Biashara ya silaha - Ujerumani | Matukio ya Kisiasa | DW | 24.10.2007
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Biashara ya silaha - Ujerumani

Inatathminiwa kuwa kiasi ya watu 80,000 hufanya kazi katika viwanda vya silaha nchini Ujerumani-hiyo ni idadi ndogo mno ikilinganishwa na ile ya wakati wa Vita Baridi.

Viwanda hivyo hasa hutengeneza silaha kwa ajili ya jeshi la Ujerumani-Bundeswehr lakini sasa hujitahidi pia kuingia katika masoko ya nje.Nyambizi na vifaru vinavyotengenezwa Ujerumani vina teknolojia ya hali ya juu kabisa, lakini soko ni dogo na kuna ushindani mkubwa. Katika orodha ya makampuni makubwa ya silaha duniani,hakuna hata kampuni moja la Kijerumani. Juu ya hivyo,Ujerumani ni miongoni mwa wauzaji wakuu wa silaha duniani.

Makampuni hayo kwa sababu ya silaha zake za hali ya juu na bei kubwa,yamefanikiwa kujiingiza katika masoko yenye ushindani na tangu miaka michache iliyopita yanaendelea kujiimarisha.

Kwa maoni ya mwaandishi wa habari Thomas Meuter ambae ni mtaalamu wa fani hiyo,sababu ni teknolojia ya hali ya juu ya viwanda vya silaha vya Ujerumani.Anasema hivi:

„Kwa hakika zana zetu zinashindana katika ligi ya mabingwa.Miongoni mwa zana hizo ni magari ya deraya na ya vitani pamoja na teknolojia ya kuhifadhi magari hayo na kuwalinda wanajeshi.“

Hasa,vifaru aina ya Leopard 2 (Chui namba 2) hununuliwa na majeshi ya nchi za ngámbo kwa sababu,vifaru hivyo huwalinda wanajeshi bora zaidi,dhidi ya risasi na mabomu yanayofukiwa chini ya ardhi.Mbali na majeshi ya nchi 16 za Ulaya,hata Kanada iliyopoteza wanajeshi wengi nchini Afghanistan sasa ni mteja mpya.

Sehemu kubwa ya silaha zinazouzwa ngambo na viwanda vya Kijerumani,huenda kwa washirika wake wa NATO na nchi za Ulaya.Kwa mujibu wa katiba, kila biashara ya silaha yapaswa kuidhinishwa na serikali.Kawaida,biashara inayofanywa pamoja na nchi za NATO na Umoja wa Ulaya huidhinishwa na serikali ya Ujerumani bila ya matatizo.

Nchi zingine zinapohusika,serikali huchunguza ikiwa biashara hiyo inaambatana na mwongozo wa usafirishaji wa silaha.Mwongozo huo ulifanyiwa marekebisho wakati wa utawala wa serikali ya mseto ya chama cha SPD na cha Kijani.Mbunge wa SPD Uta Zapf,mwanachama wa miaka mingi katika baraza la wabunge linalohusika na masuala ya ulinzi amesema,uamuzi unapopitishwa,maeneo ya mivutano na kuheshimiwa kwa haki za binadamu ni mambo yanayozingatiwa.

Hayo ni muhimu,lakini wakati mwingine kwa sababu ya maslahi ya usalama ya Ujerumani,nchi kama vile Pakistan huuziwa nyambizi za Kijerumani licha ya kuwepo mivutano na matatizo ya haki za binadamu nchini humo.

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com