Afrika katika magazeti ya Ujerumani juma hili | Magazetini | DW | 20.07.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Magazetini

Afrika katika magazeti ya Ujerumani juma hili

Baraza la mahakama nchini Libya labatilisha hukumu dhidi ya wauguzi watano wa Bulgaria na daktari mmoja mpalestina na mkutano wa kutafuta amani nchini Somalia wafanyika mjini Mogadishu.

Baraza la mahakama nchini Libya lilibatilisha hukumu ya kifo dhidi ya wataalaamu wa afya walioshtakiwa kwa kuwaambukiza virusi vya ukimwi watoto zaidi ya 400 katika hosptali ya mjini Bengazi nchini Libya. Gazeti la Tageszeitung lilisema hofu ya kunyongwa wataalamu hao sasa haipo tena kufuatia uamuzi huo wa baraza la mahakama.

Wauguzi watano raia wa Bulgaria na daktari mmoja raia wa Palestina wamekuwa wakizuiliwa gerezeni mjini Tripoli tangu mwezi Februari mwaka wa 1999. Mnamo mwezi Mei mwaka wa 2004 walihukumiwa kifo na mwezi Disemba mwaka wa 2006 mahakama ikaidhinisha hukumu hiyo licha ya wataalamu wa kimatiafa kubaini kuwa watoto wote walikuwa tayari wameambukizwa virusi vya ukimwi kabla wauguzi wa Bulgaria na daktari mplaestina kuwasili katika hospitali ya Bengazi.

Waziri mkuu wa Bulgaria, Sergei Stanischev, amenukuliwa na gazeti la Tagesszeitung akisema kesi dhidi ya raia wake itamalizika wakati watakaporudi nchini humo. Umoja wa Ulaya umeashiria kutaka kuishinikiza Libya iwaachie wataalamu warejee nchini mwao.

Mada ya pili inahusu mkutano wa kutafuta amani nchini Somalia. Mhariri wa gazeti la General Anzeiger alisema mkutano huo haukutarajiwa kufikia mafanikio makubwa. Mamia ya viongozi wa kimbari, wanasiasa na wababe wa kivita walikusanyika mjini Mogadishu Jumapili iliyopita kwa mkutano wa upatanisho uliolenga kusaka amani ya Somalia.

Kuanza kwa mkutano huo kuliahirishwa sio kwa sababu ya shambulio la bomu ila kushindwa kuwasili waziri mkuu wa Somalia aliyetakiwa kusafiri kwa njia ya ndege kutoka mjini Nairobi Kenya na spika wa bunge ambaye naye alitakiwa kusafiri kutoka Baidoa. Juhudi za kuleta amani nchini Somalia zinafanyika kwa mara ya 18. Nchi zinazoidhamini serikali ya rais Abdulahi Yusuf, zinataka mambo yaende haraka na zimeendelea kutoridhishwa na hali ilivyo nchini Somalia.

Umoja wa Ulaya, Uingereza, Norway na Marekani zimetuma dola milioni nane kwa ajili ya mkutano wa mjini Mogadishu unaotarajiwa kuendela kwa majuma kadhaa lengo likiwa kufikia msamaha na makubaliano miongoni mwa mbari mbalimbali nchini Somalia. Hili litakuwa na ugumu wake kwani mbari hizo zimekuwa zikipigana na makundi mbalimbali kutaka madaraka nchini Somalia.

Kansela wa Ujerumani Bi Angela Merkel amekataa wanajeshi wa Ujerumani wapelekwe kwenda nchini Chad. Gazeti la Frankfurter Allgemeine lilisema Ujerumani haitashiriki katika mpango uliopendekezwa na serikali ya Ufaransa kutaka vikosi vya Ulaya vipelekwe Chad kuwasaidia wakimbizi wa Sudan.

Kansela Merkel alinukuliwa na gazeti hilo akisema ikizingatiwa vikosi vya jeshi la Ujerumani vinavyofanya kazi nje ya nchi, haina haja kutuma wanajeshi kwenda Chad. Hata hivyo kansela Merkel alifafanua wazi kwamba wazo la Ufaransa kutaka wanajeshi au polisi 1,500 wapelekwe katika kambi za wakimbizi wa Sudan nchini Chad, ni la kufikiriwa. Alisema serikali yake haitalipinga pendekezo hilo katika Umoja wa Ulaya wala katika ngazi ya kimataifa lakini haitashiriki.

Tukimalizia na hukumu dhidi ya viongozi wa upinzani nchini Ethiopia gazeti la Frankfurter Allgemeine lilisema mahakama moja mjini Addis Ababa iliwahukumu viongozi 30 wa upinzani kifungo cha maisha gerezani mnamo Jumatatu iliyopita. Waongozaji mashtaka nchini Ethiopia walitaka wanasiasa hao wahukumiwe kifo.

Kwa mujibu wa mahakama viongozi hao wa upinzani walipatikana na makosa ya kuchochea machafuko na uvunjaji wa sheria. Walikamatwa mnamo mwaka wa 2005 wakati walipokuwa wakiandama kupinga kuchaguliwa tena waziri mkuu Meles Zenawi. Wengi wao ni wanachama wa muungano wa Umoja na Demokrasia, CUD. Washukiwa wote walikataa kuutambua uamuzi wa mahakama wakisema imetumiwa kama chombo cha kisiasa kuwanyanyasa.

Viongozi wote wa upinzani waliachiliwa huru Ijumaa iliyopita, baada ya rais wa Ethiopia kuwasamehe.

 • Tarehe 20.07.2007
 • Mwandishi Josephat Charo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CHSM
 • Tarehe 20.07.2007
 • Mwandishi Josephat Charo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CHSM