakistan kwa siku 30 kutokana na ongezeko la maambukizi ya COVID-19 katika ukanda huo. Marufuku hiyo imeanza kutekelezwa Alhamis jioni, ikiwa ni saa chache baada ya India kuripoti maambukizi mapya zaidi ya laki tatu katika saa 24 zilizopita.

Wizara ya afya ya Canada imesema nusu ya watu walioambukizwa COVID wanaowasili kwa ndege wanatokea India na idadi kubwa pia kutoka Pakistan. Kasi ya utoaji chanjo imeongezeka nchini Canada, lakini wataalam wa afya wanasema aina mpya ya virusi na kushindwa kuchukua hatua sahihi dhidi ya virusi kumesababisha wimbi la tatu la maambukizi

Umoja wa Falme za Kiarabu nao pia umezuia ndege zote kutoka India kutokana na wasiwasi huo. New Delhi imetoa onyo kwamba wagonjwa wanaweza kufariki ikiwa vifaa vya oksijeni katika hospitali havitaongezwa. Mfumo wa afya nchini humo unatajwa kuzidiwa na wimbi la pili lililochangiwa na aina mpya ya virusi vinavyoenea kwa kasi.