Afrika katika magazeti ya Ujerumani juma hili | Makala | DW | 13.04.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Makala

Afrika katika magazeti ya Ujerumani juma hili

Maelfu ya wakimbizi kutoka Somalia wapiga kambi katika mpaka wa Kenya. Sudan yalaumu jeshi la Chad kwa mauaji ya wanajeshi wake. Umoja wa Mataifa na Umoja wa Ulaya waongeza mbinyo dhidi ya serikali ya Khartoum kuhusu mzozo wa Darfur. Na shirika la mazingira la Greenpeace laonya juu ya ukataji wa misitu nchini jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo.

Tunaanza na habari za kupiga kambi maelfu ya wakimbizi wa kisomali katika mpaka wa Kenya. Gazeti la Tageszeitung lilisema wakimbizi hao wamekusanyika katika kijiji cha mwisho nchini Somalia karibu na mpaka na Kenya cha Doble baada ya kuyatoroka mapigano mjini Mogadishu. Mpaka wa Kenya umefungwa huku serikali mjini Nairobi ikisema inataka kuzuia wanamgambo wa kiislamu kuingia nchini humo.

Mhariri wa gazeti la Tageszetung alimnukulu Bi Catherine Weibel wa shirika la wakimbizi la Umoja wa Mataifa, UNHCR, akisema wakimbizi hao hawana mahitaji muhimu kama vile chakula, matibabu na maji ya kunywa. Shirika la UNHCR pamoja na mashirika mengine ya misaada hayawezi kuwasaidia kwa sababu hayaruhusiwi kuwafikia.

Gazeti la Frankfurter Rundschau liliueleza mji mkuu wa Somalia, Mogadishu, kuwa katika hali mbaya ya usalama ikilinganishwa na hapo zamani. Tisho la wanamgambo wa kisomali kufanya uasi nchini humo halikuwa maneno matupu huku serikali ya mpito ya Somalia ikishindwa kuudhibiti mji huo. Naibu waziri mkuu wa Somalia, Hussein Aidid, ameeleza wasiwasi wake wa Somalia kugeuka kuwa Irak ya pili.

Likitupeleka nchini Sudan gazeti la Neue Zürcher lilisema serikali ya Sudan imewalaumu wanajeshi la Chad kwa kuwaua wanajeshi 17 wa Sudan wakati walipokuwa wakiwafukuza waasi waliovuka mpaka na kuingia Sudan Jumatatu iliyopita. Serikali ya Chad mjini Ndjamena imekiri kuwa wanajeshi wake waliwafuata waasi wa Chad hadi mpaka wa Sudan. Serikali ya Sudan inaishinikiza Chad itoe maelezo ya kina kuhusu mauaji hayo ya mpakani.

Gazeti la Frankfurter Allgemeine lilikuwa na habari kuhusu hatua ya Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afika kuongeza mbinyo wake kuitaka serikali ya Sudan ifanye haraka kushirikiana katika kuutanzua mzozo wa Darfur kwa amani. Rais wa Afrika Kusini, Thabo Mbeki, alikuwa mjini Khartoum mnamo Jumanne iliyopita kuishinikiza Sudan itekeleze ahadi yake iliyoitoa mnamo mwezi Novemba mwaka jana.

Mwishoni mwa juma hili naibu waziri wa mashauri ya kigeni wa Marekani, John Negroponte, anatarajiwa kuwasili mjini Khartoum. Wajumbe wa Umoja wa Mataifa, Umoja wa Afrika na Sudan walikubaliana usiku wa Jumatatu iliyopita juu ya kukiongeza kikosi cha Umoja wa Mataifa kufikia wanajeshi 2,500.

Ukataji wa misitu nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo huenda ukawa tisho kubwa kwa mabadiliko ya hali ya hewa. Hayo yaliripotiwa na gazeti la Tageszeitung. Mhariri wa gazeti hilo alisema kwa mujibu wa uchunguzi uliofanywa na shirika la kuyalinda mazingira la Greenpeace, makampuni ya kutengeza mbao yasiyo na uadilifu yanaivamia misitu barani Afrika, lakini hakuna anayejali kulinda.

Uharibifu wa misitu katika bonde la mto Kongo linaifanya mojawapo ya nchi masikini duniani kuwa mharibifu mkubwa wa hali ya hewa. Kwa mujbiu wa ripoti ya shirika la Greenpeace, jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo huenda ikachangia kiwango cha tani 34 za gesi ya carbon dioxide angani kufikia mwaka wa 2050 kama Uingereza miaka 60 iliyopita.

Shirika la Greenpeace linasema hatua hiyo ni ya kutia wasiwasi ikiwa Kongo itapoteza misitu yake kama mwenendo unavyoonyesha kwa wakati huu. Ripoti iliyoitwa ´Carving Up the Congo´, jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo inashikilia nafasi ya 21 mbele ya Ubelgiji, Uswissi, Uhispania na Uholanzi, kwenye orodha ya kimataifa ya nchi zinazoharibu misitu na kuachilia gesi ya carbon dioxide kuingia angani.

Jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo ina kilomita za kujaza milioni 1,28 za misitu katika nusu ya ardhi yake. Laki sita kati yao bado hazijaguswa. Kwa sababu ya machafuko na vita Kongo inabakia kuwa eneo ambalo misitu inaharibiwa kama vile nchini Brazil na Indonesia. Mito mingi haikuwa salama na bandari pekee ya kusafirishia bidhaa katika nchi za kigeni ya Matadi ni ndogo.

Lakini tangu kuchaguliwa kwa serikali na kuingia kwa wawekezaji wa kigeni, kunaweza kubadili mkondo wa mambo haraka. Mto Kongo ambao ndio njia ya pekee ya usafiri kupitia nchini humo, utapanuliwa na kusafishwa haraka ili kuziwezesha meli kupita. Hatua hiyo itawanufaisha wananchi wa mataifa jirani lakini itahatarisha misitu iliyo karibu na mto huo.

 • Tarehe 13.04.2007
 • Mwandishi Josephat Charo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CHTF
 • Tarehe 13.04.2007
 • Mwandishi Josephat Charo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CHTF