Afrika katika magazeti ya Ujerumani juma hili | Magazetini | DW | 30.11.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Magazetini

Afrika katika magazeti ya Ujerumani juma hili

Mkutano kati ya Umoja wa Ulaya na Afrika kufanyika bila waziri mkuu wa Uingereza, Gordon Brown na mapigano mapya yazuka mashariki mwa Chad.

default

Waziri mkuu wa Uingereza Gordon Brown

Kuhusu mkutano kati ya Umoja wa Ulaya na Afrika utakaofanyika mjini Lisbon nchini Ureno tarehe 9 mwezi huu, gazeti la Süddeutsche limesema uamuzi wa waziri mkuu wa Uingereza Gordon Brown kutoshiriki kwenye mkutano huo ulitarajiwa katika makao makuu ya Umoja wa Ulaya mjini Brussels, Ubelgiji.

Katika majuma yaliyopita Brown amekuwa akisema hatakaa meza moja na rais Robert Mugabe wa Zimbabwe. Baada ya rais Mugabe kutangaza atahudhuria mkutano huo wa Lisbon, waziri mkuu Gordon Brown aliamua kutohudhria mkutano huo. Hata hivyo, Uingereza ina uwezo wa kuukwamisha mkutano huo kutumia kura yake ya turufu.

Gazeti la Neues Deutschland lilisema wakati rais Mugabe atakapokuwa mkutanoni nchini Ureno, mazungumzo kati ya upinzani na serikali ya Zimbabwe yatakuwa yakiendelea mjini Harare ili kujaribu kuutanzua mgogoro unaondelea nchini humo.

Rais wa Afrika Kusini, Thabo Mbeki, amenukuliwa na gazeti hilo akisema inawezekana kuumaliza mzozo wa kisiasa nchini Zimbabwe.

Mada ya pili inahusu mapigano mapya yaliyozuka mashariki mwa Chad. Gazeti la Neue Zürcher lilisema mwezi mmoja baada ya kusainiwa mkataba wa kusitisha mapigano, waasi na wanajeshi wa serikali walikabiliana kwenye mapigano makali.

Machafuko hayo yalizuka karibu na kambi ya wamkimbizi ya Farchana, takriban kilomita 100 mashariki mwa mji mku wa pili wa Chad, Abeche, karibu pia na mpaka wa Sudan. Pande zote mbili zimedai ushindi.

Waasi wengi waliuwawa na wanajeshi 60 wa Chad waliojeruhiwa wakahamishwa kutoka mjini Abeche. Helikopta za Chad na Ufaransa ziliwakimbiza waasi hao wa muungano wa vikosi vinavyopigania demokrasia na maedneleo, UFDD.

Nalo gazeti la Frankfurter Allgemeine lilisema mapigano kati ya wanajeshi wa Chad na waasi wa kundi la UFDD yaliyozuka Jumatatu iliyopita, ni ya pili kutokea.

Mapigano hayo ya kwanza tangu mwezi Aprili mwaka huu, yalitokea katika eneo ambako wanajeshi 3,700 wa Umoja wa Ulaya watapelekwa kuwalinda wakimbizi dhidi ya mashambulizi ya waasi.

Waziri wa mashauri ya kigeni wa Ufaransa, Bernard Kouchner, alinukuliwa na gazeti hilo akisema mapigano hayo yanaonyesha umuhimu wa kutuma kikosi cha Umoja wa Ulaya mashariki mwa Chad haraka iwezekanavyo.

Gazeti la Frankfurter Allgemeine pia liliripoti kuhusu kuongezeka kwa wasiwasi wa kuzuka mapigano kati ya Ethiopia na Eritrea. Gazeti hilo lilisema muda uliopewa mahakama ya mjini The Hague Uholanzi kusuluhisha mgogoro wa mpaka kati ya nchi hizo mbili ulimalizika Jumanne iliyopita.

Ethiopia na Eritrea zilipigana vita vikali kati ya mwaka wa 1998 na 2000 kuhusu mpaka, ambapo Eritrea iliingia ardhi ya Ethiopia na kuuteka mji wa mpakani wa Badme, ambao inasema ni mali yake.

Watu 80,000 waliuwawa wakati wa vita hivyo kabla mkataba wa amani kusainiwa mnamo mwaka wa 2000 mjini Algiers nchini Algeria.

Nchi hizo mbili zimekuwa zikisubiri uamuzi wa mahakama ya mjini The Hague lakini Ethiopia imekuwa ikiteta kuhusu mji wa Badme. Eritrea na Ethiopia zimetuma wanajeshi katika eneo la mpakani.

Na hatimaye gazeti la General Anzeiger liliripoti ziara ya Watanzania wanne waliolitembelea kanisa la kiinjili la jimbo la Bonn. Mhariri wa gazeti hilo alisema wajerumani wanaweza kujifunza mengi kutoka kwa Watanzania.

Mchungaji Jackson Mbelwa Ruguma aliyeuongoza ujumbe huo alinukuliwa na gazeti hilo akiisifu idadi kubwa ya wazee wanaohudhuria ibada za Jumapili, lakini akashangazwa na idadi ndogo mno ya vijana wa kijerumani wanaokwenda kanisani.

Bi Cornelia Kokuhabwa Kitambi, muuguzi katika hospitali ya Bukoba alisema urafiki kati ya usharika wa Kusini A na mji wa Bonn ni mzuri. Alifurahi kwamba kanisa la Bonn pia lina wachungaji wa kike.

Kwa kuwa ushirikiano kati ya usharika wa Kusini A na kanisa la jimbo la Bonn umefanikiwa, mwaka ujao kwaya ya vijana kutoka Kusini A imealekwa Ujerumani kama mfano wa utandawazi wa kuigwa.

 • Tarehe 30.11.2007
 • Mwandishi Josephat Charo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CV3f
 • Tarehe 30.11.2007
 • Mwandishi Josephat Charo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CV3f
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com