Afrika katika magazeti ya Ujerumani juma hili | Magazetini | DW | 27.02.2009
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Magazetini

Afrika katika magazeti ya Ujerumani juma hili

Polisi nchini Kenya washutumiwa kwa mauaji ya kinyama ya raia

Rais wa Kenya Mwai Kibaki alaumiwa kwa kuukandamiza uhuru wa vyombo vya habari

Rais wa Kenya Mwai Kibaki alaumiwa kwa kuukandamiza uhuru wa vyombo vya habari

Gazeti la Frankfurter Allgemeine liliripoti habari kuhusu wanajeshi wa Ujerumani kushiriki kwenye operesheni ya jumuiya ya kujihami ya kambi ya magharibi, NATO, dhidi ya maharamia katika pwani ya Somalia. Waziri wa ulinzi wa Ujerumani, Franz Josef Jung, amenukuliwa na gazeti hilo akisema Ujerumani itatuma manowari yake iitwayo Emden pamoja na meli itakayobeba mizigo na mahitaji.

Waziri huyo amedokeza kuwa wanajeshi hao watashiriki kwenye operesheni hiyo kwa muda mfupi kuanzia katikati ya mwezi Machi hadi mwishoni mwa mwezi Julai mwaka huu. Ujerumani tayari ina manowari yake iitwayo Rheniland-Pflaz kwenye pwani ya Somalia katika operesheni nyengine ya kuwadhibiti maharamia inayoongozwa na Umoja wa Ulaya, iiitwayo ´Atalanta´.

Mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa aliyechunguza mauaji nchini Kenya ameilaumu polisi ya nchi hiyo kwa kuua, kutumia mfumo maalum. Hayo yameripotiwa na gazeti la Berliner Zeitung. Mhariri wa gazeti hilo amesema profesa Philip Alston kwenye ripoti yake aliyoiwasilisha Jumatano Februari 25 amefichua kuwa zaidi ya mauaji 500 yalifanywa kati ya mwezi Juni na Oktoba mwaka 2007. Maiti nyingi ziligunduliwa kwenye vichaka, chini ya madaraja au misituni katika mji mkuu wa Nairobi.

Bwana Alston alinukuliwa na gazeti la Berliner Zetung akisema wauaji hawakupatikana wala kusakwa. Mauaji yalifanywa kinyama, wauaji hawajulikani mpaka leo, polisi waliua kama walivyotaka na viongozi wa ngazi ya juu katika jeshi la polisi na wanasiasa walihusika katika mauaji hayo. Alston ametaka kamanda wa polisi na muongoza mashtaka mkuu wa serikali walijiuzulu mara moja.

Gazeti la Tagesspiegel liliripoti habari za rais wa Kenya, Mwai Kibaki, kuukandamiza uhuru wa vyombo vya habari. Gazeti hilo limesema kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 75 mwanzoni mwa mwaka huu alisaini sheria ya vyombo vya habari iliyopingwa vikali na waandishi wa habari na jumuiya za kiraia nchini Kenya.

Rais Kibaki anakabiliwa na shinikizo kutoka kwa chama shirika kwenye serikali yake cha Orange for Democratic Change, ODM, pamoja na vyama tanzu vinavyounda muungano wa chama chake cha PNU. Amempa jukumu waziri wa habari, Samuel Poghisio, kudurusu upya sheria hiyo na kupendekeza mageuzi.

Mhariri wa gazeti la Tagesspiegel amesema waandishi wa habari nchini Kenya wanakabiliwa na hatari mpya. Maiti ya mwandishi habari wa kujitegemea ilipatikana imetupwa msituni mwishoni mwa mwezi Januari baada ya kuripoti visa vya ufisadi katika jeshi la polisi. Aliwaambia marafiki zake kuhusu vitisho alivyopokea kutoka kwa polisi kabla kupotea.

Habari nyingine zilizoripotiwa katika magazeti ya Ujerumani wiki hii ni mazungumzo ya amani kati ya serikali ya Sudan na waasi wa jimbo la Darfur. Gazeti la Neues Deutschland lilikuwa na kichwa cha habari kilichosema ´Maadui kwenye meza ya Mazungumzo´.

Mazungumzo kati ya pande hizo mbili yalifanyika mjini Doha, Qatar, ambapo viongozi wa serikali ya Sudan na waasi wa kundi la Haki na Usawa, JEM, walisaini makubaliano ya nia njema yanayozitaka pande hizo mbili kubadilishana wafungwa wa kivita na kuendeleza mazungumzo ya kusaka amani.

Msemaji wa kundi la waasi wa JEM, Ahmed Hussein Adam, amenukuliwa na gazeti la Neues Deutschland akisema mkataba huo ni hatua ya kwanza inayoweka msingi utakaotumiwa kuanza mchakato wa kutafuta amani.

Kamba wa baharini na ugonjwa wa kipindundu. Rais wa Zimbabwe Robert Mugabe aruhusu kamba waletwe ikulu, huku hospitali zikiwa hazina sindano na dawa. Hivyo, ndivyo lilivyoripoti gazeti la Süddeutsche Zeitung. Rais Mugabe alitimiza miaka 85 Jumamosi Februari 21 na kama kawaida yake kila mwaka yeye hufanya sherehe ya gharama kubwa bila kujali.

Chupa 2,000 za pombe ya shampeni, kamba 8,000 na chupa 500 za pombe ya wisky viliagizwa kwa ajili ya sherehe ya siku ya kuzaliwa kwake. Pamoja na vitu hivyo kulikuwa na ng´ombe 76 ambao wakulima maskini wa Zimbabwe walilazimika kuchangia kwenye sherehe hiyo.

Mhariri wa gazeti la Süddeutsche Zeitung anasema kiroja cha mambo ni kwamba Zimbabwe wakati huo huo inakabiliwa na tatizo kubwa la kibanadamu kutokana na ugonjwa wa kipindupindu na maisha magumu yaliyosababishwa na kuporomoka kwa sarafu ya nchi hiyo.

Mgogoro wa kiuchumi unaoikabili dunia unaziathiri nchi za Afrika. Gazeti la Neue Zürcher limeripoti kuwa uchumi wa Afrika Kusini ulinywea kipindi cha nne cha biashara cha mwaka jana hii ikiwa ni mara ya kwanza katika muongo mmoja. Kupungua kwa bidhaa zinazouzwa nje ya nchi hiyo kumesababisha kupungua kwa uzalishaji wa viwandani nchini humo.

 • Tarehe 27.02.2009
 • Mwandishi Charo, Josephat/ http://dwkadb10.dwelle.de/BASIS
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/H2Oo
 • Tarehe 27.02.2009
 • Mwandishi Charo, Josephat/ http://dwkadb10.dwelle.de/BASIS
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/H2Oo