Afrika katika magazeti ya Ujerumani juma hili | Magazetini | DW | 07.09.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Magazetini

Afrika katika magazeti ya Ujerumani juma hili

Vita vyazuka upya mashariki mwa Jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo. Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon, aitembelea Sudan. Uswisi yataka kuwatuma maafisa wake wa usalama kusini mwa Sudan. Na Umoja wa Ulaya unataka mkutano wa Afrika ujadili tatizo la Zimbabwe.

Tunaanza na mapigano mashariki mwa Kongo. Gazeti la Tageszeitung lilisema mapigano makali yalizuka kati ya waasi wa jenerali Laurent Nkunda na majeshi ya serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo. Maelfu ya raia wamelazimika kuyahama makazi yao kutokana na mapigano hayo mapya.

Kwa mujibu wa ripoti za Umoja wa Mataifa katika mji mkuu wa jimbo la Kivu Kaskazini, Goma, wakaazi wote wa kijiji cha Masisi na vijiji jirani walilazimika kukimbilia maeneo mengine na wengine kwenda nchi jirani ya Uganda. Mji wa Masisi unapatikana katika milima ya Masisi ambako ni ngome ya waasi wa Laurent Nkunda.

Alhamisi iliyopita waasi wa Nkunda walijaribu kuiteka kambi ya jeshi mjini Katale na kuwalazimisha wanajeshi wa serikali kukimbia. Wadadisi wanasema kuzuka kwa mapigano mapya nchini Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo kumeanzisha vita vipya kati ya waasi wa jenerali Laurent Nkunda na majeshi ya serikali ya Kongo Kinshasa kutaka kulidhibiti jimbo la Kivu Kaskazini.

Gazeti la Frankfurter Allgemeine lilisema Laurent Nkunda anailaumu serikali ya mjini Kinshasa kwa kutaka vita na kukwamisha mazungumzo yote kuhusu njia za kuumaliza mzozo huo kwa amani. Kwa mujibu wa tume ya kulinda amani ya Umoja wa Mataifa nchini Kongo, MONUC, watu mia kadhaa wameuwawa katika mapigano mashariki mwa Kongo na ipo haja kufanya juhudi kuzuia mauaji zaidi. Inakadiriwa watu 10,000 wameyahama makazi yao wakiyakimbia mapigano.

Taarifa ya pili inahusu ziara ya katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon, nchini Sudan. Gazeti la Frankfurter Allgemeine lilisema katibu mkuu huyo aliwasili mjini Khartoum mnamo Jumatatu iliyopita kwa ziara iliyolenga kujadili kupelekwa wanajeshi na polisi 26,000 wa kulinda amani katika eneo linalokabiliwa na mzozo la Darfur. Kikosi hicho kilichoidhinishwa na baraza la usalama la Umoja wa Mataifa mnamo Julai 31 kitakuwa kikosi kikubwa kabisa duniani cha umoja huo cha kulinda amani.

Ban Ki Moon alilitembelea eneo la Darfur na mji wa Juba kusini mwa Sudan. Kiongozi huyo alikwenda Chad Ijumaa iliyopita kujadili mzozo wa Darfur na rais wa nchi hiyo, Idriss Deby.

Kuhusu ziara ya Ban Ki Moon nchini Sudan, gazeti la Suddeutsche lilisema ziara ya kiongozi huyo katika jimbo la Darfur ni kama kipindi cha masomo. Mhariri alisema kwa mara nyengine tena kiongozi huyo alitaka kuhakikisha kuwa hali ya Darfur ni mbaya kweli kama anavyoarifiwa na wajumbe wake maalumu ambao hulitembelea eneo huilo mara kwa mara.

Ukweli wa mambo bila shaka ulidhihirika kwa katibu mkuu Ban Ki Moon wakati alipojionea idadi kubwa ya wakimbizi na wanaume walivyomueleza jinsi wanavyoshambuliwa kwa mabomu na wanajeshi wa serikali ya Sudan. Wanawake kwa upande wao walimueleza matatizo ya kubakwa na uporaji wa mali.

Taarifa ya tatu inahusu ukosefu wa amani na utulivu katika jimbo la Darfur. Gazeti la Neue Zürcher lilisema mpaka sasa hakuna amani katika eneo hilo la magharibi mwa Sudan. Kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Afrika katika eneo la Darfur hakifaulu kudumisha amani katika eneo hilo. Inasubiriwa ikiwa hatua ya baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kuidhinisha kikosi kikubwa kupelekwa Darfur itafaulu kuleta amani katika eneo la Darfur.

Ripoti ya nne inahusu hatua ya Uswisi kutuma wataalamu wake wa wizara ya ulinzi kulisaidia kundi la waasi la Sudanese People´s Liberation Army, SPLA. Katika pendekezo la pamoja, waziri wa mambo ya kigeni, Micheline Calmy-Rey na waziri wa ulinzi, Samuel Schmid, nchini Uswisi, wanataka wataalamu watatu wa wizara ya usalama wapelekwe kama raia wa kawaida kutoa mafunzo kwa kundi la SPLA kuhusu sheria za kimataifa kuhusu binadamu, vita na kuyasimamia makundi yanayopigana kwa njia ya demokrasia.

Uswisi itashauriana na serikali ya mjini Khartoum na utawala wa Sudan kusini pamoja na tume ya Umoja wa Mataifa iliyo katika eneo hilo kuhusu kupelekwa kwa wataalamu hao.

Tunamalizia na mwito wa Umoja wa Ulaya kutaka mkutano wa Afrika kujadili tatizo la Zimbabwe. Gazeti la Financial Times Deutschland lilisema kamishna anayehusika na sera ya kigeni katika halmashauri ya umoja huo, Benita Ferrero-Waldner, amependekeza Umoja wa Ulaya ubadili sera zake kuelekea Afrika kwani China imepiga hatua kubwa mbele katika ushirikiano wake na bara la Afrika.

 • Tarehe 07.09.2007
 • Mwandishi Josephat Charo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CHRt
 • Tarehe 07.09.2007
 • Mwandishi Josephat Charo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CHRt