Bush aondoka Ujerumani | NRS-Import | DW | 11.06.2008
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

NRS-Import

Bush aondoka Ujerumani

Rais George Bush wa Marekani ameondoka Berlin akielekea Roma, Italy

Rais George Bush wa Marekani na Kansela Angela Merkel wa Ujerumani katika mkutano wa waandishi wa habari huko Meseberg, karibu na Berlin, Ujerumani

Rais George Bush wa Marekani na Kansela Angela Merkel wa Ujerumani katika mkutano wa waandishi wa habari huko Meseberg, karibu na Berlin, Ujerumani

Rais George Bush ameondoka Berlin kuelekea Roma, Italy, baada ya kufanya mazungumzo na Kansela Angela Merkel wa Ujerumani yaliotwama sana kuhusu programu ya Iran ya kuwa na nishati ya kinyukliya, jambo ambalo linabishwa na nchi za Magharibi.

George Bush ameihimiza Ujerumani ivunje maingiliano yake ya kibiashara na Iran na akaonya kwamba hajauondosha moja kwa moja uwezekano wa Marekani kutumia nguvu katika malumbano yake ya kuitaka Iran isitishe programu yake ya kinyukliya.

"Njia zote ziko mezani. Chaguo langu la kwanza ni kutafuta suluhisho la kidiplomasia. Na njia ilio bora kabisa ya kupata suluhisho la kidiplomasia ni kufanya kazi pamoja na washirika wetu, na hivyo ndivyo hasa tunavofanya. Risala kwa serekali ya Iran ni wazi. Ina njia ilio bora ya kwenda mbele kuliko ile njia ya kujitenga, nayo ni kukomesha mpango wake wa kinyukliya."

Rais George Bush alikutana na Bibi Merkel kama sehemu ya kile alichokitangaza kuwa ni ziara yake ya mwisho barani Ulaya kabla ya kuacha madaraka hapo Januari mwakani. Ziara hiyo aliianzia Slovenia juzi na pia itamfikia Vatikani, huko Roma, Ufaransa, Uengereza na Ireland ya Kaskazini.

Nchini Italy anatazamiwa kumshawishi mshirika wake wa siku nyingi, waziri mkuu Silvio Berlusconi, akubali nchi yake ibebe mzigo mkubwa zaidi katika vita vya Afghanistan, lakini mazungumzo yake yanatarajiwa pia yatagusia mzozo na Iran. Naye Silvio Berlusconi anatazamiwa kumuomba George Bush aunge mkono kikamilivu takwa la Italy kuingizwa katika mashauriano na Iran, licha ya madola matano ya kudumu yalio wanachama wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa pamoja na Ujerumani. Huko Roma George Bush atakutana na Pope Benedikt wa Kumi na Sita.

Katika mkutano na waandishi wa habari, akiwa pamoja na mwenyeji wake, kansela Angela Merkel wa Ujerumani, George Bush aliunga mkono mpango wa nchi za Ulaya kuizawadia Iran kiuchumi na kidiplomasia pindi viongozi wa Iran wataachana na mpango wa kurutubisha madini ya Uranium, jambo ambalo litakuwa hatua muhimu kwa nchi hiyo kuwa na silaha za kinyukliya. Alisema wataangalia Iran itaamua vipi, ikiwa ni siku moja baada ya nchi za Umoja wa Ulaya kuchukuwa hatua za kuziwekea vikwazo benki za Iran. Naye Bibi Merkel alisema:

"Naamini mbinyo wa kidiplomasia umeshaleta tija. Pale mtu anapoiangalia hali ya mambo ilivyo huko Iran, basi mtu anahisi juhudi hizi zinaweza kuleta mafanikio; lakini sharti ni kwamba tufanye kazi kwa pamoja, ndani ya Umoja wa Ulaya na pia ndani ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa."

Alisema ikiwa Iran haitatimiza masharti, basi vikwazo zaidi vitafuata.

Iran inazikataa shuku za nchi za Magharibi kwamba mpango wake wa kinyukliya unaficha azma ya kutaka kuwa na silaha za kinyukliya.

Ikumbukwe kwamba Rais Bush bado amapoteza imani ya watu wengi barani Ulaya kutokana na vita ambavyo ameiingiza nchi yake katika Iraq . Lakini, leo, kuhusu jambo hilo alisema hasikitiki hata kidogo kumuondosha Saadam Hussein kwani jambo hilo limeifanya dunia iwe mahala pa salama zaidi. Pia hapa Ulaya George Bush analaumiwa kukataa kutia saini mapatano ya kimataifa kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa duniani. Bush alisema kwamba kabla hajaondoka madarakani, nchi yake itatia saini mapatano juu ya mabadiliko ya hali ya hewa duniani.


 • Tarehe 11.06.2008
 • Mwandishi Othman, Miraji
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/EHyj
 • Tarehe 11.06.2008
 • Mwandishi Othman, Miraji
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/EHyj
Matangazo

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com