Afrika katika magazeti ya Ujerumani | Magazetini | DW | 01.05.2015
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Magazetini

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

Magazeti ya Ujerumani wiki hii yameandika juu ya mgogoro wa kisiasa nchini Burundi uliosababishwa na uamuzi wa Rais Nkurunziza wa kuwania muhula wa tatu.Pia yameandika juu ya kupambana na maradhi ya Malaria

Maandamano ya kumpinga Rais Pierre Nkurunziza anaewania muhula wa tatu nchini Burundi

Maandamano ya kumpinga Rais Pierre Nkurunziza anaewania muhula wa tatu nchini Burundi

Gazeti la "die tageszeitung" limandika juu ya mgogoro wa kisiasa nchini Burundi. Mgogoro huo umesababishwa na uamuzi wa chama tawala nchini humo CNDD-FDD wa kumteua Rais Pierre Nkurunziza kugombea muhula wa tatu wa urais kinyume na katiba. Gazeti hilo linasema Rais Nkurunziza anazichochea cheche za vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Gazeti la "die tageszeitung" linaeleza kwamba ghasia zinazotokea nchini Burundi kutokana na watu kuupinga uamuzi wa Rais Nkurunziza kuwania muhula wa tatu zinazitia wasiwasi nchi jirani.

Wanajeshi wa Rwanda wawekwa kwenye mpaka na Burundi

Ripota wa gazeti la "die tageszeitung" amearifu kwamba amewaona kwa macho yake wanajeshi wa Rwanda wakipelekwa kwenye mpaka na Burundi. Mpaka sasa Rwanda imekuwa inayaweka majeshi yake kwenye mpaka wake na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Gazeti la "Franfurter Allgemeine" wiki hii limeandika juu ya tatizo la wakimbizi na linauliza jee fedha za msaada wa maendeleo zinazotolewa na Ujerumani kwa nchi za Afrika zitasaidia katika juhudi za kulitatua tatizo la ukimbizi ?

Gazeti hilo linaarifu kwamba serikali ya Ujerumani imo katika hatari ya kutoa ahadi kubwa kuliko inavyoweza kuzitekeleza. Gazeti hilo limemnukulu Kansela wa Ujerumani wa Ujerumani Angela Merkel akisema kwamba serikali yake itaimarisha juhudi ili kuung'oa mzizi wa tatizo la ukimbizi.


Gazeti la "Frankfurter Allgemeine" limeripoti kwamba Kansela Merkel aliyasema hayo siku moja tu baada ya kutokea maafa ya wakimbizi kwenye bahari ya Mediterania. Gazeti hilo pia limemnukulu Waziri wa maendeleo wa Ujerumani Gerd Müller akiutaka Umoja wa Ulaya utenge haraka kiasi cha Euro Milioni 10 za msaada.

Hata hivyo gazeti la "Frankfurter Allgemeine" linatilia maanani kwamba msaada wa maendeleo unaotolewa na Ujerumani kwa nchi za Afrika umekosolewa na taasisi moja ya Marekani.


Kwa mujibu wa chuo cha Marekani kinachofuatilia maendeleo ya uchumi wa duniani,Global economy and Development cha Brookings, Ujerumani inatoa misaada kwa nchi nyingi kwa pamoja na pia inafadhili miradi chungunzima. Kwa mujibu wa taasisi hiyo sera ya misaada ya Ujerumani haileti tija barani Afrika.

Lakini gazeti la "Frankfurter Allgemeine" limesema serikali ya Ujerumani imeyakanusha madai hayo.

Chanjo dhidi ya Malaria yakaribia kupatikana

Gazeti la "Neues Deutschland" limeandika katika makala yake kwamba maradhi ya malaria yanaendelea kuua duniani.

Gazeti hilo linaeleza kwamba kila mwaka watoto 1,200,000 wanakufa kutokana na maradhi ya Malaria duniani, na hali ni mbaya zaidi nchini Malawi. Sababu ni kwamba hakuna taratibu za kinga na utafiti wa kutafuta chanjo dhidi ya ugonjwa huo unachelewa.

Gazeti la "Neues Deutschland" limearifu kwamba watu zaidi ya 4,000,000 wanaugua maradhi ya Malaria kila mwaka nchini Malawi na hasa watoto na akina mama wajawazito. Gazeti hilo linasema ugonjwa wa Malaria ndiyo unaoongoza kwa kuua nchini Malawi.

Lakini gazeti la "Berliner Zeitung" limechapisha habari za kufurahisha .

Gazeti hilo linasema chanjo ya ugonjwa wa Malaria inakarabia sana kupatikana. Gazeti hilo limemnukulu mtaalamu wa Ujerumani wa magonjwa ya nchi za joto Peter Kremsner akiripoti kwamba chanjo hiyo imefanya kazi wakati wa majaribio.

Mtaalamu huyo amenukuliwa na gazeti la "Berliner " akisema kwamba waliwapa chanjo watoto 1800 katika kipindi cha mwaka mmoja na hakuna alieambukizwa maradhi ya Malaria katika muda huo. Kwa mujibu wa gazeti la "Berliner "mtaalamu huyo anao uhakika kwamba chanjo waliyoijaribu, "RTSS " imethibiti kuwa na uwezo wa kuwakinga binadamu na maradhi ya Malaria.

Hata hivyo wataalamu bado hawajaweza kubainisha jinsi dawa hiyo inavyofanya kazi.

Mwandishi:Mtullya Abdu.Deutsche Zeitungen.

Mhariri. Yusuf Saumu