1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaMarekani

Biden na Trump waendelea kujipigia debe

29 Februari 2024

Rais wa Marekani Joe Biden na mpinzani wake wa chama cha Republican Donald Trump watafanya ziara kwenye mpaka wa Marekani na Mexico wakati suala la uhamiaji likiendelea kuibua mjadala.

https://p.dw.com/p/4d2Ud
Kura ya mchujo South Carolina
Mtu akipiga kura katika jimbo la South Carolina.Picha: Allison Joyce/AFP/Getty Images

Rais Biden, ambaye amekuwa akijitetea juu ya suala la uhamiaji katika miezi ya hivi karibuni, atatumia ziara katika mji wa mpakani wa Brownsville, Texas, kujaribu kuwaaibisha wabunge wa Republican kwa kukataa juhudi za pande mbili za kuimarisha sera za uhamiaji baada ya Trump kuwaambia wasiipitishe na kumpa Biden ushindi wa sera.

Biden alichukua madaraka mnamo 2021 na kuahidi kubadilisha msimamo mkali wa sera za uhamiaji za Trump, lakini tangu wakati huo amekabiliwa na changamoto katika kuishughulikia kadhia hiyo.

Soma pia: Biden na Trump washinda chaguzi za awali Michigan

Huku akikabiliwa na shinikizo kutoka kwa Warepublican wanaomtuhumu kushindwa kudhibiti mpaka, mwaka jana Biden alitoa wito kwa bunge la Marekani kutoa ufadhili zaidi wa utekelezaji akisema kwamba "atafunga mpaka" iwapo atapewa mamlaka mapya ya kuwarudisha makwao wahamiaji.

Trump, ambaye alikuwa rais kuanzia 2017 hadi mapema 2021 alizingatia msimamo mkali mipakani kuwa suala sahihi kwake, na ataitumia fursa kumshutumu Biden kwa kushindwa kushughulikia masuala ya uhamiaji.

Trump atafanya ziara katika mji wa Eagle Pass, Texas, ambapo wahamiaji wamekuwa changamoto kubwa kwa mamlaka katika miezi ya hivi karibuni.

Je Trump ana kinga dhidi ya uhalifu?

USA Donal Trump Prozess in New York
Rais wa zamani wa Marekani Donald Trump mbele ya Mahakama ya Juu ya Jimbo la New York.Picha: Seth Wenig via REUTERS

Mahakama ya Juu ya Marekani imesema itaamua ikiwa Rais wa zamani Donald Trump ana haki ya kuwa na kinga dhidi ya mashtaka ya kuingilia uchaguzi ambayo anatajwa kupanga njama za kupindua matokeo ya uchaguzi wa 2020.

Agizo hilo kutoka kwa mahakama kuu, ambayo ina wabunge wengi wa kihafidhina 6 na waliberali 3, ni mara ya pili ndani ya mwezi mmoja kwa majaji hao kutathmini kesi yenye athari kubwa kwa rais huyo wa zamani.

Soma pia: Korti kusikiliza kesi ya Trump ya kinga ya kushtakiwa Aprili

Katika mzozo huu, Mahakama ya Juu itazingatia iwapo mashtaka ya Trump yanaweza kusonga mbele, au kama amekingwa dhidi ya dhima ya uhalifu.

Mahakama haijawahi kuamua kama rais wa zamani hawezi kushtakiwa kwa makosa ya jinai kwa madai ya vitendo visivyo halali vilivyofanywa wakati akiwa madarakani. Trump ndiye rais wa kwanza wa zamani kufunguliwa mashtaka, hata hivyo amekanusha mashtaka dhidi yake.

Trump akabiliwa na changamoto

USA Protesten von Trump-Anhänger in Denver
Mfuasi wa Rais wa Marekani Donald Trump.Picha: Bob Strong/REUTERS

Jaji katika jimbo la Illinois ameamuru kwamba Trump aondolewe kwenye kura ya mchujo ya jimbo hilo kutokana na jukumu lake katika ghasia za Januari 6 katika Bunge la Marekani.

Hatua sawa za kupiga kura dhidi ya Trump zimeongezeka katika majimbo kadhaa, ikiwa ni pamoja na uamuzi wa Colorado ambao sasa umefikishwa mbele ya Mahakama ya Juu.

Soma pia: Haley bado hajakata tamaa licha ya kushindwa na Trump katika jimbo la South Carolina

Colorado na zaidi ya majimbo kumi na mbili yatapiga kura ya kumchagua mgombea wa urais wa chama cha Republican mnamo Machi 5 na Mahakama ya Juu inatarajiwa kutoa uamuzi wake kabla ya wakati huo.