1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Brexit na watoto waliokwama pangoni Thailand

Oumilkheir Hamidou
9 Julai 2018

Uingereza baada ya Brexit, juhudi za kuwaokoa watoto walionasa pangoni nchini Thailand na mtihani uliosababishwa na waziri wa mambo ya ndani wa serikali kuu ya Ujerumani Horst Seehofer kuhusu wakimbizi magazetini

https://p.dw.com/p/314Ci
Großbritannien Theresa May bespricht Brexit Pläne mit dem Kabinett
Picha: Reuters/MOD/J. Rouse

Tunaanzia Uingereza ambako waziri mkuu Theresa May amefafanua mipango itakayofuatwa na serikali yake baada ya nchi hiyo ya kifalme kujitoa katika Umoja wa Ulaya  au Brexit. Mhariri wa gazeti la "Westfälische Nachrichten " anajiuliza kama nchi za Umoja wa Ulaya zitauridhia mpango huo. Gazeti linaendelea kuandika:

Hakuna bado anayeweza kuashiria kwa kiwango gani Umoja wa Ulaya utaridhia. Ni sawa kwamba kupitia kanda ya biashara huru utaepukwa angalao ule mvutano katika mpaka wa ndani wa Ireland. Na pia hakuna ushahidi kama Waziri Mkuu Theresa May, kwa kutangaza mpango huo mpya, hafanyi kile kile kinachokosolewa kila mara na Umoja wa Ulaya, yaani kujitapilia wao tuu. Kwa sababu biashara huru na wakati huo huo ukosefu wa haki sawa kwa waajiriwa au kufuata mwongozo wao wenyewe katika shughuli za huduma za jamii, yote hayo  hayataurahisishia mambo Umoja wa Ulaya."

Walimwengu wawaaombea watoto waliokwama

Macho ya walimwengu yanakodolewa dakika hii Thailand ambako wapiga mbizi wanaendelea kuwaokoa watoto waliokwama ndani ya pango la Tham-Luang, kaskazini mwa nchi hiyo. Gazeti la "Neue Westfälische" linaandika:"Hadi hivi karibuni si wasafiri wengi waliokuwa wakilijua pango hilo linalokutikana katika eneo la hifadhi ya mazingira karibu na mpaka wa Myanmar. Lakini tangu mwishoni mwa wiki iliyopita macho ya ulimwengu mzima yanakodolewa katika eneo hilo. Kwa sababu hakuna asiyejali kinachotokea tangu wiki mbili zilizopita katika eneo hilo la msituni. Kisa cha kuhuzunisha cha kukwama  gizani vijana 12 na kocha wao ndani ya pango hilo. Na kitisho cha kukotwa na maji yanayotishia kujaa. Na wazee wao wanaopiga kambi nje ya eneo hilo. Yote hayo yanatufanya na sisi pia tuingiwe na huzuni na kuwaombea salama.

Mzozo wa wakimbizi na madhara yake

Mada yetu ya mwisho magazetini inaturejesha hapa hapa Ujerumani na mtihani uliokuwa nusra usababishe serikali kuu ya muungano ivunjike. Gazeti la "Augsburger Allgemeine" linazungumzia uchunguzi wa maoni ya wananchi kuhusu kisa hicho na kuandika: "Wajerumani kwa wingi wao wamechoshwa au hata kukirihishwa na jinsi Seehofer, Dobrindt na Söder walivyokishambulia chama ndugu cha CDU. Viongozi wa CSU wanaonyesha walikuwa wakiamini kwamba kwa kufuata  mkondo huo wataweza kuwavutia wapiga kura wa chama cha AfD. Kama mbinu hizo zitaleta tija,  kuna wengi wanaoshuku. Na hakuna pia anayemwamini Seehofer anapodai hili ni suala la kina. Ameyataka mwenyewe .

 

Mwandishi: Hamidou Oumilkheir/Inlandspresse

Mhariri: Mohammed Khelef