Afrika katika magazeti ya Ujerumani juma hili | Magazetini | DW | 10.08.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Magazetini

Afrika katika magazeti ya Ujerumani juma hili

Waasi wa Darfur wakubali kufanya mazungumzo na serikali ya Sudan. Hali ya kisiasa yapamba moto nchini Kenya huku uchaguzi mkuu ukikaribia. Hali ya wasiwasi yatanda nchini Sierra Leone. Na naibu waziri wa afya wa Afrika Kusini atimuliwa.

Tunaanza na makubaliano ya waasi wa jimbo la Darfur kutaka kufanya mazungumzo na serikali ya Sudan. Gazeti la Tagesspiegel lilisema waasi hao sasa wamechoshwa na vita lakini sio maswala yote ambayo yamewekwa bayana. Kwenye mkutano uliofanyika mjini Arusha nchini Tanzania mwanzoni mwa juma, makundi ya waasi kutoka jimbo la Darfur yalihudhuria mazungumzo juu ya hatima ya jimbo hilo, na kukubaliana kufanya mazungumzo na serikali ya mjini Khartoum katika kipindi cha miezi miwili ijayo.

Katika taarifa yao ya pamoja makundi yote manane ya waasi wa Darfur yalikubaliana juu ya maswala ya usalama, ardhi, kugawana madaraka na raslimali, lakini pia usambazaji wa misaada ya kibinadamu. Maelezo ya kina hayakutolewa, lakini makundi hayo yanataka kufikia makubaliano mapya ya amani na serikali ya Khartoum.

Nalo gazeti la Neue Zürcher lilisema makundi yote ya waasi yameamua kuwa na msimamo mmoja dhidi ya serikali ya Sudan. Makubaliano hayo lakini yana kasoro kwani kiongozi wa kundi muhimu la waasi mwenye ushawishi mkubwa, Abdul Wahid Mohammed Ahmed al Nur, aliyagomea mazungumzo ya siku nne mjini Arusha nchini Tanzania.

Likitufungia mada hii gazeti la Tageszeitung lilimnukulu kiongozi wa kundi la waasi la Justice and Equality Movement, JEM, Ahmed Hussein Adam, akisema ameridhika kwamba waliweza kufikia msimamo mmoja. Mjumbe maalumu ya Umoja wa Afrika katika juhudi za kutafuta amani Darfur, Dr Salim Ahmed Salim, aliwasifu waasi kwa kusema walijitolea kwa dhati na kufanya kila waliloweza.

Mada ya pili inahusu hali ya kisiasa nchini Kenya huku uchaguzi mkuu ukikaribia nchini humo. Gazeti la Tageszeitung lilisema kwa wabunge 222 wa Kenya ni fursa ya mwisho kujipatia kiwango kikubwa cha fedha na kuhakikisha hawaipotezi nafasi hiyo, wamekuwa wakijitetea kwa bidii kubwa. Wabunge hao wanataka kujipatia shilingi milioni sita fedha zisizotozwa kodi, miezi sita kabla uchaguzi mkuu kufanyika. Kila mbunge atapata euro 64,000.

Miriam Kahiga, wa shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu, Amnesty International nchini Kenya, alinukuliwa na gazeti la Tageszeitung akisema ni aibu kubwa kwa nchi ambayo raia wake wengi wanaishi katika umaskini uliokithiri. Kwa sasa kila mbunge nchini Kenya hupokea nusu milioni kila mwezi pamoja na marupurupu mengine. Huo ni mshahara ambao kwa kila mkenya ni ndoto kubwa.

Mada ya tatu inahusu hofu ya Sierra Leone kurejea katika vita na machafuko wakati wa uchaguzi wa urais na bunge. Gazeti la General Anzeiger liliieleza hali nchini humo kabla uchaguzi kuwa ya wasiwasi. Waandamanaji wengi katika barabara za mjini Freetown walisema hali si shwari nchini humo. Ipo hofu pia kwamba polisi nchini Sierra Leone huenda ikakiunga mkono chama tawala cha SLPP na kuwachakaza wafuasi wa wagombea watakaoshindwa.

Nchi hiyo bado haijasahau yaliyotokea wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe vya miaka 11 vilivyomalizika mnamo mwaka 2002. Vita hivyo viliiharibu Sierra Leone na kusababisha vifo vya watu takriban 120,000. Raia milioni mbili walilazimika kuwa wakimbizi na maelfu wengine wakafanywa walemavu kwa kukatwa mikono, viganja na masikio na waasi wa zamani.

Tunamalizia na kusimamishwa kazi naibu waziri wa afya wa Afrika Kusini, Nozizwe Madlala Routledge. Gazeti la Neue Zürcher lilisema hatua ya rais Thabo Mbeki wa Afrika Kusini kumtimua kazini naibu waziri huyo mnamo Jumatano iliyopita, ni pigo kubwa kwa sera mpya ya kupambana na janga la ukimwi nchini humo.

Sababu ya kufutwa kazi Nozizwe Madlala ni ziara aliyoifanya nchini Uhispania mnamo mwezi Juni mwaka huu ambayo haikuidhinishwa. Lakini inashukiwa sababu halisi ya masaibu ya naibu waziri huyo ni waziri wa afya wa Afrika Kusini, Manto Tshabalala Msimang, ambaye inasemakana kwa muda mrefu amekuwa akijaribu kumfukuza mwenzake kazini. Nozizwe Madlala hakuikosoa tu sera ya ukimwi ya waziri wa afya Tshabalala, bali pia kulaani vikali hali mbaya ya hospitali mbalimbali za kiserikali.

 • Tarehe 10.08.2007
 • Mwandishi Josephat Charo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CHSB
 • Tarehe 10.08.2007
 • Mwandishi Josephat Charo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CHSB
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com