1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

BERLIN: Kurnaz asema aliteswa na wanajeshi wa Ujerumani

5 Oktoba 2006
https://p.dw.com/p/CD6A

Mjerumani mwenye asili ya kituriki, Murat Kurnaz, aliyeachiliwa huru na Marekani kutoka jela ya Guantanamo Bay bila kufunguliwa mashtaka, amedai wanajeshi wawili wa Ujerumani walimtesa katika jela moja ya Marekani huko Kandahar Afghanistan, muda mfupi baada ya kukamatwa kwake mnamo mwaka wa 2001 nchini Pakistan.

Wizara ya ulinzi ya Ujerumani imeanzisha uchunguzi, ikisema haina ushahidi wowote kuhusiana na kisa kama hicho.

Katika mahojiano yake ya kwanza tangu arejee nyumbani mjini Bremen, Kurnaz aliliambia jarida la Stern kwamba wanajeshi wawili waliokuwa na bendera ya Ujerumani kwenye sare zao walikigongesha kichwa chake sakafuni. Aidha alisema wanajeshi wa Marekani walitumia umeme na kumfunga mikono yake juu kwa muda mrefu.

Tangu kuwasili jela ya Guantanamo mwaka wa 2002, Kurnaz anasema alishuhudia kituo cha kuzuia wafungwa kisicho na sheria. Alisema walinzi huwapiga wafungwa na kuwatenga.