1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani: Kwanini umri wa rais Joe Biden ni mjadala?

Amina Mjahid
19 Februari 2024

Washauri wa rais wa Marekani Joe Biden mnamo mwaka 2020 walifanikiwa kumuelezea kiongozi hodari atakayeleta utulivu baada ya kipindi cha mivutano katika uongozi wa rais wa zamani Donald Trump.

https://p.dw.com/p/4cZcB
Marekani | Rais Joe Biden
Rais wa marekani Joe Biden akiwasili katika akisaidiwa kuingia katika chumba cha mkutano na Mfalme wa Jordan Abdullah IIPicha: Andrew Harnik/AP Photo/picture alliance

Washauri wa rais wa Marekani Joe Biden walijua mwaka 2020 kwamba umri wa rais huyo utakuja kuwa tatizo kwa wamarekani, lakini wakafanikiwa kumuelezea namna atavyoleta utulivu katika ikulu ya White House.

Kwa sasa Biden ana miaka 81, na kura za maoni zinaonesha kuwa umri wake sasa unawapa wasiwasi wapiga kura kuelekea uchaguzi wa mwezi Novemba.

Akiwa madarakani, amepunguza mno kasi yake ya uongozi, mwendo wake pia ni wa pole na kwa kawaida huwa anauma na kuchanganya maneno wakati wa hotuba zake na kufikia mbali ya hata kuchanganya majina ya baadhi ya viongozi wa dunia.

Lakini baadhi ya viongozi wamesema baada ya kukutana naye kwamba, ni mtu aliyetulia na makini katika mikutano ya faragha, lakini licha ya hilo bado suala la umri wa Biden linamtia doa hii ikiwa ni kulingana na kura za maoni.

Baraza maalum wiki iliyopita lilitoa ripoti yake, likikataa kumshitaki Biden kwa kuzihifadhi kwa maksudi nyaraka za siri lakini likamkosoa kwa kukosa kumbukumbu.

Soma pia:Biden asisitiza ana uwezo mzuri wa kukumbuka matukio

Wanachama wa Republican katika Baraza la wawakilishi walikuwa wa kwanza kumuelezea rais Biden kutoka chama cha Democratic kama mtu asiyefaa kuiongoza nchi.

Baadhi ya wachambuzi wa masuala ya kisiasa wamesema Ikulu ya White House haikushughulikia shutuma hizo mapema.

Samuel Woolley Mkurugenzi katika taasisi ya utafiti katika chuo kikuu cha Texas amesema kile kilichoonekana katika ikulu hiyo ya Marekani ni kujaribu kuendelea na mambo kama kawaida na kupuuzia mambo mabaya yanayoangaziwa.

Maoni: Biden ni mzee kuendelea kufanyakazi serikalini

Uchunguzi mpya wa Reuters na Ipsos unaonesha kwamba asilimia 78 ikiwemo asilimia 71 ya wademocrats wanafikiri kwamba Biden ni mzee mno kufanya kazi serikalini.

Washington, Marekani | Joe Biden na mkewe  Jill Biden
Rais wa Marekani Joe biden akiwa na mkewe Jill BidenPicha: Alex Brandon/AP Photo/picture alliance

Wakati Ikulu ya Marekani ikijikokota kujibu madai ya watu wanaomsema vibaya Biden kuhusiana na umri wake na kumbukumbu mbovu, mitandaoni kuna wimbi la picha zake na video watu wakitengeneza vidio za kuchekesha juu ya umri wa kiongozi huyo wa Marekani zikimuonesha kama mtu mzee asiyeweza tena kuongoza.

Kufanyia mzaka umri wake, hotuba zake na namna anavyotembea ndio limekuwa gumzo mitandaoni katika miaka yake hii mitatu ya uongozi.

Kituo cha habari cha Sky News cha Australia kina kipindi maalum katika mtandao wake wa Youtube ulio na wafuasi milioni nne, kinachoitwa "Biden vs. teleprompter," pamoja na video nyengine pia inayomuhusu Biden hasa akiuma maneno wakati wa hotuba zake mwaka 2022 imeonekana mara milioni 2.4.

Soma pia:Trump akimbilia Mahakama ya Juu kuzuwia asiondolewe kwenye kura

James Clyburn, Mwanachama wa Baraza la Congress anayetokea chama cha Democrat aliliambia shirika la habari la Reuters kwamba akaunti za wafuasi wa republican katikamitandao ya kijamii pamoja na washirika wa Trump zinazomdhihaki mno rais Biden zinawafanya kushindwa kuelezea mafanikio yake.

Hata hivyo Ikulu pamoja na timu ya kampeni ya Biden kuelekea uchaguzi mkuu wa Novemba imesema itaanza kushughulikia wasiwasi juu ya umri wa Biden mwaka huu kwa kuangazia zaidi mafanikioyake ikiwemo ukuaji wa ajira na mipango mikubwa ya miundombinu.

Huku hayo yakiarifiwa wachambuzi wengine wa masuala ya kisiasa wamesema Biden anaonewa kwa kulengwa na kumulikwa na vyombovya habari juu ya umri wake wakati mpinzani wake rais wa zamani Donald Trump akiwa na miaka 77 pia akiwa ameshawahi kusema maneno asiyoyafahamu au kuuma maneno wakati wa hotuba zake alipokuwa rais wa taifa hilo kubwa na lililo na nguvu duniani.

Biden awasamehe waliopatwa na hatia ya kuvuta bangi